Wednesday, January 8, 2014

ZITTO ADAIWA KUWEKA NJIA PANDA UANACHAMA WAKE CHADEMA


Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe.
MBUNGE wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe ameuweka njia panda uanachama wake ndani ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) baada ya Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, kukubali pingamizi lake la kuizuia Kamati Kuu (CC) ya chama hicho isimjadili hadi kesi yake ya msingi itakapokuwa imesikilizwa.

Kwa uamuzi huo, Zitto sasa atabaki kuwa mwanachama kwa nguvu ya mahakama hadi hapo itakapoamriwa vinginevyo.

Sasa Zitto ataungana na wabunge wenzake wawili, David Kafulila wa Kigoma Kusini (NCCR-Mageuzi) na Hamad Rashid Mohammed wa Wawi (CUF) ambao pia ubunge wao upo kwa nguvu ya mahakama.

Zitto alifungua kesi mahakamani hapo siku moja kabla ya CC kuanza vikao vyake ambavyo vilikuwa vijadili utetezi wa tuhuma zake za kuendesha mkakati wa siri wa kusaliti chama, akiomba mahakama izuie suala la uanachama wake lisijadiliwe hadi kesi yake isikilizwe.

Akitoa uamuzi wa awali, Jaji John Utamwa, alisema kuwa mahakama imeridhia ombi la Zitto kuwa CHADEMA au chombo chochote kisijadili uanachama wake hadi kesi ya msingi itakapomalizika.

Akisoma maelezo ya awali, Utamwa alisema kuwa wakili Peter Kibatala anayewakilisha Bodi ya Udhamini ya CHADEMA na Katibu Mkuu ambao ndio washtakiwa, alikula kiapo kwa niaba yao jambo ambalo si sahihi.

Utamwa alisema kuwa kwa mazingira ya kesi kuhusisha Bodi ya Udhamini ya CHADEMA na Katibu Mkuu, ilikuwa si sahihi kwa wakili kula kiapo kwa niaba yao.

Wakizungumza baada ya kutoka mahakamani, mawakili wa upande wa CHADEMA, Kibatala na Tundu Lissu walisema kuwa kuhusiana na hati ya kiapo, ipo sheria inayoruhusu wakili kula kiapo kwa ajili ya mteja wake.

Walisema kuwa wanaheshimu uamuzi wa mahakama japo hawajaridhika, na hivyo watachukua hatua za ziada.

Wakili wa Zitto, Albert Msando, aliomba uamuzi wa mahakama uheshimike kwani ni hatua za haki kutendeka na mteja wake kupata nafasi ya kusikilizwa.

Katika kesi ya msingi, Zitto anaiomba mahakama ikizuie chama hicho kumchukulia hatua, ambapo kesi hiyo inatarajiwa kutajwa Februari 13, mwaka huu.

Zitto aliwasilisha maombi dhidi ya Baraza la Wadhamini la CHADEMA pamoja na Katibu Mkuu wa chama, Dk. Willibrod Slaa, akiiomba mahakama itoe zuio la muda kwa Kamati Kuu kutojadili uanachama wake.

Katika kesi hiyo, Zitto anaiomba mahakama iizuie Kamati Kuu kujadili uanachama wake hadi rufaa yake itakaposikilizwa na Baraza Kuu la chama na kuomba mahakama imwamuru Dk. Slaa ampe nakala za taarifa za vikao vilivyomvua uongozi ili akate rufaa.

Hali ilivyokuwa

Zitto alipokelewa na wanachama wa CHADEMA kwa kuzomewa kuanzia hoteli ya Hyatt Kempisky hadi katika lango kuu la kuingia Mahakama Kuu.

Sauti hizo zilisikika zikimba na kuzomea; “Zitto kibaraka wa CCM; CCM huyo…”

Zitto ambaye aliongozana na walinzi wanne wenye miili mikubwa (mabaunsa), alikuwa ameinamisha sura chini na kutembea haraka kuingia mahakamani.

Hata hivyo, kabla ya kuingia lango kuu la mahakama, alipepesuka na kuvuka kiatu kimoja cha mguu wa kushoto.

