Tuesday, February 19, 2013

60% WAPATA ALAMA SEFURI MATOKEO YA KIDATO CHA NNE MWAKA 2012.


Kwa ufupi
Kwa mujibu wa matokeo hayo, watahiniwa waliopata daraja la kwanza ni 1,641, wavulana wakiwa 1,073 na wasichana 568, daraja la pili ni 6,453, wavulana wakiwa 4,456 na wasichana 1,997.

Waziri wa Elimu Dk Shukuru Kawambwa.


MATOKEO ya mtihani wa kidato cha nne uliofanyika mwaka jana yametangazwa. Watahiniwa 240,903 sawa na asilimia 60.6 wamepata sifuri, huku wanafunzi 23,520 tu ambao ni sawa na asilimia 5.16 ndiyo waliofaulu na wengine 103,327 sawa na asilimia 26.02 wamepata daraja la nne.

Akitangaza matokeo hayo jana, Waziri wa Elimu Dk Shukuru Kawambwa alisema watahiniwa walikuwa 456,137, wa shule wakiwa 397,136 huku wa kujitegemea wakiwa 68,806.
“Matokeo ya mwaka huu yamekuwa mabaya sana, Serikali tunasikitika kutokana na hali hii lakini tuna mipango mbalimbali ya kuhakikisha tunaweza kutatua hili tatizo,” alisema Dk Kawambwa.

Dk Kawambwa alisema watahiniwa wote kwa ujumla waliosajiliwa walikuwa 480,036 kati yao wasichana 217,583 sawa na asilimia 45.33 na wavulana 262,453 sawa na asilimia 54.67 lakini waliofanya mtihani huo ni 456,137 sawa na asilimia 95.44, wengine 21,820 (asilimia 4.55) hawakufanya mtihani.

Alisema watahiniwa wa shule (school candidates) walikuwa 397,136 sawa na asilimia 96.57, miongoni mwao, 14,090 sawa na asilimia 3.43 hawakufanya mtihani huo kutokana na sababu mbalimbali zikiwamo utoro, ugonjwa na vifo.

Ufaulu kwa madaraja
Kwa mujibu wa matokeo hayo, watahiniwa waliopata daraja la kwanza ni 1,641, wavulana wakiwa 1,073 na wasichana 568, daraja la pili ni 6,453, wavulana wakiwa 4,456 na wasichana 1,997.

Waliopata daraja la tatu ni 15,426, wavulana 10,813 na wasichana 4,613, waliopata wa daraja la nne 103,327, wavulana 64,344 na wasichana 38,983 huku waliopata sifuri wakiwa 240,903, wavulana 120,664 na wasichana 120,239.

Shule 20 bora
Katika hali isiyokuwa ya kawaida, wizara ilitaja shule 20 zilizofanya vizuri badala ya 10 kama ilivyozoeleka, kati yake 18 zilikuwa za watu binafsi na mashirika ya dini na mbili za Serikali.

Shule hizo ni pamoja na St.Francis Girls ya Mbeya, Marian Boys ya Pwani, Feza Boys ya Dar es Salaam, Marian Girls ya Pwani, Rosmini ya Tanga, Canossa ya Dar es Salaam, Jude Moshono ya Arusha, St. Mar’s Mazinde Juu ya Tanga, Anwarite Girls ya Kilimanjaro na Kifungilo Girls ya Tanga.

Nyingine ni Feza Girls ya Dar es Salaam, Kandoro Sayansi Girls ya Kilimanjaro, Don Bosco Seminary ya Iringa, St. Joseph Millenium ya Dar es Salaam, St. Iterambogo ya Kigoma, St. James Seminary ya Kilimanjaro, Mzumbe ya Morogoro, Kibaha ya Pwani, Nyegezi Seminary ya Mwanza na Tengeru Boys ya Arusha.

Shule 10 za Mwisho
Kwa upande wa shule 10 za mwisho, iliyofanya vibaya zaidi ni Mibuyuni ya Lindi, Ndame ya Unguja, Namndimkongo ya Pwani, Chitekete ya Mtwara, Maendeleo ya Dar es Salaam, Kwamndolwa Tanga, Ungulu Morogoro, Kikale ya Pwani, Mkumba na Tongoni za Tanga.

Matokeo yaliyofutwa
Jumla ya watahiniwa 789 wamefutiwa matokeo kwa sababu mbalimbali ikiwa ni pamoja na udanganyifu na kuandika matusi.

Baadhi ya udanganyifu huo ni karatasi za majibu kuwa na mfanano usio wa kawaida, kukamatwa na simu za mkononi kwenye chumba cha mtihani, kukutwa na karatasi au madaftari pamoja na kubadilishana karatasi za majibu.

Dk Kawambwa alisema matokeo ya watahiniwa 28,582 yamezuiwa kwa sababu ya kutolipa ada ya mtihani na wanatakiwa kulipa fedha hizo ndani ya mwaka mmoja.

Matokeo ya QT
Dk Kawambwa alisema waliosajiliwa kufanya Mtihani wa Maarifa (QT) walikuwa 21,310, wasichana 13,134 na wavulana 8,176 na waliofanya ni 17,137 sawa na asilimia 80.42... “Watahiniwa 5,984 kati ya 17,132 waliofanya mtihani huo wamefaulu.”

No comments:

Post a Comment

POSTED TITLE

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...