Monday, March 9, 2015

DAKTARI AANIKA UGONJWA WA BANZA STONE

Gladness Mallya/ijumaawikienda
Inasikitisha sana! Huku akitundikiwa dripu nyumbani kwao, Sinza ya Vatican jijini Dar, daktari ameanika ugonjwa unaomtesa staa wa muziki wa Dansi Bongo, Ramadhan Masanja ‘Banza Stone’ kuwa vipimo vinaonesha anashambuliwa na fangasi kichwani (ubongo) na shingoni.

Staa wa muziki wa Dansi Bongo, Ramadhan Masanja ‘Banza Stone’.
YU HOI TENA
Habari zinaeleza kuwa tatizo hilo limesababisha Banza kuwa hoi kwa mara nyingine akiumwa na kichwa kupita kiasi hivyo kushindwa kufanya lolote.Kufuatia maumivu anayoyapata, Banza amewaomba Watanzani wamuombee kwani anaamini katika maombi yao.


MAOMBI MUHIMU
Akizungumza kwa tabu na Ijumaa Wikienda, Banza ambaye kwa sasa hawezi kunyanyuka kwenye kochi alisema anatamani angepona ili arudi jukwaani hivyo maombi yao ni muhimu kuliko kitu chochote na ni msaada tosha kwake.

“Kikubwa nawaomba Watanzania waniombee kwani hali niliyonayo siyo ya kawaida, nasikia maumivu makali sana ya kichwa na shingo hadi nashindwa kula.“Hata kuongea ndiyo hivi kwa shida na muda mwingi naweka kitambaa cha maji ya baridi kwenye paji la uso ili kupunguza makali ya maumivu,” alisema Banza kwa masikitiko makubwa.
Banza kwa sasa anatibiwa nyumbani kwao baada ya kupata matibabu kwenye Hospitali ya Sinza-Palestina ambapo anaongezewa maji (dripu) na kuendelea kumeza dawa za ugonjwa huo.
DAKTARI ATHIBITISHA
Banza alisema ugonjwa huo amethibitishiwa na daktari wake kwenye hospitali hiyo baada ya kuchukuliwa vipimo.

FANGASI KICHWANI AU KWENYE UBONGO IKOJE?
Kwa mujibu wa mtaalam wa magonjwa ya kichwa, kitaalam ugonjwa huo huitwa Mucormycosis.
Ni ugonjwa ambao katika siku za hivi karibuni umekuwa maarufu huku ukisababisha vifo vya watu wengi. Kitaalam, ugonjwa huu husababishwa na fangasi waitwao Murcorales ambao huingia ndani ya mwili wa binadamu kwa njia ya hewa.

Ukivuta hewa yenye fangasi hao, huingia na kwenda moja kwa moja kwenye mfumo wa damu kisha kuanza kuzunguka ndani ya mwili kufuata damu. Baada ya kukaa kwa wiki kadhaa kwenye mfumo wa damu, huhamia kwenye uti wa mgongo (spinal) ambapo huzaliana kwa wingi na kuanza kusambaa kuelekea kwenye ubongo.
Fangasi hawa wanapofika kwenye ubongo, huushambulia na kusambaa kwa kasi ambapo uwezekano wa mgonjwa kupona huwa mdogo. Kati ya kila watu 100 wenye ugonjwa huo, karibu 30 hupoteza maisha.
DALILI ZA UGONJWA
Dalili za awali za ugonjwa huo ni kuwa na uvimbe mwekundu unaotokea kuzunguka macho ambao huongezeka kadiri fangasi wanavyozidi kushambulia ubongo.

Dalili nyingine ni pamoja na kuumwa kichwa upande mmoja, uso kuuma, homa kali, kupumua kwa shida na kutokwa kamasi za rangi nyeusi.Pia ngozi ya mwili wa mgonjwa huanza kubadilika rangi na kuwa nyekundu. Hali hiyo huendelea hadi ngozi inapobadilika zaidi na kuwa nyeusi.
TIBA
Vipimo vya ugonjwa huo hufanywa kwa mashine ya MRI ambapo mtu akibainika ameambukizwa fangasi hao, hutibiwa kwa upasuaji wa ubongo na kuondoa sehemu zilizoathirika pamoja na kutumia dawa kali za Amphotericin B au Posaconazole, wakati mwingine dawa hizi huchanganywa pamoja.

WATU WALIOPO KWENYE HATARI
Watu wanaoweza kuupata ugonjwa huu kwa urahisi ni wagonjwa wa kisukari, HIV, waliofanyiwa upasuaji wa kupandikiza viungo ndani ya miili yao kama figo au ini, na matumizi ya dawa za ‘corticosteroids’ kwa kipindi kirefu.

POSTED TITLE

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...