Saturday, February 28, 2015

AZAM 'HATUNAYO' KLABU BINGWA TENA, TIMU ZA BONGO ZAJENGA UTEJA KWA WASUDAN...KMKM NAYE MHHH!!...

Mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara na wawakilishi wa Tanzania katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, Azam FC, wametupwa nje ya michuano hiyo kwa wastani wa mabao 3-2.
Azam, wamepigwa mabao 3-0 katika mechi ya marudiano iliyomalizika usiku huu mjini Khartoum, Sudan dhidi ya wenyeji wao, Al Merrikh.
Hata hivyo wenyeji wangefunga mabao mengi zaidi kama wasingekosa penalti katika dakika ya 46'.
Mechi ya kwanza uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es salaam, Azam walishinda mabao 2-0.
Katika mechi hiyo, Azam walipoteza nafasi nyingi za kufunga na kama wangekuwa makini wangepata ushindi mkubwa ambao ungewasaidia ugenini.
Al Merrikh walioanza fitina tangu Azam wanatua Khartoum walikuwa bora kwa kila kitu na walitumia vyema nafasi hizo tatu walizopata kati ya nyingi walizotengeneza.
Azam wameshiriki kwa mara ya kwanza ligi ya mabingwa na wametupwa nje asubuhi kabisa na sasa wanarejea kwenye mechi za ligi ambako nako kuna cheche za Yanga.
Kabla ya ligi ya mabingwa, mabingwa hao wa Tanzania waliwekeza pesa nyingi katika maandalizi, waliweka kambi uganda, wakaenda kushiriki kombe la Mapinduzi mwanzoni mwa mwaka huu na wakamalizia kambi nchini Congo DR, lakini mavuno yamekuwa hafifu.
Wakati huo huo, KMKM, wawakilishi wa Zanzibar kwenye ligi ya mabingwa, wametolewa na wapinzani wakubwa wa Merrikh, Al Hilal kwa wastani wa mabao 2-1.
KMKM walishinda 1-0 jioni ya leo uwanja wa Amaan Zanzibar, lakini mechi ya kwanza walipigwa 2-0 nchini Sudan.
Tanzania imebakiwa na timu mbili tu katika mashindano ya kimataifa kwa maana ya Yanga na Polisi FC ya Zanzibar, lakini kama taswira ilivyo, tutabaki na Yanga tu.
Yanga walifuzu raundi ya pili jana usiku kwa wastani wa mabao 3-2.
Walifungwa 2-1 na BDF XI mjini Gaborone, lakini wao walishinda 2-0 Dar es salaam.
Polisi wana uwezekano mkubwa wa kutupwa nje ya mashindano kwani mechi ya kwanza nchini Gabon, walipigwa 5-0 na CF Mounana, wao wanashuka dimbani kesho kusaka mabao 6-0 ili kusonga mbele.


No comments:

Post a Comment

POSTED TITLE

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...