LIKUWA kama kitu cha ajabu baada ya mastaa wa fani mbalimbali nchini
hasa wa muziki na filamu, kutangaza nia zao za kujiingiza kwenye masuala
ya siasa ambapo mpaka sasa mastaa kama Profesa Jay na Afande Sele
wameweka wazi nia zao huku mastaa kama Joseph Mbilinyi ‘Sugu’ ambaye ni
Mbunge wa Mbeya Mjini na Vicky Kamata ambaye ni Mbunge wa Viti Maalum
wakiwa ni baadhi ya mastaa waliotinga bungeni tangu uchaguzi uliopita.
Bongo siyo nchi pekee ambayo suala hilo limejitokeza, bali hata
kwenye nchi mbalimbali za Afrika, Ulaya na Marekani limewahi kutokea
ambapo kwa nyakati tofauti mastaa wakubwa wamewahi kujitokeza kuwania
nafasi mbalimbali huku wengine wakishindwa na wengine kushinda nafasi za
kuwakilisha wananchi katika nyadhifa mbalimbali. Wafuatao ni baadhi ya
mastaa wakubwa wa majuu ambao wamewahi au wanaendelea kushiriki kwenye
siasa:-
ARNOLD SCHWARZENNEGGER
Huyu ni staa mkubwa wa
filamu za ‘action’ nchini Marekani ambaye anajulikana sana kwa umbo lake
kubwa. Jamaa alianza kama mtunisha misuli na kuingia kwenye tasnia ya
filamu ambapo alifanya vema na muvi zake kama Terminator na Predator.
Arnold alianza siasa mwaka 2003 ambapo aligombea ugavana wa Jimbo la
Calfornia na kushinda, alishikilia nafasi hiyo hadi mwaka 2011.
ANDRIY CHEVSHENKO
Ni msakata kabumbu raia wa
Ukraine ambaye alipata mafanikio makubwa katika historia ya soka duniani
ambapo alichezea klabu kubwa duniani kama AC Milan na Chelsea.
Alitangaza kustaafu mwaka 2012 baada ya kucheza soka kwa muda mrefu.
Baada ya kustaafu alijiunga na Chama Cha Demokrasia cha Ukraine
akigombea nafasi ya ubunge, hata hivyo alishindwa kupata nafasi hiyo
kutokana na ushindani mkubwa uliojitokeza.
WYCLEF JEAN
Ni staa wa muziki toka Marekani
aliyehamia nchini humo akiwa na familia yake kama wakimbizi waliotokea
nchini Haiti. Jamaa aliwika na ngoma zake kama 911, Two Wrongs na Hips
Don’t Lie aliyoshirikiana na Shakira. Jamaa alijitosa kwenye siasa mwaka
2010 akitangaza kugombea nafasi ya urais katika nchi yake ya kuzaliwa
ya Haiti ambapo hata hivyo alitolewa kwenye kinyang’anyiro hicho
kutokana na sababu za makazi yaani kuishi Marekani zaidi kuliko Haiti.
YOUSSOU N’DOUR
Huyu ni staa mkubwa zaidi Afrika
ambaye anatajwa kushika namba moja kwenye orodha ya wasanii wa muziki
matajiri Afrika huku Jarida la Rollingstone likimtaja kama mwanamuziki
anayejulikana sana Afrika.
Mwanamuziki huyu anayejulikana Afrika na
duniani kwa kibao chake cha Dirima, alitangaza nia ya kugombea urais
mwaka 2012 lakini akatolewa kwenye kinyang’anyiro hicho kutokana na
saini za wadhamini wake kuwa na kasoro na pia kutokana na ushawishi wake
aliteuliwa kuwa Waziri wa Utalii na Utamaduni ambapo anaendelea na
nafasi hiyo hadi hivi sasa.
MANNY PACQUIAO
Jina lake kamili ni Emmanuel
Dapridran Pacquiao ni mkali wa ndondi tokea Ufilipino mwenye heshima na
mafanikio makubwa duniani kwa ujumla. Pamoja na mafanikio yake
alitangaza kujiingiza kwenye siasa mwaka 2007 lakini alishindwa kiti cha
baraza la uwakilishi katika Jimbo la Manila na mwaka 2009 aliamua
kugombea tena kupitia Jimbo la Sarangani ambapo alishinda kwa kishindo
kikubwa bila pingamizi chochote ambapo pamoja na masuala ya ngumi
anaendelea kushika nafasi hiyo hadi hivi sasa.
No comments:
Post a Comment