Wednesday, July 22, 2015

Yanga: Lazima tuwachinje

Wachezaji wa Yanga wakishangilia goli.
Waandishi Wetu, Dar es Salaam
YANGA leo inatarajiwa kujitupa Uwanja wa Taifa kuvaana na Telecom FC ya Djibouti katika mchezo wa pili wa Kombe la Kagame. Ni lazima wawachinje .
Yanga wanatakiwa kuhakikisha wanapata ushindi kwenye mchezo huu baada ya kupoteza mchezo wa kwanza dhidi ya Gor Mahia na kama wakipoteza na huu, basi watakuwa wamejiweka kwenye mazingira magumu sana.

Kwa sasa Yanga wanaburuza mkia pamoja na Telecom kwenye Kundi A huku kila moja ikiwa haina pointi.
Gor Mahia wameshafuzu hatua ya robo fainali wakiwa na pointi sita na wanafuatiwa na KMKM ambao wana pointi tatu.
Kutokana na hali hiyo, Yanga inalazimika kuingia uwanjani ikiwa na hasira ikitaka kujiweka sawa kwa kushinda mchezo huo na angalau kufufua matumaini yake. Ikitoka sare au kufungwa ni tatizo kubwa kwao.
Kulingana na msimamo ulivyo na changamoto waliyonayo Yanga kwenye kundi lao, inawalazimu kuibuka na ushindi katika mchezo huo ili wakae sawa mapema kuliko kupoteza tena au kutoa sare ambako kutawafanya kuambulia pointi moja na kuzidi kudidimia au kuwanyong’onyeza zaidi katika kusaka tiketi ya kutinga robo fainali.
Kwa nini lazima ishinde?
Pamoja ya kwamba Yanga ni lazima kushinda ili ikae sawa na kuzidi kusonga mbele, lakini ukubwa na umaarufu wa timu hiyo katika michuano hiyo ambayo waliwahi kubeba ndoo mara tano, pia unawasuta na kuwapa msukumo wa kufanya vema na kuendelea kulinda hadhi yao.
Lakini kingine, inasadikika kuwa ni kati ya timu chache zilizofanya usajili wa mamilioni ya pesa katika timu shiriki za Kagame msimu huu.
Tatizo lililoonekana Yanga
Yanga inaonekana kukamilika kila idara lakini katika mechi yao ya kwanza pekee ilionekana kuwa na tatizo la kuzuia na kumiliki mipira kutokea katikati ya uwanja, eneo ambalo anatumika zaidi katika majukumu hayo, Mnyarwanda Mbuyu Twite.
Twite amekuwa nguzo kubwa kwa Yanga kwa takriban misimu mitatu mfululizo sasa kutokana na ufanisi wa kazi zake uwanjani lakini anaonekana kuchoka na kushindwa kufanya vizuri kwenye nafasi ya kiungo mkabaji.
Katika hilo, kocha Hans van Der Pluijm, anahitaji upembuzi yakinifu na utatuzi wa haraka wa nafasi hiyo.
Kauli ya Pluijm“Tumepoteza mchezo wa kwanza, nafikiri kadi nyekundu na kukosa penalti vilichangia, lakini tulifungwa pia na moja ya timu bora hapa Afrika Mashariki.
“Lakini tunafahamu kuwa tuna michezo mingine mbele ukiwemo huu unaofuata wa Telecom, hivyo tutahakikisha tunarekebisha makosa na kushinda katika michezo iliyobaki na hatimaye tusonge mbele na kutimiza azma tuliyonayo, mashabiki waje uwanjani, wasikate tama,” alisema Pluijm.
Telecom imeruhusu mabao sita hadi hivi sasa katika mechi mbili walizocheza tangu michuano ya Kagame imeanza dhidi ya KMKM ambayo walifungwa bao 1-0 na mchezo mwingine dhidi ya Khartoum wakafungwa 5-0.
Kikosi
Taarifa ambazo Championi imezipata zinasema Pluijm amepanga kuwatumia washambuliaji wake, Malimi Busungu, Amissi Tambwe pamoja na Kpah Sherman kwa ajili ya kuhakikisha wanaziba pengo la Donald Ngoma ambaye atakuwa nje akitumikia kadi nyekundu.

POSTED TITLE

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...