Wednesday, August 28, 2013

PAMOJA NA CHANGAMOTO ZOTE ULIZOZIPATA ... HONGERA SANA CHAZ BABA



HATIMAYE mwanamuziki wa Bendi ya Mashujaa, Charles Gabriel Cyprian ‘Chaz Baba’ amefunga ndoa na mchumba wake wa muda mrefu aitwaye Rehema Sospeter Marwa lakini mambo kadhaa ya kushangaza yamebainika ambayo ni kati ya kasoro zilizoitia doa sherehe hiyo.



Ndoa hiyo ilifungwa Jumamosi iliyopita katika Kanisa la St. Peter, Oysterbay jijini Dar kisha sherehe zikahamia kwenye Ukumbi wa Marido, Sinza Makaburini ambako shamrashamra zilichukua nafasi.

CHAZ BABA AKIRI KASORO

Akizungumza na gazeti hili juzi, Chaz Baba alisema wakati anatangaza ndoa baadhi ya watu hawakuamini lakini hatimaye ndoto yake hiyo imetimia licha ya kasoro ndogondogo zilizojitokeza.

MIL. 3 ZA MCHANGO ZADAIWA KULIWA

Akifafanua moja kati ya kasoro zilizojitokeza katika sherehe hiyo, Chaz Baba alidai kusikitishwa na kitendo cha muweka hazina wake aliyemtaja kwa jina la Rehema ‘kutia ndani’ sehemu ya fedha za michango zipatazo shilingi milioni 3.

“Sikutegemea mtu kama Rehema kunifanyia hivi, nilimheshimu na kumuamini sana, nikapendekeza apewe jukumu la kutunza fedha matokeo yake amenifanyia hivi,” alidai Chaz Baba.
WANAKAMATI WALEWA KABLA YA WAALIKWA

Kingine kilichoitia dosari sherehe hiyo ni kitendo cha wanakamati kujipendelea katika suala vinywaji na kuwafanya wawe wa kwanza kulewa kabla ya wageni waalikwa.

Mmoja wa wanakamati ambaye kidogo alionekana kuwa mstaarabu aliliambia Risasi kuwa, alishangazwa na jinsi wenzake walivyokuwa wakiichangamkia pombe na kuwaacha wageni wakitoa macho.

“Ona wenzangu walivyolewa, yaani wamejipendelea wao kwanza badala ya kuwahudumia waalikwa, hii inanishangaza sana,” alisema mwanakamati huyo aliyeomba jina lake lisiandikwe gazetini.MADEMU WA CHAZ WAINGIA MITINI

Aidha, licha ya baadhi ya mademu waliowahi kuwa na uhusiano na Chaz Baba akiwemo msanii Husna Idd ‘Sajent’ kutoa ushirikiano katika maandalizi ya sherehe hiyo, wivu uliwazidia na hatimaye kushindwa kuhudhuria.

ILIFANA ILE MBAYA

Licha ya kasoro chache, sherehe hiyo ilifana sana na baada ya kutoka ukumbini maharusi walienda kucheza Twanga.

1 comment:

POSTED TITLE

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...