Friday, July 19, 2013

CHADEMA WAJITOA KUWANIA UMEYA JIJI LA ARUSHA



Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kimeamua kuachana na kuwania umeya wa Jiji na badala yake kimemwomba Meya, Gaudence Lyimo (CCM), atende haki.

Katibu wa Kanda ya Kaskazini wa chama hicho, Amani Golugwa alisema jana, kwamba Chadema haina uroho wa madaraka kama baadhi ya watu wanavyofikiri, bali inasimamia vipaumbele vya maendeleo.

Hata hivyo, kauli hiyo inapingana na nyingine ya chama hicho ya wiki hii pia, kwamba ushindi katika uchaguzi mdogo wa kata nne, ni chachu katika msimamo wa chama kutaka uchaguzi wa Meya wa Jiji la Arusha, urudiwe.

Mwenyekiti wa Madiwani wa Chadema, Isaya Doita, ndiye aliyenukuliwa wiki hii akisema hayo, akiamini kuwa Meya Lyimo wa CCM, alichaguliwa kimizengwe.

Baada ya Chadema kutetea viti vyake vinne vya udiwani kwenye uchaguzi mdogo wa hivi karibuni, kimefikisha viti 15 kwenye Baraza la Madiwani la Arusha, huku CCM ikibaki na viti 12 na TLP sita.

Pia Chadema ina nafasi ya kuongeza kiti, kwani ina nafasi moja ya viti maalumu iliyokuwa inakaliwa na Rehema Mohamed, aliyetimuliwa mwaka 2011.

Hata hivyo, pamoja na Chadema kuongoza kwa kuwa na viti vingi vya udiwani jijini hapa, haina uwezo wa kuweka Meya, bila kushirikiana na CCM au TLP.

Chadema ikikosa ushirikiano huo, ushirikiano wa CCM na TLP, utabaki kuwa na nguvu ya kuweka Meya na naibu wake madarakani, huku Chadema ikibaki kuwa kambi ya upinzani yenye nguvu katika Baraza la Madiwani.

Golugwa alisema Chadema haina uroho wa madaraka, bali inataka uchaguzi wa Meya wa Jiji urudiwe ingawa haitaki nafasi hiyo kwa kuwa si kipaumbele chake.

"Tunaangalia wananchi wanafikiwaje na maendeleo tuna imani muda si mrefu Jiji la Arusha litapata Meya ambaye amechaguliwa kwa misingi ya sheria," alisema Golugwa.

"Hatuna shida na Meya wala hatuna uroho wa madaraka tunachopinga ni upatikanaji wa Meya huyo na tunamtaka afanye kazi zake kwa kusimamia misingi ya sheria na si upendeleo, tunahitaji kuona kila mwananchi ananufaika na maendeleo hadi mitaani," aliongeza.

Pia alikaririwa wakati mmoja akisema ushindi huo unaihakikishia Chadema wingi wa wajumbe katika Baraza la Madiwani, hivyo kuwa na fursa ya kumwondoa Lyimo madarakani.

No comments:

Post a Comment

POSTED TITLE

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...