Friday, March 13, 2015

JANUARY MAKAMBA SIFA LUKUKI ALIZONAZO NA CHANGAMOTO ZA KUINGIA IKULU


January Yusuf.
MWAKA mmoja uliopita nilikutana na mwanasiasa kijana January Yusuf Makamba na kumuuliza kama ana wazo la kugombea urais; jibu lake lilikuwa ni: “Ni wazo sahihi.”
Sikumwelewa alimaanisha nini, lakini habari zilizopo mtaani hivi sasa kuwa anakusudia kuchukua fomu za kuomba uteuzi ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na hatimaye kuingia kwenye kinyang’anyiro cha kugombea urais nimeelewa kuwa jibu lake wakati ule lilimaanisha; NDIYO.
Ni wazi mtu kuamka na wazo la aina hii, kwamba na mimi nataka kugombea urais, ukimsikia akisema hivyo lazima nia yake hiyo itakuwa na historia. Bila shaka January amewaza jambo hilo tangu zamani, pengine kwa sababu amelelewa kwenye mikono ya mwanasiasa ambaye ni baba yake au amenogewa na uhondo wa uongozi.
JANUARY MAKAMBA NI NANI?
Ni mwanasiasa kijana aliyezaliwa Januari 28, 1974. Ameishi katika kijiji cha Mahenzagulu wilayani Lushoto, mkoani Tanga. Amesoma Shule ya Msingi Handeni, akaingia Sekondari ya Galanos na Forest Hill.


Baadaye alitimkia nchini Marekani ambako alisoma kozi fupi zinazohusu masuala ya amani kabla ya kuingia Chuo Kikuu cha George Mason  alikochukua  Masta yake katika Sayansi kuhusu Uchambuzi na Ufumbuzi wa Migogoro.

Alipohitimu masomo yake Makamba ambaye mama yake mzazi anaitwa Josephine mwenyeji wa Missenyi mkoani Kagera, alirejea nchini na kuajiriwa kama mtumishi daraja la pili katika Wizara ya Mambo ya Nje ambayo kwa wakati huo ilikuwa ikiongozwa na Rais Jakaya Kikwete.
ALIANZAJE SIASA?
Pamoja na kwamba January amelelewa na mwanasiasa Yusuf Makamba aliyewahi kuwa Katibu Mkuu wa CCM, kijana huyo hakuwa amechipuka kwenye anga hizo hadi pale alipojiunga rasmi kwenye mtandao uliokuwa ukiratibu harakati za Rais Kikwete kuingia madarakani.

Akiwa na umri mdogo, January alitumika vilivyo kwenye mtandao huo, akisafiri sehemu mbalimbali kushawishi makundi ya watu wamuunge mkono bosi wake wakati huo ili ashike dola, jambo ambalo liliwezekana mwaka 2005.
Baada ya Mheshimiwa Kikwete kuingia madarakani, hakuifukia lulu ya January pengine kwa sababu aliona umahiri wake wakati wa harakati. Rais hakujali umri mdogo aliokuwa nao kijana huyo, alimsogeza ikulu na kumfanya kuwa msaidizi wake akisimamia kazi maalum za kiongozi huyo wa nchi.
Utumishi wa nafasi hiyo ulizidi kumjenga mwanasiasa huyo, ingawa hakutajwa sana kwenye vyombo vya habari, lakini mgogoro wa dili la ‘Malaria No More’ wa mwaka 2008, ulioibuka kati yake na Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi, ulimleta kwenye sura ya jamii na kuonekana yupo na pengine watu walipata fursa ya kumperuzi kwa lengo la kumjua zaidi.
January alimudu nafasi ya usaidizi wa rais kwa miaka mitano mfululizo, mwaka 2010 aliamua kutema utamu wa ikulu na kwenda kugombea ubunge katika jimbo la Bumbuli mkoani Tanga ambako alishinda kwa kishindo na kuthibitisha uwezo wake kisiasa.
MAISHA YA UBUNGE NA UWAZIRI
Baada ya kuingia bungeni 2010, January alianza kuwa mwiba mchungu kwa serikali, michango yake makini kwenye  mijadala ya bunge iliwavutia wananchi wengi. Fumba na kufumbua aliteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Nishati na Madini ambapo aliiongoza vizuri.

