Friday, April 11, 2014

TFF YAMTEUA MWAMUZI CHACHA KUCHEZESHA MICHUANO YA AYG


Release No. 061
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Aprili 11, 2014
CHACHA KUCHEZESHA MICHUANO YA AYG

Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) limeteua mwamuzi msaidizi wa Tanzania anayetambuliwa na Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA), Ferdinand Chacha ameteuliwa kuchezesha michezo ya Vijana ya Afrika (AYG- African Youth Games).

Michezo hiyo ya kwanza ya Afrika itachezesha jijini Gaborone, Botswana kuanzia Mei 22-31 mwaka huu. Tanzania pia itashiriki katika mashindano hayo ya vijana wenye umri chini ya miaka 15.

SIMBA, ASHANTI UTD KUVAANA TAIFA
Michuano ya Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) kuwania ubingwa wa Tanzania Bara inaendelea kesho(Aprili 12 mwaka huu) katika raundi ya 25 ambapo Simba na Ashanti United zitapambana Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kuanzia saa 10 kamili jioni.

Mechi nyingine zitakuwa kati ya Tanzania Prisons na Rhino Rangers (Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine, jijini Mbeya) wakati Coastal Union itakuwa mwenyeji wa JKT Ruvu kwenye Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga.

Keshokutwa (Aprili 13 mwaka huu) kutakuwa na mechi nyingine nne za kukamilisha raundi hiyo. Uwanja wa Sheikh Kaluta Amri Abeid jijini Arusha utakuwa mwenyeji wa mechi kati ya wenyeji Oljoro JKT na Yanga.

Mtibwa Sugar itacheza na Ruvu Shooting (Uwanja wa Manungu, Morogoro), Mgambo Shooting na Kagera Sugar zitaoneshana kazi kwenye Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga huku Mbeya City ikiumana na Azam kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine jijini Mbeya.

TIMU YA WATOTO WA MITAANI YATAMBULISHWA BUNGENI

Timu ya Watoto wa Mitaani ya Tanzania iliyotwaa ubingwa wa Dunia wa Watoto wa Mitaani nchini Brazil baada ya kuifunga Burundi mabao 3-1 kwenye fainali imetambulishwa leo (Aprili 11 mwaka huu) katika Bunge Maalumu la Katiba mjini Dodoma.

Baadaye timu hiyo leo itapata chakula cha mchana na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mizengo Pinda. Saa 10 jioni itatembeza kombe hilo katika maeneo mbalimbali ya Manispaa ya Dodoma katika gari za wazi.
Jioni imeandaliwa hafla maalumu ya chakula pamoja na burudani hapo hapo mjini Dodoma ambapo mgeni rasmi atakuwa Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dk. Fenella Mukangara.

MWENYEKITI WA CECAFA KUZUNGUMZA NA WAANDISHI

Mwenyekiti wa Baraza la Vyama vya Mpira wa Miguu Afrika Mashariki na Kati (CECAFA), Leodegar Tenga atakuwa na mkutano na waandishi wa habari Jumatatu (Aprili 14 mwaka huu).

Mkutano huo utafanyika kwenye ofisi za Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) zilizopo Ghorofa ya 3, Jengo la PPF Tower mtaa wa Ohio/Garden Avenue kuanzia saa 5 kamili asubuhi.

BONIFACE WAMBURA
OFISA HABARI NA MAWASILIANO
SHIRIKISHO LA MPIRA WA MIGUU TANZANIA (TFF)

POSTED TITLE

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...