Baada ya kadhia hiyo ya nje, alikutana na wanachama wengine wa CHADEMA ndani ya mahakama, ambao walimzomea hadi kwenye mlango wa vyumba vya mahakama.

Nako nje, mamluki wanaodaiwa kukodiwa na Zitto tangu kuanza kwa kesi hiyo, jana hali ilikuwa ni tofauti kutokana na kufika kwa uchache huku wakizomewa na wanachama wa CHADEMA.

Tanzania Daima ilidokezwa kuwa walinzi waliokuwa wanamlinda Zitto, walifahamika kwa jina moja moja la Tino, Evans na Ziggy.

Ndani ya mahakama, kabla ya kesi kuanza baadhi ya wanachama wa CHADEMA walimtambua mtu mmoja aliyevaa suti nyeusi na kuanza kumshambulia kwa maneno kuwa ni kibaraka wa Ridhiwani Kikwete hadi mtu huyo alipojitetea akidai ni wakili.

Vituko vya Zitto kisiasa

Zitto ambaye anahaha kila kona ili asivuliwe uanachama wa CHADEMA, amekuwa na mtiririko wa matukio mengi ya kauli ambazo zimechangia wananchi kumtilia shaka mwenendo wake ndani ya chama.

Mwaka 2010 wakati nchi ikielekea uchaguzi mkuu, Zitto alitishia kutowania tena ubunge katika jimbo lake la Kigoma Kaskazini kwa madai kuwa ameombwa kugombea katika majimbo ya Kigoma Mjini, Kinondoni, Geita na Kahama.

Lakini dakika za mwishoni kabisa, Zitto alirudi kugombea jimboni kwake akidai ameshauriwa na wazee.

Baada ya uchaguzi mkuu, mwanasiasa huyo alitangaza kutogombea ubunge katika uchaguzi mkuu wa 2015, akidai kuwa ataachana na siasa ili akafanye kazi ya kitaaluma chuo kikuu.

Muda mfupi baadaye, akakaririwa na vyombo vya habari kwamba anaandamwa ndani ya chama, kiasi cha kufikia hatua ya kutembea na barua ya kutaka kujiuzulu nafasi ya Naibu Katibu Mkuu.

Machi mwaka jana, mbunge huyo alitangaza nia ya kuutaka urais wa Tanzania, lakini baada ya kuibuka mjadala mkubwa ndani na nje ya chama chake akielezwa kuwa umri wake hajakidhi matakwa kikatiba, Septemba mwaka huo, alitengua nia hiyo.

Akiwa katika ziara ya kichama mkoani Tabora Novemba mwaka jana, Zitto pia alitengua kauli yake ya kutogombea ubunge mwaka 2015 akisema anaitafakari upya baada ya kuona kero nyingi zinazowakabili wananchi.

Kauli tatanishi za Zitto zimezidi kuongeza shaka hasa katika majibu yake hivi karibuni kupitia mtandao wake wa kijamii wa facebook wakati akifafanua tuhuma zilizoelekezwa kwake na mwanasheria wa CHADEMA, Lissu.

Lissu alidai kuwa Zitto amehongwa magari mawili na Mbunge wa Musoma Vijijini, Nimrod Mkono ili amwezeshe kupita bila kupingwa katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2010.

Hata hivyo, katika utetezi wake wa maandishi kupitia ukurasa wake, Zitto aliandika kuwa; “Lissu amenituhumu kuwa nimehongwa magari 2 na mheshimiwa Nimrod Mkono. Mimi ninamiliki gari mbili, Freelander ninayotumia Dar es Salaam na Toyota Carina ninayotumia jimboni.”

Majibu ya Zitto yalitofautiana na Mkono ambaye katika taarifa yake alisema kuna magari mawili yanayohusishwa na Zitto na kuyataja kuwa ni Toyota Land Cruiser na Nissan Patrol.

“Sijawahi kumpatia Zitto magari, isipokuwa kuhusu hiyo Land Cruiser, nilitoa msaada wa kuwanusuru Zitto na Mbowe (Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe), kule Tarime kwenye msiba wa marehemu Chacha Wangwe (aliyekuwa Makamu Mwenyekiti CHADEMA), kwani walikuwa wakitishiwa kupigwa.

