Tuesday, July 23, 2013

WALIOWAUA WANAJESHI WA TANZANIA WATAJWA.....NI KUNDI LA "JANJAWEED" LINALOUNGWA MKONO NA SERIKALI YA SUDAN



WAKATI miili ya wanajeshi saba ikiwa imeagwa jana katika Viwanja vya Makao Makuu ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania, imeelezwa kuwa kundi la Janjaweed linaloungwa mkono na serikali ya Sudan ndilo lililowavamia na kuwaua askari hao nchini humo na kuwajeruhi wengine 17 .

Wanajeshi hao wa Tanzania ambao walikuwa ni sehemu ya Jeshi la Kulinda Amani la Umoja wa Mataifa (Unamid), walifanyiwa unyama huo Julai 13, mwaka huu katika eneo la kusini mwa Darfur, nchini Sudan.

Kiongozi wa moja ya makundi ya wapiganaji la Sudan Liberation Movement (SLM), Minni Mannawi ameibuka na kuwatuhumu wanamgambo wa Janjaweed wanaoungwa mkono na serikali ya nchi hiyo na ametaka ufanyike uchunguzi wa kimataifa.

Katika mahojiano yake na Gazeti la Sudan Tribune alipokuwa anahudhuria mkutano wa majadiliano kuhusu namna ya kupata amani ya kudumu nchini Sudan uliofanyika jijini Geneva Uswisi wiki iliyopita, alikanusha kuwa kundi lake linahusika na shambulio hilo.

“Tuna uhakika shambulio lililofanywa dhidi ya walinzi wa amani wa Unamid liliandaliwa na kutekelezwa na Janjaweed, tuko tayari kutoa ushirikiano kwa chombo maalum cha kimataifa kitakachoundwa kufanya uchunguzi kuhusu tukio hili…Nashauri serikali (ya Sudan) isishiriki katika uchunguzi kwa sababu itaficha ukweli,” alisema Mannawi.

Aliongeza kuwa wanamgambo hao waliowashambulia wanajeshi wa kulinda amani hivi sasa wanakabiliwa na ukata wa hali ya juu na kukosa vifaa kwa sababu serikali haina tena uwezo wa kuwahifadhi, hivyo wameamua kufanya matukio ya uporaji kukidhi mahitaji yao.

Msemaji wa Katibu Mkuu wa UN, Martin Nesirky alisema wameanza kufanya uchunguzi wao binafsi. Taarifa ya UN ilieleza juzi kuwa mashuhuda wamekuwa wakieleza mauaji hayo yamefanywa na kundi linaloungwa mkono na serikali ya Sudan.

Wakati huo huo, majeshi ya Nigeria yamejitoa kulinda amani Darfur. Hazikutolewa sababu za kufanya hivyo japokuwa UN imethibitisha.

No comments:

Post a Comment

POSTED TITLE

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...