Thursday, March 26, 2015

TUZO ZA WATU ZAJA KIVINGINE, VIPENGELE VYAONGEZEKA

 Mhariri mkuu wa Bongo5  Bw. Fredrick Bundara akiwa pamoja  na mwariri msaidizi, Sandu George wakizungumza leo na waandishi wa habari  katika uzinduzi wa Tuzo za watu 2015
 Mhariri mkuu wa Bongo5  Bw. Fredrick Bundara akiwa pamoja  na mhariri msaidizi, Sandu George wakizungumza leo na waandishi wa habari  katika uzinduzi wa Tuzo za 
watu 2015
Kampuni ya Bongo5 Media Group,  imezindua msimu mpya na wa pili wa Tuzo za Watu Tanzania zilizoanzishwa mwaka jana ili kuwatuza watu kwenye sekta ya burudani na habari wanaofanya vizuri.
Akiongea kwenye mkutano na waandishi wa habari leo, mhariri mkuu wa mtandao wa Bongo5, Fredrick Bundala amesema tuzo za mwaka huu zimeboreshwa zaidi kwa kuongeza vipengele vitatu vipya.
“Mwaka huu tuzo zimeongezewa nguvu zaidi. Kutoka vipengele 11 tulivyokuwa navyo mwaka jana hadi vipengele 1. Mwaka huu tumeongeza vipengele vitatu muhimu,” amesema Bundala.
Amevitaja vipengele vilivyoongezeka kuwa ni pamoja na muongozaji wa filamu anayependwa, tovuti/blogu inayopendwa na mfadhili maarufu anayependwa.
“Kwenye jamii yetu kuna watu maarufu ambao wamekuwa mstari wa mbele kusaidia jamii hususan watu wasio na uwezo ama wanaoshi katika mazingira magumu. Tumeona ni muhimu pia kuwatambua watu hawa ambao huamua kujinyima na kugawana kile wanachokipata ili kuwasaidia watu wanaohitaji msaada,” ameongeza.
Amesema zoezi la kuanza kupendekeza majina ya washiriki limeanza rasmi Alhamis hii ambapo wananchi wanaweza kuwapendekeza kupitia website ya www.tuzozetu.com ama kwa njia ya ujumbe mfupi wa simu kwa kuandika neno TZW, code ya kila kipengele na jina la anayependekezwa kwenda 15678.
“Baada ya wiki tatu kuanzia leo tutatangaza majina ya washiriki watano waliochaguliwa kuingia kwenye awamu ya kwanza ya mchujo ambapo katika kipindi cha wiki mbili itafanyika michujo mingine miwili ili kuwapata washiriki watatu watakaoingia fainali,” amesisitiza Bundala.
“Washiriki watatu kwenye kila kipengele watahudhuria kilele cha tuzo hizo kitakachofanyika katikati ya mwezi wa tano.”
Kwa upande wake mhariri msaidizi wa Bongo5,  Sandu Mpanda, amesema kuwa utofauti wa tuzo za watu na tuzo zingine ni kuwa wananchi wana nguvu ya asilimia 100 kumchagua mshindi.
“Kura za wananchi ndizo zitakazompata mshindi. Ni muhimu wananchi kuwapigia kura watu wanaowapenda ili kuhakikisha wanashinda vipengele walivyotajwa kuwania,” amesema Mpanda.
Mpanda amevitaja vipengele vinavyowaniwa kwenye tuzo za mwaka huu kuwa ni pamoja na Mtangazaji wa redio anayependwa (TZW1), Kipindi cha redio kinachopendwa (TZW2), Mtangazaji wa kipindi cha runinga anayependwa (TZW3), Kipindi cha runinga kinachopendwa (TZW4), Tovuti/Blogu inayopendwa (TZW5) na Muongozaji wa video za Muziki anayependwa (TZW6).
Vingine ni Muongozaji filamu anayependwa (TZW7), Mwigizaji wa kike anayependwa (TZW8), Mwigizaji wa kiume anayependwa (TZW9), Mwanamuziki wa kike anayependwa (TZW10), Mwanamuziki wa kiume anayependwa (TZW11), Filamu inayopendwa (TZW12), Video ya Muziki inayopendwa (TZW13) na Mfadhili maarufu (TZW14).
Hashtag za kwenye mitandao ya kijamii mwaka huu ni #TZW2015 na #TuzozaWatu.



No comments:

Post a Comment

POSTED TITLE

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...