Tuesday, February 19, 2013

PADRI EVARIST MUSHI ALIYEPIGWA RISASI KUZIKWA KESHO MJINI ZANZIBA




PADRI Evarist Mushi (55), aliyeuawa juzi kwa kupigwa risasi na watu wasiojulikana Zanzibar, anatazamiwa kuzikwa Kitope katika eneo lililotengwa la makaburi ya mapadri.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Askofu wa Kanisa Katoliki, Jimbo la Zanzibar, Augostino Shao, alisema maandalizi ya maziko yanaendelea vizuri.


“Tunatarajia kuupumzisha mwili wa marehemu Mushi katika makaburi ya Kitope ambako kuna sehemu maalumu ya kuzikwa mapadri,” alisema.

Marehemu Mushi atakuwa Padri wa tatu kuzikwa eneo hilo mkoani Kaskazini Unguja, ambako alisema kwa sasa ni mapema kujua viongozi watakaohudhuria maziko.

Akielezea jinsi alivyopokea taarifa ya kifo cha Padri Mushi, ambaye alikuwa Msaidizi wake Mkuu, Askofu Shao alisema alipokea wakati akiendesha ibada ya kawaida ya Jumapili katika Kanisa la Minara Miwili.

“Nilikuwa naongoza ibada, lakini wenzangu tayari walikuwa wamepata taarifa ya kifo cha Padri Mushi.

Nilikuwa naye asubuhi saa 12 tukaagana, naye akaenda kuongoza misa Mtoni katika Kanisa la Beit-el-Ras,” alisema.

Askofu Shao alivitaka vyombo vya ulinzi, kufanya kazi za kusaka wahalifu kwani jamii tayari imeanza kupoteza imani.

Padri Mushi aliuawa kwa risasi tatu alizopigwa kichwani na watu wasiojulikana juzi saa moja asubuhi, akienda kanisani kuongoza ibada.

Akiwa katika gari lake aina ya Toyota Hilux Surf, Padri Mushi alipigwa risasi kichwani kupitia dirisha la mlango wa kulia.

Mauaji hayo yalifanyika wakati akikata kona kuingia kanisani, ambako watu hao walikuwa wakimsubiri wakiwa na usafiri wa Vespa na baada ya kumpiga risasi walikimbia.
Kutokana na hali hiyo, gari la Padri Mushi lilipoteza mwelekeo na kupamia ukuta wa nyumba iliyo meta chache kutoka Kanisa la Mtakatifu Theresia, ambako alikuwa akienda.

No comments:

Post a Comment

POSTED TITLE

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...