“Walipofika Mwanza, Zitto aliwasiliana na mimi kuhusu ununuzi wa gari hilo na kupitia wakala wangu nilimuuzia,” alisema Mkono.

Kuhusu Nissan Patrol, Mkono alisema lilikodishwa kwa Zitto na hadi sasa bado analipa gharama za kulikodisha.

Utata katika suala hili uko kwenye aina za magari zilizotajwa na wanasiasa hawa wawili. Wakati Zitto akitaja kumiliki Freelander na Toyota Carina bila kufafanua kama anayo magari mengine, Mkono anasema amemuuzia Land Cruiser na Nissan Patrol.

Kada CCM anena

Aliyewahi kuwa Mwenyekiti wa CHADEMA Mkoa wa Morogoro, David Mgesi, amesema yanayotokea sasa kwa Zitto ni kile alichokuwa akikisema kwa muda mrefu kuhusu mbunge huyo.

Mgesi ambaye kwa sasa ni kada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), alisema wakati akiwa CHADEMA, alishaonya mienendo ya Zitto kwa kuona kwamba ni mtu ambaye anaweza kukisaliti chama wakati wowote.

Kwamba viongozi wa juu wa CHADEMA waliweza kumuamini Zitto na kumuona kuwa ni mtu mwenye busara.

Akitolea mfano, alisema ilikuwa mwaka 2005, Zitto alipewa dhamana ya kutengeneza bajeti ya chama, na baada ya kuwagawia taarifa ya wajumbe wa Kamati Kuu alitaka wazirudishe kwa madai kuwa hawaamini kwani wanaweza kuvujisha siri nje.

“Baada ya kauli ile nilimuomba Mwenyekiti, Freeman Mbowe tujadili kauli hiyo, lakini lilifunikwa na Zitto akatetewa kuwa aliteleza.

“Sasa ukiangalia leo nani msaliti kama sio yeye ambaye amekuwa akipokea fedha kwa muda mrefu kwa lengo la kukivuruga chama?” alihoji.

Akizungumzia hatua ya Zitto kwenda mahakamani, Mgesi alisema sio sahihi na badala yake alitakiwa kwanza kujibu tuhuma zote zilizoelekezwa kwake ili kuwaelewesha Watanzania na kuwahakikishia anachotuhumiwa si sahihi.

Hata hivyo, Mgesi alisema inasikitisha kuona hadi sasa Zitto na CCM wanaotuhumiwa katika kupeana fedha ili kukiharibu CHADEMA wameshindwa kujitokeza kukanusha taarifa hizo.

“Zitto anapaswa ajitokeze akane kama hakupokea fedha hizo zinazodaiwa kupitia benki ya CRDB, vile vile Serikali ya CCM ilipaswa kuthibitisha kama akaunti zilizotajwa kuwa za Idara ya Usalama wa Taifa ni za kweli au hapana,” alisema.

Mgesi alisema kitendo cha pande zote kukaa kimya wakati suala tajwa likiendelea kushika kasi, kunaibua maswali mengi kwa wananchi.

Alisema mgogoro huu ni wa muda mrefu na umetengenezwa huku akikumbushia namna ambavyo Waziri Stephen Wasira alikuwa akisisika akisema kuwa CHADEMA itakufa kabla ya mwaka 2015.

Mgesi pia alitaja matukio ya kubambikiwa kesi ya ugaidi kwa Mkurugenzi wa Usalama wa CHADEMA, Wilfred Lwakatare na vijana wengine watano kuwa ulikuwa ni mwendelezo wa mkakati wa kukiua chama hicho.

Aliwaonya vingozi wa CCM ambao wamekuwa wakizungumzia mgogoro huo wa CHADEMA majukwaani, akiwataka kuachana na kazi hiyo kwa kuwa sio iliyowaweka madarakani.

“Wakati CCM inapewa dhamana na wananchi kuongoza, katika ahadi zake hakuna mahali wanasema watakuwa wakijadili mgogoro wa CHADEMA,” alisema.

HABARI NA TANZANIA DAIMA

No comments:

Post a Comment

POSTED TITLE

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...