Monday, March 3, 2014

MWAKALEBELA: BUNGE KUONGEZEWA MUDA IKIWA...

Na Elvan Stambuli

MWANASIASA na mdau wa soka kijana, Frederick Mwakalebela ametabiri kuwa ikiwa malumbano ndani ya Bunge Maalum la Katiba linaloketi mjini Dodoma litaendeleza malumbano ya makundi, bunge hilo litaongezewa muda na hata kusababisha Uchaguzi Mkuu wa 2015 kusogezwa mbele.

Akizungumza na waandishi wa habari katika ofisi za gazeti hili Bamaga Mwenge jijini Dar mwishoni mwa wiki iliyopita, Mwakalebela alisema makundi ndani ya Bunge Maalum la Katiba ni tatizo ambalo anaamini Rais Jakaya Kikwete atakapolifungua rasmi hilo atalizungumzia.

Baadhi ya mahojiano kati ya Mwakalebela na waandishi wa Global ni haya yafuatayo:
Mwandishi: Makundi yameibuka bungeni, wewe ungewashauri nini wajumbe wa bunge hilo?

Mwakalebela: Ni kweli nafuatilia na hata mimi nimeliona hilo la makundi. Wajumbe wakiendeleza malumbano ya kimakundi, naamini muda waliopewa wa siku 70 hautatosha na wataongezewa siku 20 na kuwa 90. Lakini malumbano ya kimakundi nilikuwa naamini CCM (Chama Cha Mapinduzi) watakuwa kitu kimoja lakini humo namo kuna wanaopingana.

Wajumbe wale 600 waelewe kuwa wapo pale kutuwakilisha sisi zaidi ya milioni 44 tulio nje, wajue kuwa wao ni wawakilishi tu. Naamini Rais Jakaya Kikwete atakapowahutubia wakati wa ufunguzi atawaeleza hilo na atawahimiza wawe wamoja kwani jukumu kubwa la kupata katiba mpya tumewaachia wao.
Mwandishi: Mwaka 2010 wakati wa uchaguzi mkuu ulipokuwa ukigombea Ubunge Jimbo la Iringa Mjini ulikumbwa na kashfa ya kutoa rushwa kabla ya mahakama kukuona huna kosa. Unaweza kueleza ilikuwajekuwaje yakatokea yale?

Mwakalebela: Ni kweli mwaka ule upepo wa kura za maoni kwa upande wa chama changu (CCM) ulikuwa kwangu, lakini baadaye nilishitukia nikiambiwa niende nikatoe maelezo kwenye vyombo vya serikali nikayakuta hayo. Lakini kama mjuavyo mahakama iliniona sina hatia na nikaachiwa huru.

Mwandishi: Je, baada ya kutokea zahama hiyo, unasemaje kuhusu mwaka 2015, utagombea?
Mwakalebela: Kanuni za chama changu haziruhusu kwa sasa mtu kutangaza kugombea lakini niseme tu kwamba natamani kuingia katika kinyang’anyiro cha uchaguzi wa mwakani.

Ni kwamba katika maisha yangu nimesaidia watu wengi sana kulingana na uwezo wangu na wananchi wanapenda nivae koti la uongozi wakiamini kwamba nitasaidia zaidi ya hivi ninavyofanya sasa.
Mwandishi: Kabla ya kuingia katika siasa ulikuwa Katibu Mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na ukafanya vizuri kiuongozi, unaweza kutaja changamoto za wakati ule pale?

Mwakalebela: Nilikumbana na changamoto nyingi. Nakumbuka siku ya kwanza Rais wa TFF (wakati ule), Leodiger Tenga aliponitambulisha, makomandoo wa pale walisema huyu unayetuletea si mtu wa soka bali ni mwimbaji wa kwaya eti kwa sababu nilikuwa nimevaa tai. Sijui walitaka nivaaje. Lakini changamoto mojawapo ilikuwa ni kuhusu fedha zilizotokana na mapato ya milangoni.

Nilisema tuzitangaze ili wadau wajue. Tukawa tunafanya hivyo lakini wananchi wakawa hawaridhiki na tunachotangaza. Baadaye tulifanya kazi na viongozi wenzangu wa TFF wakati ule, ushirikiano na serikali ukawa mkubwa kuanzia kwa Rais Kikwete na mawaziri waliokuwa wakihusika na michezo, Seif Khatibu, Joel Bendera na baadaye Amos Makalla walituunga mkono sana.

Mwandishi: Licha ya soka na siasa kuna mengine unayoyafanya kitaifa?
Mwakalebela: Ndiyo, kwa sasa mimi ni Mtawala Mkuu wa Makumbusho ya Taifa na tumekuwa tukijitahidi kufanya kitengo hicho kinufaishe taifa.Tunataka ifanyiwe matangazo.

Hivi sasa wananchi,watu kutoka nje ya nchi wanakuja kuangalia Makumbusho ya Taifa na tunaingiza kama dola za Kimarekani 300,000 kwa mwaka.

POSTED TITLE

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...