Tuesday, February 23, 2016

KESSY APIGIWA SIMU ZA VITISHO NA BAADHI YA WADAU WA SIMBA KISA MECHI YA WATANI!

Beki wa kulia wa timu ya Simba, Hassan Kessy


BEKI wa pembeni wa Simba, Hassan Kessy, wikiendi iliyopita aliimaliza vibaya baada ya kupokea simu nyingi za mikwara na vitisho akilaumiwa kutokana na kuifungisha timu hiyo ilipovaana na Yanga.
Katika mechi hiyo iliyomalizika kwa Yanga kushinda mabao 2-0, beki huyo alisababisha bao la kwanza dhidi ya timu yake, baada ya kumrudishia pasi fupi kipa wake, Muivory Coast, Vincent Angban ambayo ilinaswa na Donald Ngoma na kufunga katika dakika ya 39.

Kosa hilo, lilionekana kuwakera mashabiki wa Simba waliokuwepo uwanjani hapo na kumtolea lawama beki huyo ambaye alikuwa ameonyesha kiwango kizuri kwenye michezo saba iliyopita.
Akizungumza na Championi Jumatano, Kessy alisema kuwa tangu mechi hiyo ya Yanga imalizike, anapata usumbufu mkubwa kutoka kwa mashabiki ambao kila wakati wanampigia simu na kumtumia meseji za mikwara na vitisho.
Kessy alisema, anashangaa kuona mashabiki hao wakiendelea kumpigia simu na kumtumia meseji, licha ya kuwaomba msamaha kwa makosa hayo aliyoyafanya.

Aliongeza kuwa, kikubwa anachokifanya yeye hivi sasa ni kukaa kimya ili kuepusha matatizo mengine kwa faida yake na badala yake anaendelea kutimiza majukumu yake ya ndani ya uwanja akiwa na Simba.
“Mchezo wa soka ni wa uvumilivu sana na hadi hapa nilipofikia kukaa kimya kugombana na shabiki yeyote nimejitahidi kutokana na simu ninazopigiwa na meseji ninazotumiwa na mashabiki wa Simba.
“Wengi wao wanaonipigia simu na kunitumia meseji, wanalalamika kuwa mimi nimesababisha tufungwe baada ya kufanya kosa la kurudisha pasi fupi kwa kipa kabla ya Ngoma kufunga.
“Kikubwa wanachotakiwa kukifahamu ni kuwa, soka ni mchezo wa makosa ambayo mimi niliyafanya na kusababisha tufungwe bao moja katika kipindi cha kwanza, ninaomba nichukue nafasi hii kuwaomba radhi Wanasimba wote,” alisema Kessy.
Aidha, alipotafutwa meneja wa mchezaji wa timu hiyo, Athumani Tippo kuzungumzia suala hilo, kwanza kabisa alikiri kuwepo na taarifa hizo za mchezaji wake kutishiwa maisha na mashabiki wa Simba.
“Hizo taarifa za kweli kabisa, mchezaji wangu wanamtumia meseji na kumpigia simu za vitisho, hivyo hivi sasa nimepanga kukutana na mwanasheria wangu ili kuhakikisha sheria inachukua mkondo wake,” alisema Tippo.

No comments:

Post a Comment

POSTED TITLE

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...