Saturday, January 31, 2015

YANGA: PLUIJM ANA MAISHA MAREFU JANGWANI

Pluijm

Uongozi wa klabu ya Yanga, umesema unaamini kocha wake, Hans van Der Pluijm ana nafasi kubwa ya kuwa klabuni hapo kwa muda mrefu kutokana na kuwa na falsafa inayoendana na sekretarieti iliyopo madarakani kwa sasa.
Pluijm anatajwa kuwa kocha bora wa Jangwani katika misimu ya hivi karibuni, kutokana na mafanikio makubwa ndani ya kipindi kifupi alichokaa na timu msimu uliopita na uongozi unaamini atafanya mambo makubwa kutokana na mtazamano wake, lakini wakatoa angalizo kwa wanachama na mashabiki wa timu hiyo kuwa watulivu na kumuacha kocha afanye kazi yake.
Akizungumzia kasumba ya timuatimua ya makocha, Katibu Mkuu wa Yanga, Dk. Jonas Tiboroha alisema uongozi umetokea kumuamini Pluijm kutokana na mawazo chanya aliyonayo katika maendeleo ya soka klabuni hapo na kuamini anaweza kuwa nao kwa muda mrefu.
“Popote pale, kocha uhukumiwa na matokeo mabaya, kwa hiyo katika hili sio kusema Yanga ina tabia ya kufukuza makocha, sema wanafanyiwa mabadiliko kutokana na aina ya matokeo. Lakini naweza kusema kwa sasa ni tofauti kidogo kwa kocha Pluijm. 

“Kwanza ni mtu mwenye mtazamo chanya, tunaendana kimawazo, amekuwa akitupa ushauri chanya katika kuimarisha vikosi vyetu- vijana na wakubwa. Binafsi namuona kama ana maisha marefu Jangwani, ila tu angalizo ni kwa mashabiki wetu, wanatakiwa kuwa wavumilivu na kutodhubutu kuingilia kazi yake. Maana soka la Tanzania limezoeleka kuendeshwa na mashabiki. Tunaamini wakibadilika na kumuacha afanye kazi yake, hakika atatufikisha mbali,” alisema Tiboroha.
Katibu Mkuu wa Yanga, Jonas Tiboroha, kushoto.

No comments:

Post a Comment

POSTED TITLE

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...