VITA! Saa chache tu baada ya kutua kwenye Uwanja wa Ndege wa
Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), Dar akitokea nchini Marekani kwa
shughuli za kimuziki, staa wa Bongo Fleva, Ali Saleh Kiba ametangaza
kile kinachotafsirika kuwa ni vita dhidi ya hasimu wake kwenye anga la
muziki huo, Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’, Ijumaa Wikienda lina ‘full’ stori.
TUJIUNGE ENEO LA TUKIO
Ali Kiba alitema cheche Alhamisi ya wiki iliyopita ndani ya Hoteli ya
Sea Cliff, Masaki jijini Dar, kulikokuwa na uzinduzi wa kampeni ya
kupinga vita ujangili, iliyoratibiwa na Wizara ya Maliasili na Utalii,
huku akiwa ni mmoja wa mabalozi sanjari na mlimbwende wa zamani,
Jacqueline Ntuyabaliwe Mengi ‘K-Lyin’.
USO KWA USO NA PAPARAZI
Baada ya shamrashamra za ‘event’ hiyo, haraka sana kama mshale wa
Mmakonde, mwandishi wetu alimfuata Ali Kiba, lengo kuu likiwa ni kusikia
chochote juu ya ushindi wa Tuzo za Kili ambapo alizoa tano binafsi na
moja ya kushirikishwa.
Kiba alisema anaamini alistahili kushinda tuzo zote kwani vigezo na
sifa anazo na amejiandaa kikamilifu kupambana na yeyote anayedhani kuwa
ni mfalme wa muziki huo.
JINA LA DIAMOND LAMCHEFUA!
Katika
mahojiano hayo, mwandishi wetu alimkumbusha Ali Kiba uwepo wa Diamond
ambapo kwa haraka sana alimkata kauli mwandishi kwa kusonya na kuweka
wazi kuwa miongoni mwa mambo ambayo humpa kichefuchefu, ni pamoja na
kusikia jina la Diamond likitajwa mahali popote penye uwepo wake!
“Kaka, sitaki kabisa kulisikia jina hilo, linanipa kichefuchefu,
unajua kwa kipindi ambacho nilikaa kimya, nilikuwa nausoma mchezo lakini
hakuna aliyeweza kuchukua kiti changu na kuamua kurejea ulingoni kwa
kishindo na kuanzia sasa hivi ni mapambano mwendo mdundo,” alisema Kiba
na kuongeza:
“Simaanishi kuwa hakuna msanii mzuri kama mimi, naomba nisieleweke
vibaya, wapo lakini siyo huyo dogo (Diamond), muziki ni zaidi ya
mbwembwe, niko kikazi na sasa nimedhamiria kweli, kama anaamini yuko
fiti, kazi zitaweka wazi ukweli na si drama za kitoto.”
VIPI KUHUSU YEYE NA WEMA?
Mwandishi wetu alitaka kujua kulikoni msanii huyo alimuweka Wema
Sepetu kwenye ukurasa wake wa Instagram akimmwagia shukrani lukuki na si
mtu mwingine?
“Wema amekuwa ni shabiki wangu wa siku nyingi mno, alianza kunipenda
kupitia wimbo wangu wa Hands Across the World (kwenye Project ya
One-Eight) na kuanzia hapo amekuwa akinipa sapoti kubwa sana, siwezi
kukaa naye mbali eti kisa huyo jamaa (Diamond).
“Naamini kwa asilimia nyingi sana hata huu ushindi wangu wa tuzo,
umechangiwa na sapoti yake pamoja na wadau wangu wengine,” alisema Kiba.
AFUNGUKA KUHUSU VIDEO YA MWANA!
Pia, mwandishi wetu alimtaka staa huyo kufafanua madai ya kutoitendea
haki video ya Wimbo wa Mwana, ambapo alisema, watu wengi walitarajia
aifanye kulingana na mawazo yao ndiyo maana akaamua afanye vile
anavyoaamini ingekuwa bora.
“Kila mtu alikuwa ameshatengeneza picha ya jinsi video ya wimbo
itakavyokuwa, halafu sifanyi kazi kwa kushindana na mtu, ndiyo maana
ilionekana tofauti na mawazo ya wengi, namalizia kwa kusema salamu
zimfikie jamaa (Diamond) kuwa mapambano ndiyo kwanza yameanza,” alisema
Kiba.
DIAMOND ANASEMAJE?
Hadi tunakwenda mitamboni, jitihada za kumpata Diamond aweze
kuzungumzia vita hiyo iliyofufuka upya hazikuzaa matunda kufuatia simu
ya staa huyo aliyekuwa nchini Afrika Kusini kikazi, kuita bila majibu.
TUJIKUMBUSHE
Kwa muda mrefu sasa, Kiba na Diamond wamekuwa wakiripotiwa kuwa na
bifu la chini kwa chini linalotokana kugombania ufalme wa muziki Bongo.
No comments:
Post a Comment