Monday, March 24, 2014

ZA KUAMBIWA NA JK, WARIOBA TUCHANGANYE NA ZETU


Rais  wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Jakaya Mrisho Kikwete.
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Jakaya Mrisho Kikwete Ijumaa iliyopita alilizindua rasmi Bunge Maalum la Katiba kwa kutoa hotuba iliyokigawa chombo hicho muhimu kwa taifa kwa sasa, baada ya wajumbe wake kutofautiana misimamo.
Hotuba hiyo ya Rais, ilikuja siku chache tu baada ya Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba kuwasilisha rasimu ya katiba hiyo mbele ya wajumbe hao hao.
Akiwasilisha rasimu hiyo huku akishangiliwa na wajumbe wengi, Jaji Warioba alisema suala la serikali tatu haliepukiki, kwani hiyo ndiyo njia pekee ya kuunusuru Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, hasa kwa vile tayari upande mmoja umeshavunja katiba ya sasa, kwa kujitangaza nchi kamili, haki ambayo inapaswa pia kutolewa kwa upande wa pili.
Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba.
Lakini katika hotuba yake ya uzinduzi wa bunge hilo, Rais Kikwete, naye huku akishangiliwa na idadi kubwa ya wajumbe, alisema mfumo wa serikali mbili ndiyo pekee unaopaswa kufuatwa, kwa sababu serikali ya tatu, siyo tu haitakuwa na chanzo cha uhakika cha mapato, bali pia inaweza kusababisha machafuko, hasa kama itashindwa kusimamia vizuri vyombo vya ulinzi na usalama.
Wakati Warioba aliwasilisha rasimu kama maoni ya wananchi yaliyoratibiwa na tume yake, Rais Kikwete alisema alichokisema ni maoni yake binafsi, licha ya ukweli kwamba msimamo huo unafanana na ule wa chama chake cha CCM.
Wote wawili, kila mmoja alipopata nafasi ya kusimama mbele ya wajumbe na taifa kwa jumla, walitoa sababu zinazounga mkono misimamo yao, kwa nini serikali tatu ni muhimu na jinsi gani serikali mbili zinavyoweza kudumisha umoja na mshikamano kama taifa.
Katika moja ya hotuba zake nyingi kwa taifa, Rais Kikwete aliwahi kutoa kauli moja ya msingi sana, kwamba akili ya kuambiwa, changanya na yako.
Huu ndiyo unaoweza kuwa ujumbe wangu kwa wajumbe wa bunge hili, ambao wataipitia, kuijadili na hatimaye kutupatia katiba mpya ya Tanzania ili wananchi tuweze kupiga kura ya maoni.
Nimezisikia hotuba zote mbili na ni lazima niwe mkweli kwamba maelezo ya kila upande yana ushawishi wa aina yake kwangu. Ni wazi kwamba kutakuwa na mvutano mkubwa wa mawazo wakati wa mjadala wa rasimu hii, ingawa zipo dalili kwamba mchakato mzima unaweza kutekwa na itikadi za kimakundi badala ya kuiweka nchi mbele.
Nionavyo, kwa jinsi hali ilivyo, ili tutembee katika maneno ya Rais Kikwete, ni lazima Zanzibar ikubali kuiondoa katiba yake, ili tubaki na ile ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Wapo baadhi ya watu wanaodai serikali tatu kwa sababu ya chuki tu, lakini hawana hoja yoyote vichwani mwao.
Na chuki hii inakuja kwa vile wanajiuliza mbona wenzao wa Zanzibar wana Katiba yao, inayoitambua kama nchi kamili, yenye wimbo wake wa taifa, yenye bendera yake na bunge lake, lakini Tanganyika ikiwa haina vitu vyote hivyo?
Wanaotetea muungano wa serikali mbili lazima wawe na jibu la kutosheleza maswali kama haya. Haitoshi tu kusema tutavunja muungano bila kupata muarobaini wa hili.
Na hata serikali tatu nazo zina maswali yanayohitaji majibu, kama chanzo chake cha mapato ni kipi na jukumu lake kama serikali ni lipi. Maana isije ikafikia wakati tunatengeneza serikali ya heshima (Ceremonial Government) isiyo na kazi ya maana ya kufanya.
Ndiyo maana tukasema katika suala la katiba ya nchi, ni jambo la hekima sana kila mmoja kuchanganya akili zake na zile za kuambiwa, tulizoletewa na Rais Kikwete pamoja na Jaji Warioba.
Wote kama taifa, ni lazima tukubali kwamba nchi yetu inahitaji mabadiliko ya kimfumo, vinginevyo taifa litaendelea kudumaa kiuchumi na kimaendeleo, licha ya rasilimali nyingi zilizopo ambazo wakati mwingine wanaofaidika nazo ni wachache kwa sababu ya ufisadi.
Ili hili lifanikiwe, ni lazima akili ya makundi tuiache. Tujadili na kupitisha vifungu bila kujali kama wewe ni Mpemba au Mtanganyika, bila kuhusisha chama chako cha siasa wala masilahi ya kundi unalowakilisha. Tunachohitaji ni katiba itakayowafaa Watanzania.
Asiwepo Mtanzania anayedhani yeye au kundi lake ni bora kuliko katiba tunayotaka kuitengeneza inayolenga kutumika sasa na vizazi vijavyo!

No comments:

Post a Comment

POSTED TITLE

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...