Sunday, November 24, 2013

ZITTO KABWE ATOA YA MOYONI MWAKE KWA WANANCHI



MBUNGE wa Chadema na Naibu Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Zitto Kabwe amesema hawezi kufanya maamuzi magumu ya kutaka kujitoa ndani ya chama hicho kwa kile kilichotokea ndani ya chama hicho hivi karibuni. Amesema yeye atakuwa wa mwisho kutoka Chadema na si vinginevyo,kama wanavyofikiria watu wengine.

Zitto ameyatoa maneno hayo leo katika mkutano na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam,wakati alikizungumzia maamuzi ya Kamati Kuu ya Chadema ya kumvua nafasi zake zote za uongozi yeye pamoja na Mjumbe wa Kamati Kuu ya chama hicho Dk. Kitilla Mkumbo na aliyekuwa Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Arusha,Samson Mwigamba.

Zitto amekana kabisa kuhusika na wala kuujua waraka wa siri ambao ndiyo uliosababisha kumvua madaraka baada ya uamuzi wa Kamati Kuu ya chama kuunasa waraka huo.

"Mimi nimeusikia ule waraka kwa mara ya kwanza kwenye Kamati Kuu na nilisikitika sana kwanini haukunifikia haraka kwani ningeanza kutekeleza mara moja." alisema Zitto akizungumza.

Zitto aliendelea kusema "Huenda leo watu walitegemea nitafanya maamuzi magumu ya kuondoka kwenye chama; "Mimi bado ni mwanachama wa Chadema na nitakaekuwa wa mwisho kutoka kwenye chama hiki kwa hiyari yangu, nitafanya taratibu zote za chama kuhitimisha jambo hili mimi sitoki ng'o kwenye chama hiki labda wanitoe wao," alisema Zitto.

Zitto alisema anaumia sana anapotuhumiwa kwa kuwa yeye ni binadamu. "...ninapotuhumiwa naumia ninapoambiwa nahujumu chama hiki naumia kwa kuwa nakipenda chama na nimekitumikia muda mrefu. Aidha aliwataka viongozi wa Chadema kuacha siasa za uzushi ili kujenga chama imara na kuwakomboa Watanzania.

"...Sisemi kama mimi sina makosa,kwani mimi ni binadamu na nimefanya mambo mengi kwa chama changu, lakini kinachoendelea kwa sasa ndani ya chama chetu ni mapambano ya kukuza demokrasia na ni mapambano ya wanaotaka mabadiliko na wasiopenda mabadiliko ndani ya chama...mapambano ya wawajibikaji na wasiopenda kuwajibika ni mapambano ya wanaopenda demokrasia na wanaokwaza demokrasia." alisema Zitto huku akionesha kusikitishwa.
Mbunge wa Kigoma Kaskazini,Mh. Zitto Kabwe akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam mapema leo,wakati akitoa taarifa yake ya kuhusu kuvuliwa nyadhifa mbalimbali ndani ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) pamoja na aliekuwa Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA),Dkt. Kitika Mkumbo (kushoto),kwenye Hoteli ya Serena jijini Dar es Salaam leo.

Aliekuwa Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA),Dkt. Kitika Mkumbo akizungumza.

Zitto Kabwe (kulia) na Dk. Kitilla Mkumbo, wakisikiliza kwa makini maswali yaliyokuwa yakiulizwa na waandishi wa habari wakati wa mkutano huo.
Sehemu ya Waandishi wa habari wa vyombo mbali mbali wakiwa kwenye Mkutano huo,uliofanyika kwenye Hoteli ya Serena,jijini Dar es Salaam leo.

Zitto Kabwe na Kitila Mkumbo wakiingia Ukumbini katika Hoteli ya Serena jijini Dar es Salaam,kwa ajili ya kuzungumza na waandishi wa habari.
Zitto Kabwe, akiagana na baadhi ya waandishi wa habari wakati akiondoka ukumbini.

No comments:

Post a Comment

POSTED TITLE

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...