Monday, January 27, 2014

MAZIKO YA MCD WA TWANGA PEPETA KUFANYIKA KESHO MCHANA MOSHI


MCD akiwa katika pozi enzi za uhai wake

 
ALIYEKUWA mpiga tumba wa Twanga Pepeta Soud Mohamed 'MCD' aliyefariki jana usiku, atazikwa kesho saa 7 mchana Moshi mjini.

Kwa mujibu wa kiongozi wa Twanga, Luizer Mbutu mazishi ya MCD ilikuwa yafanyike leo saa 10 lakini familia ikakubali kusogeza mbele ili wafanyakazi wenzie pamoja na marafiki wa marehemu waweze kuwahi mazishi hayo.

Msafara wa wasanii wa Twanga, wawakilishi wa bendi zingine, wadau na marafiki, utaondoka Dar es Salaam leo saa 4 usiku kuelekea Moshi.

MCD aliyefariki sekunde chache baada ya kufikishwa hospitali ya KCMC atazikwa Kiislam, dini aliyoitumikia hadi kufa kwake baada ya kubadili dini mara kadhaa.

Mpiga tumba huyo, kiasi cha kama miaka 13 iliyopita alibadili dini kutoka Uislam na kuwa mkristo hiyo ni kufuatia ndoa yake na Renada mtoto wa Chang’ombe lakini walipoachana akarejea tena kwenye Uislam.

Japo katika miezi ya hivi karibuni kulikuwa na mashaka kuhusu dini yake, lakini MCD aliithibitishia familia yake pamoja na wafanyakazi wenzake kuwa yeye ni Muislam.
Katika hatua nyingine usiku wa kuamkia leo, viongozi wa Twanga Pepeta, wadau na wasanii wa bendi mbali mbali walikutana na kuchagua kamati itakayoratibu safari ya kuelekea Moshi pamoja na mambo mengine ya kusaidia taratibu za mazishi.

Wajumbe wa kamati hiyo ni Omary Baraka (Mkurugenzi Msaidizi ASET), Hassan Rehani (Meneja ASET), Abdallah Dossi(Mwenyekiti Macamp ya ASET), Martin Sospeter (Meneja Mashujaa Musica), Tarsis Masela (Kiongozi Akudo Impact), Deo Mutta (Katibu wa Macamp ya ASET), Rehema Kiluvia (Mdau Twanga Pepeta) na Super Nyamwela (Kiongozi Mkuu Shoo Extra Bongo) na Luizer Mbutu (Kiongozi Mkuu Twanga Pepeta) ambaye ndiye mweka hazina wa kamati hiyo.

Luizer ameiambia kuwa leo kuanzia saa 6 mchana hadi muda wa kuelekea Moshi, wadau wote watakutana katika ukumbi wa Vijana Hostel Kinondoni kwenye ofisi mpya za Twanga Pepeta.
Kwa wote watakaotaka kuchangia msiba huo kwa njia ya simu za mkononi basi wanaombwa kutuma pesa zao kupitia simu zifuatazo ambazo zote ni za Luizer Mbutu: 0653 797976, 0762 46 00 90, 0787 090 090.

CHANZO SALUTI 5

No comments:

Post a Comment

POSTED TITLE

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...