Moja kati ya matunda aliyotoa mbunge huyo kwenye kamati yake ni pale alipoonesha ujasiri wa kukabiliana na wizara ya nishati katika tatizo la mgao mkali wa umeme lililokuwa likiitesa nchi wakati huo. Msimamo wake ulikuwa ni kutafuta suluhu ya tatizo hata ikiwezekana baadhi ya maslahi ya wafanyabiashara na viongozi wa serikali kuguswa.
Mwaka 2012 January alichaguliwa kuwa Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM, huku nyota ya mwanasiasa huyo kijana ikiendelea kung’aa kwa kuchaguliwa kuwa Naibu Waziri wa  Mawasiliano Sayansi na Teknolojia
ANAFAA KUINGIA IKULU
Sifa za kuingia ikulu anazo, hakika ni kijana aliyejipambanua kupitia utumishi wake kwa jamii kuwa ni mtu makini, mbunifu na mwenye dira ya maendeleo na uwezo wa kuleta mabadiliko kwenye mazingira magumu.

Katika nafasi ndogo aliyopewa ya unaibu waziri, kiongozi huyo ameonesha kwa vitendo kupambana na ufisadi ndani ya shirika la simu (TTCL) huku akibuni  mikakati ya namna ya kulifufua na kulifanya liondokane na kasumba ya kujiendesha kwa ubia.
January ni mtu wa vitendo, mfuatiliaji wa mambo, muumini wa haki na msimamizi wa mali za umma. Kabla ya kuwa mbunge aliandika kitabu alichokiita ‘Bumbuli Jana, Leo na Kesho’ ambacho kilichambua matatizo ya jimbo hilo na namna ya kuyashughulikia.
Mpaka leo mwanga wa maendeleo katika jimbo hilo umeanza kuonekana, hii inamaanisha kwamba kiongozi huyo kijana ambaye ameandika pia kitabu cha ‘Tanzania Mpya’ ni hazina isiyotakiwa kupotezwa kwa namna yoyote.
Katika masuala ya siasa na hasa unapozungumzia sifa za mgombea lazima awe anauzika na mwenye mvuto kwenye jamii, vitu ambavyo January kwa jinsi alivyo, ameonesha kuwa navyo.
Rais Mstaafu wa Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi amemuelezea January kuwa ni kijana makini.

CHANGAMOTO ZAKE
Pamoja na sifa alizonazo mbunge huyo kijana bado kuna changamoto nyingi ambazo zinaweza kukwaza safari yake ya kwenda ikulu, miongoni mwa hizo ni kukosa mtandao. Mbali na ndani ya chama chake hata nje nako January haonekani kama ana watu wengi wanaomuunga mkono katika safari yake ya urais. Ushindi wa kisiasa unahitaji mtaji wa watu, usipokuwa nao wa kutosha matarajio yako ya kushinda yanakuwa hafifu mno.

Changamoto nyingine ninayoiona kwa January ni kuhukumiwa kwa makosa ya baba yake. Ripoti ya uchunguzi wa mdororo wa CCM iliyowakilishwa na Wilson Makama mwaka 2011, ilionesha kwamba katibu mkuu wakati huo, Yusuf Makamba, alikuwa dhaifu kwenye kusimamia baadhi ya mambo.
Mbali na hilo taarifa za chini kwa chini ndani ya CCM zinaeleza kwamba mzee Mkamba alikuwa na msuguano na baadhi ya viongozi na makada nguli wa chama.
Kwa tabia za Kiafrika ni rahisi sana udhaifu wa baba kuhukumiwa nao mtoto na maadui wa wazazi kuwa wa familia nzima, tafsiri ambayo inaweza kumuondolea uungwaji mkono January na hasa ndani ya chama chake.
Hata hivyo, mtazamo huu unaweza kuwa siyo wa kudumu endapo juhudi za kumaliza dosari zikichukuliwa.

No comments:

Post a Comment

POSTED TITLE

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...