Monday, February 15, 2016

UKWELI WA TAJIRI ALIYE AUAWA NA MAMACHINGA HUU HAPA!

Mchumba wa tajiri huyo kiuaga mwili wa mpendwa wake.
Mchumba wake akiwa amezimia.

Stori: Makongoro Oging’, Uwazi
DAR ES SALAAM: Inauma sana! Mfanyabiashara mkubwa wa Kariakoo jijini Dar, Stephen Elija Silas (27) ameuawa kwa kupigwa mawe na wafanyabiashara wadogowadogo ‘Wamachinga’ kwa madai ya kukanyaga kwa gari lake nyanya walizopanga barabarani, Uwazi limefuatilia.

Tukio hilo lenye simulizi ya kusikitisha lilijiri usiku saa nne ya Februari 8, mwaka huu katika makutano ya Mtaa wa Msimbazi na Aggrey, Kariakoo jijini Dar es Salaam wakati marehemu huyo alipokuwa akilikwepa gari lililobeba maziwa.
Marehemu Stephen alikuwa akiendesha gari lake aina ya Toyota Corolla lenye namba za usajili T 312 AZU ambalo pia lilipondwa kwa mawe na Wamachinga. Alikuwa njiani kuelekea nyumbani kwake, Kinondoni, Dar.

Marehemu Stephen na mchumba wake.

MBALI NA MAWE, ALICHOMWA KISU
Taarifa zaidi zinadai kuwa, mbali na marehemu huyo kupigwa mawe, pia Wamachinga hao walimchoma kisu kwenye kwapa la mkono wa kulia akiwa ndani ya gari.

SHUHUDA ASIMULIA
Mmoja wa mashuhuda wa tukio hilo ambaye hakupenda jina lake liandikwe gazetini alisema marehemu alikuwa akitokea upande wa uliyokuwa mzunguko wa Shule ya Uhuru, akaingia Barabara ya Msimbazi. Alipofika makutano ya mtaa huo na Aggrey, mbele yake kulikuwa na gari lililobeba maziwa ambalo liliyumba, hivyo ili asiligonge akalikwepa na hivyo kujikuta akikanyaga kwa bahati mbaya nyanya za Wamachinga hao ambao palepale walianza kumshambulia kwa maneno, baadaye mawe na kumalizia na kisu.

WALICHANGANYIKA NA WAHUNI
“Jitihada za wasamaria wema kumuokoa zilishindikana licha ya jamaa kuomba msaada. Mimi naamini kuwa, mbali na Wamachinga pia wahuni wa mitaani walikuwepo kwa lengo la kupora vitu vyake,” kilisema chanzo hicho.

ALIOMBA MSAMAHA
Chanzo: “Kwanza jamaa alipobaini amekanyaga nyanya za biashara ya Wamachinga hakufanya fujo kwa kunena mabaya, aliomba asamehewe au alipe fedha kulingana na nyanya zilizoharibika lakini Wamachinga na wahuni hao hawakumsikiliza, waliendelea kumwadhibu.
“Kulikuwa na wananchi waliokuwa wakitokwa machozi walipomuona jamaa akipigwa mawe kwa kosa ambalo halina kichwa wala miguu.”

WANANCHI WAPIGA SIMU POLISI
Inaelezwa kuwa, baadhi ya wananchi waliamua kupiga simu Kituo cha Polisi Msimbazi ili wakamuokoe Stephen lakini licha ya kuwahi katika eneo la tukio, walimkuta akiwa hoi kutokana na kipigo na alifariki dunia wakati polisi wakimkimbiza Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa matibabu.

UWAZI LAFIKA MSIBANI
Uwazi kama ada yake, lilifika kwenye msiba wa Stephen, kwa baba yake mkubwa marehemu aitwaye Charles Losaru, Mtoni Kijichi jijini Dar na kuzungumza na mdogo wa marehemu aliyejitambulisha kwa jina la Rebeca Elija ambaye alisema alikuwa na marehemu muda mfupi kabla ya kifo chake. Alikuwa na haya ya kusema:
“Marehemu kaka Stephen alikuwa mfanyabiashara mwenye maduka ya bidhaa mbalimbali, Kariakoo na Sinza. Huwa ana kawaida ya kutusindikiza na gari lake baada ya kufunga maduka. Mimi na ndugu zangu wengine tunaishi Kitunda yeye Kinondoni. Amekuwa akitusindikiza hadi Banana na kutuacha tupande daladala.

Ndugu wa marehemu akiwa amezimia.

“Siku ya tukio, alitusindikiza na kutuacha Buguruni. Ilikuwa saa tatu usiku. Ni sisi tuliamua atuache hapo badala ya Banana. Yeye akarudi akipitia Kariakoo kwa vile kuna ndugu zetu wengine wana maduka maeneo hayo.”

SIMU YAKE YAPIGWA, YAITA TU!
Rebeca anaendelea: “Tuliposhuka kwenye daladala pale Banana, nilimpigia simu mara tatu ikawa inaita bila kupokelewa. Nikampigia simu mchumba wake, anaitwa Neema William ambaye ilikuwa wafunge ndoa hivi karibuni. Nilitaka kujua kama kaka alishafika nyumbani, Neema akasema hajafika.

TAARIFA ZA KIFO KWA NDUGU
“Sasa wakati tunapanda daladala Banana kwenda Kitunda, nilipigiwa simu na marafiki zake na kuniambia kuwa Stephen amepata matatizo yupo Muhimbili. Niliposhuka Kitunda, alinipigia simu kaka yangu mkubwa, anaitwa Silas ambaye tulikuwa naye Kariakoo, akaniambia kaka amefariki dunia (machozi).

“Kaka Stephen alikuwa mpole kupita kiasi! Hivi ni kwa nini walimuua kikatili vile? Kwanza pale walipompigia mawe, mbona ni sehemu ya magari na wala si pa kupanga nyanya wala bidhaa nyingine. Inaniuma sana (machozi tena).”

MAREHEMU AAGWA DAR, AZIKWA ARUSHA
Mwili wa marehemu Stephen uliagwa Alhamisi ya wiki iliyopita katika Kanisa la Anglikana lililopo Muhimbili na kusafirishwa kwenda nyumbani kwao, Daraja Mbili mkoani Arusha kwa mazishi yaliyofanyika Ijumaa iliyopita.

POLISI WAZUNGUMZIA
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ilala, ACP Ernest Matiku alipohojiwa na Uwazi ofisini kwake wiki iliyopita, alikiri kutokea kwa tukio hilo na kueleza kuwa, marehemu alipigwa na kundi la watu baada ya kugonga gari lililokuwa likiuza maziwa kisha kukanyaga bidhaa za Wamachinga zilizokuwa zimepangwa chini.

Gari likiwa limehalibika vibaya.

“Mpaka sasa tunawashikilia watu kumi kutokana na tukio hilo na bado upelelezi unaendelea. Kwa sasa hakuna biashara ya Wamachinga inayoendelea maeneo yale ya Mtaa wa Msimbazi.
“Nalaani kitendo kile cha mauaji kwani hata kama marehemu alifanya kosa lakini sheria zipo na siyo kuchukua maamuzi hayo mazito ya kukatisha maisha ya binadamu, wote waliofanya unyama ule watashughulikiwa kisheria upelelezi ukikamilika,” alisema kamanda huyo.

No comments:

Post a Comment

POSTED TITLE

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...