WAKATI joto likizidi kupanda kuhusu nani atapeperusha bendera
ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika uchaguzi mkuu ujao, siri imevuja
kuwa upande wa pili, yaani upinzani unaoundwa na vyama vinavyojinasibu
kuwa ni Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) utamsimamisha mgombea wake
ambaye kwa sasa ni kada mwenye wafuasi wengi ndani ya CCM, Uwazi
Mizengwe linakujuza.
Habari za kuaminika kutoka ndani ya kambi ya Ukawa inayoundwa na
vyama vya Chadema, Cuf, NCCR-Mageuzi na NLD, zinasema kwa muda mrefu,
mgombea huyo amekuwa katika mazungumzo na chama kimoja kikubwa cha
upinzani Tanzania Bara na kwamba wameshakubaliana mambo makubwa muhimu
ya kuzingatiwa ili kukamilisha mchakato huo.
Inadaiwa kuwa awali mazungumzo yalikuwa kati ya Chadema na kada huyo
wa CCM ambaye ni miongoni mwa viongozi waliopewa adhabu na kamati kuu
(CC) ya chama hicho kwa kosa la kuanza mapema kampeni za kuwania kiti
hicho, wakifikia makubaliano kuwa endapo chama chake kitamuengua katika
kuwania nafasi hiyo, basi afanye hivyo kupitia chama hicho lakini kwa
sharti la kugawana vyeo yeye na wafuasi atakaoondoka nao.
“Kambi ya kada huyo ina hofu ya mzee wao kukatwa kutokana na mizengwe
inayosukwa na wapinzani wake ndani ya chama. Kwa kuwa ni lazima mtu wao
awanie urais, basi wameamua kuweka mbadala. Vikao vimefanyika na
walifikia hatua nzuri kwa sababu wanaamini endapo mgombea huyo ataondoka
CCM na kujiunga kule wana uhakika wa kupata kura nyingine zikitoka hata
kwa wafuasi wa chama hicho tawala,” alisema mtoa habari wetu.
Inadaiwa kuwa awali, kulikuwa na hofu ya mpango huo kuharibika baada
ya Chadema kujiunga na vyama vingine vya upinzani na kuunda Ukawa, ambao
wametangaza kumweka mgombea mmoja atakayekubaliwa na pande zote, lakini
imeelezwa kuwa mazungumzo yanaendelea na upo uwezekano mkubwa wa mpango
huo kukubaliwa na viongozi wa vyama vingine kutokana na nguvu kubwa ya
ushawishi iliyonayo chama hicho.
“Kwa jinsi alivyo na wafuasi wengi ndani ya CCM na vuguvugu la
mabadiliko linalosubiri uchaguzi wa mwaka huu, kuna uwezekano mkubwa wa
kushinda kupitia Ukawa. Kada huyo ametaka kuwekewa nafasi kadhaa katika
serikali itakayoundwa na makubaliano yamefikiwa juu ya vyeo ambavyo watu
wa Ukawa watapata katika serikali inayotarajiwa kuundwa,” kilisema
chanzo hicho.
Kwa mujibu wa mtoa habari wetu, baadhi ya nafasi ambazo Ukawa
wametaka kupewa ni ile ya mgombea mwenza (atakayekuwa makamu wa rais),
waziri mkuu, wizara ya fedha, wizara ya sheria, wizara ya mambo ya
ndani, wizara ya ulinzi, wizara ya nishati na madini, wizara ya ujenzi
na uchukuzi pamoja na nyingine nyeti ambazo zinadaiwa kuwa ndiyo uti wa
mgongo wa uchumi wa nchi.
“Wanaamini wakizikamata wizara hizo, basi wanao uwezo wa kubadilisha
mambo na hivyo kuonesha tofauti kati ya uongozi wao na ule wa CCM.
Ninavyokueleza hivi, vikao bado vinaendelea kwa sababu kila upande
unataka kujiridhisha kabla ya kufikia makubaliano rasmi,” kilisema
chanzo hicho.
Juzi, Uwazi Mizengwe lilimtafuta Naibu Katibu Mkuu wa Chadema
Tanzania Bara, John Mnyika kupitia simu yake ya mkononi na kumuuliza
kuhusu mipango hiyo lakini alikataa katakata kuwepo kwa suala hilo
akidai ni uvumi ambao hauna ukweli wowote.
“Huo uvumi hauna ukweli, mgombea wa Ukawa atatoka Ukawa. Wananchi
wana imani na Ukawa na siyo mtu kutoka chama kilichoshindwa kujivua
magamba ya ufisadi na kuwa chama cha mafisadi,” alisema Mnyika ambaye
pia ni mbunge wa Ubungo kwa tiketi ya Chadema.
Alipoulizwa kama Ukawa watakuwa tayari kumpokea kada wa CCM mwenye
wafuasi wengi kwa kigezo cha kuongezewa kura katika uchaguzi huo na
kumpa nafasi ya kuwania urais, Mnyika alisema milango ipo wazi kwa
kiongozi yeyote mwenye maono na maadili ambaye atakuwa tayari kumuunga
mkono mgombea atakayeteuliwa na Ukawa, siyo mwenye uzoefu wa ufisadi na
uongozi mbovu.
“Tayari Ukawa ina wafuasi wengi ambao wakiungana na wananchi wengine
wasio na vyama lakini wapenda mabadiliko wanatosha kuiondoa CCM
madarakani, lakini kama yupo mwenye maono na maadili aliye tayari
kujiunga na Ukawa toka CCM ili kuongeza kura za mabadiliko aje, lakini
nasisitiza, awe na uadilifu na uwezo siyo uzoefu wa ufisadi.”
Kwa upande wake, Katibu wa Itikadi, Uenezi wa Halmashauri Kuu ya CCM,
Nape Moses Nnauye alipoulizwa juu ya suala hilo alipuuza na kusema ni
porojo za mtaani ambazo CCM haishughuliki nazo.
Makada wa CCM wanaotajwa kuwa na nguvu katika chama hicho ambao pia
wanatumikia adhabu ya kuanza kampeni mapema ni pamoja na Emanuel
Nchimbi, Edward Lowassa, William Ngeleja, January Makamba, Steven
Wassira na Bernard Membe. Wengine ambao hawako kwenye adhabu ni Mizengo
Pinda, Hamis Kingwangalla na Lazaro Nyalandu.
No comments:
Post a Comment