Monday, March 24, 2014

CHAKULA CHA UBONGO: BUNGE LA KATIBA LICHUNGULIE ZANZIBAR


Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad.

Na Luqman Maloto
KICHWA kinauma kutokana na kufikiria jinsi Bunge Maalum la Katiba litakavyokuwa na kazi kubwa ya kuandika Katiba Mpya ya Tanzania huku kukiwa na vifungu katika Katiba ya Zanzibar ambavyo vinaashiria mambo mazito.

Rais wa Zanzibar, Ali Mohamed Shein.

Moja ya vifungu hivyo ni katika Sura ya kwanza kifungu cha 1 cha katiba hiyo kinachosema kuwa Zanzibar ni nchi ambayo eneo la mipaka yake ni eneo lote la Visiwa vya Unguja na Pemba, pamoja na visiwa vidogo vilivyoizunguka ambavyo kabla ya muungano wa Tanganyika na Zanziabar ikiitwa Jamhuri ya Watu wa Zanzibar.

Kifungu hicho ni kinyume na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayosema Tanzania ni Jamhurri ya Muungano na eneo lake la ardhi ni kuanzia Tanzania Bara hadi Zanzibar.

Hakuna ubishi kwamba kifungu hicho cha sheria ndicho kilichofanya kesi ya uhaini ya Zanzibar ambayo iliwahusisha viongozi wengi wa Chama Cha wananchi (CUF), akiwemo Maalim Seif Sharif Hamadi (pichani) kuachiwa huru na Mahakama ya Rufaa ya Tanzania

baada ya kuonekana kuwa hakuwezi kufanyika Zanzibar uhaini kwa sababu eneo hilo siyo la nchi dola inayoweza kupinduliwa nje ya Tanzania.

Lakini Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 ilisema Zanzibar ni sehemu ya Jamhuri ya Muungano, kwa maana hiyo katiba ya sasa ya Zanzibar inakana muungano kwa kuweka mipaka yake na kujitenga na Tanzania Bara.

Ibara ya 2(A) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeweka bayana kuwa pale rais anapotaka kuigawa Zanzibar, atashirikiana na Rais wa Tanzania Zanzibar, sasa sijui kama Baraza la Wawakilishi baada ya kupitisha sheria hiyo na kumkabidhi rais wa Zanzibar kabla ya kutia sahihi aliwasiliana na rais wa jamhuri?

Kama hakuwasiliana naye na tayari ameweka mipaka ya visiwa hivyo ni wazi Rais wa Zanzibar, Ali Mohamed Shein amemkosea Rais wa Jamhuri, Jakaya Mrisho Kikwete kwani kwa maneno mengine mabadiliko hayo yamekiuka Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Hakika hayo ndiyo mambo ya kujadili wakati wa kupitisha vifungu hivyo vinavyohusu mipaka ya nchi. Kuna matatizo mengi sana ya kujadili na kupatia ufumbuzi lakini hili la muungano ndilo linalogonga vichwa vya watu wengi.

Ukweli ni kwamba nchi hii waasisi wetu walikuwa na nia ya kuifanya nchi moja na ndiyo maana walipoanza tu aliyekuwa Rais wa Zanzibar akawa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Wazanzibar walikasirika baada ya cheo hicho kunyang’anywa rais wao na wakawa wanahoji, atakapokuwa anakuja katika baraza la mawaziri la Tanzania atakuja kama nani? Mjumbe tu wa kawaida? Hatukusikia jibu hadi leo.

Watu wa Unguja na Pemba baada ya kuona hivyo wakaamua kutengeneza katiba yao kama ilivyo sasa na wakatengeneza bendera yao na wimbo wao wa taifa. Haya yote wakati wa kuandikwa katiba mpya yaangaliwe kwa kina kwa sababu kulipua kunaweza kuzusha machafuko siku za usoni. Kazi kwenu wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba.

No comments:

Post a Comment

POSTED TITLE

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...