Tuesday, March 11, 2014

UCHAGUZI WA MWENYEKITI WA BUNGE LA KATIBA KUFANYIKA KESHO DODOMA,TUWAACHE WABUNGE WATUPE KITU BORA


NINA heshima kubwa kwa Mwenyezi Mungu kwa huruma yake juu yangu, kuweza kuwa pamoja na nyinyi tena leo hii, akinitumia mimi kuwafikishia ujumbe wake wenye upendo na amani.

Nimesema mara zote na kamwe sitachoka kuwakumbusha kuwa tupo wazima kama hivi tulivyo kwa sababu ya huruma yake Mungu tu, vinginevyo sisi hatuna tofauti na walio katika wodi za wagonjwa mahututi, waliofariki dunia na wale wenye shida mbalimbali.

Baada ya utangulizi huo, naomba sasa niende moja kwa moja kwenye mada yetu ya leo. Nimejaribu kuliangalia Bunge kupitia runinga na kuwasikiliza watu wanavyolitazama na kugundua kuwa wengi wetu wanaona kama wajumbe wa Bunge Maalum ni wanaopoteza muda na fedha kwa jinsi wanavyozomeana, kejeliana na kadhalika.

Mimi nimewatazama wajumbe hawa na kujikuta nikielewa nini kinafanyika huko na hivyo nachukua fursa hii kuwaelezea nilichogundua na kuwataka tuwaunge mkono.

Mabishano ya sasa ndani ya Bunge hilo ni kuhusu kanuni zitakazoendesha vikao hivyo. Kama tunavyojua, kanuni ni jambo la msingi sana katika majadiliano muhimu kama haya, kwani vinginevyo, tunaweza kujikuta tukiruhusu kanuni ambazo hazitaweza kutuongoza kupata katiba bora.

Ni afadhali wazomeane sasa, watoleane maneno ya kejeli sasa, ili mradi mwisho wa siku, tupate kanuni ambazo zitatuongoza vizuri katika kupata katiba ambayo itakuwa ni kwa faida yetu sote.

Kanuni ni kitu cha msingi sana, hasa katika mjadala mkubwa kama huu ulio mbele yao. Kanuni hizi, kwa lugha rahisi, ni sheria za kuliongoza Bunge. Tukiwa na sheria legelege, zisizoeleweka, tusitegemee kabisa kupata katiba imara.

Ingawa katika baadhi ya nyakati wajumbe hawa wamekuwa wakikera, lakini ni lazima tujue kuwa kila mmoja anafanya hivyo kwa hisia kali iliyo ndani ya nafsi yake juu ya mapenzi yake kwa nchi yetu. Nikiwatazama jinsi wanavyorushiana maneno kwa jazba na wakati mwingine kwa kutumia lugha kali, najikuta nikifurahi kwamba kila mmoja anafanya vile ili kuonyesha mapenzi yake kwa Tanzania.

Natoa rai kwa wananchi wenzangu kuwa na subira, kuacha kutoa hukumu mapema, kwani kanuni bora ndizo zitakazozaa katiba bora. Kama tutataka kuwaona wakipitisha kila kifungu kwa haraka bila upembuzi yakinifu, uwezekano wa kutuletea kitu ambacho siyo utashi wetu ni mkubwa sana.

Lakini hata hivyo, wakati ninawaomba wananchi wenzangu kuwapa muda wajumbe wa Bunge hili maalum, ni lazima pia niwe mkweli kwa wajumbe hao kuwa, baadhi ya vitendo na maneno yao, yamekuwa ni ya kukatisha tamaa, kwa vile yanaonyesha kwa kiasi kikubwa, wamekwenda pale wakiwa na ajenda ambayo siyo ya Watanzania.

Inasikitisha kuona baadhi ya wajumbe wakitoa kauli zisizo na staha, wakishindana kwa hoja zisizo na mashiko na hata kusisitiza misimamo yao binafsi kwa ajili tu ya kukomoana, kutokana na tofauti za kiitikadi.

Ni lazima tuendelee kuwakumbusha kuwa jukumu lililo mbele yao ni la kutimiza kiu ya Watanzania wote, bila kujali itikadi zao za kisiasa, asasi, jinsia wala makundi wanayowakilisha. Katiba inayotafutwa ni ya Watanzania wote, hakuna sababu ya wajumbe kuanza kutunishiana misuli na kuonyeshana tofauti katika vitu ambavyo wote wanafahamu kwamba ni muhimu kwa umma wa Watanzania.

Ni kwa sababu hiyo, wajumbe wetu lazima watambue thamani ya kazi iliyo mbele yao na vitendo vyao wanavyovifanya ambavyo watu wanavishuhudia kupitia televisheni. Haipendezi kuona wakifanya vitu vinavyowafanya watu wagune na kuanza kutilia shaka umakini wao katika kutengeneza maisha ya Watanzania wa vizazi vijavyo.

No comments:

Post a Comment

POSTED TITLE

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...