Monday, February 2, 2015

RAIS WA UJERUMANI AWASILI TANZANIA


Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Mohammed Gharib Bilal (kulia) akiwa mwenye furaha mara baada ya kumpokea Rais wa Ujerumani Mh. Joachim Gauck na Mkewe Bibi Schadt (walioshika maua), Uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere.
Rais wa Ujerumani Mh. Joachim Gauck akiwa na mkewe Bibi Schadt na Makamu wa Rais wa Tanzania Dkt. Mohammed Gharib Bilal wakitazama vikundi mbalimbali vya burudani wakati wa mapokezi ya Rais huyo wa Ujerumani Uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere jijini Dar es salaam.
Rais wa Ujerumani Mh. Joachim Gauck na Makamu wa Rais wa Tanzania Dkt. Mohammed Gharib Bilal wakifurahia jambo walipokuwa wakitazama vikundi mbalimbali vya burudani vilivyokuwa vikitumbuiza wakati wa mapokezi ya Rais huyo Uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere jijini Dar es salaam.
Baadhi ya wakazi wa jiji la Dar es salaam waliojitokeza kumpokea Rais wa Ujerumani Mh. Joachim Gauck wakiwa na nyuso za furaha. Na. Aron Msigwa -MAELEZO.
Rais wa Ujerumani Mh. Joachim Gauck na msafara wake amewasili katika Uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere usiku wa kuamkia leo majira ya saa 2.40.

Mara baada ya kuwasili uwanjani hapo akiwa ameambatana na mkewe Bibi Schadt amelakiwa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Mohamed Gharib Bilali pia mapokezi ya burudani za ngoma za asili kutoka vikundi mbalimbali na wananchi waliojitokeza kumpokea.

Rais huyo ambaye anaitembelea Tanzania kwa mara ya kwanza kufuatia mwaliko kutoka kwa Rais Jakaya Kikwete atapata mapokezi rasmi leo katika viwanja vya Ikulu majira ya saa 3 asubuhi ambapo rais huyo akiwa na mwenyeji wake, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Jakaya Kikwete atapata fursa ya kukagua gwaride maalum lililoandaliwa kwa ajili yake na Jeshi la Wananchi wa Tanzania na kupigiwa mizinga 21.

Akiwa nchini Tanzania Rais Joachim Gauck atakuwa na mazungumzo ya faragha na Rais Jakaya Kikwete, Ikulu jijini Dar es salaam na baadaye kufanya mazungumzo na baadhi ya viongozi wa Vyama vya hiari, uongozi wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheli Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Mashariki na Pwani pamoja na kukutana na wafanyabiashara wa Dar es salaam.

Pia Februari 4, 2015, Rais huyo ataelekea Zanzibar ambapo atakutana na kuwa na mazungumzo na Rais wa Zanzibar Dkt. Ali Mohamed Shein na viongozi wengine wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Kabla ya kuhitimisha ziara yake nchini Tanzania Februari 6, 2015 rais huyo wa Shirikisho la Ujerumani atatembelea mbuga ya wanyama ya Serengeti ,Makao Makuu ya Jumuiya ya Afrika Mashariki na Mahakama ya Kimataifa ya Haki za Binadamu jijini Arusha

No comments:

Post a Comment

POSTED TITLE

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...