Tuesday, February 12, 2013


"RAIS KIKWETE AMJIBU LOWASSA TATIZO LA AJIRA NCHINI



Rais Kikwete ambaye alikuwa akifungua semina ya siku mbili ya Wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM mjini Dodoma jana, alisema kusimama jukwaani na kusema kwamba ajira ni tatizo hakuna maana ikiwa mhusika hatoi pendekezo la jinsi ya kumaliza tatizo hilo.
MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rais Jakaya Kikwete katika hali inayoashiria kumjibu rafiki yake, Edward Lowassa ameponda makada wa chama hicho ambao wamekuwa wakipanda jukwaani kuhubiri kuwa ajira ni tatizo pasipo kupendekeza suluhisho la tatizo hilo.

Rais Kikwete ambaye alikuwa akifungua semina ya siku mbili ya Wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM mjini Dodoma jana, alisema kusimama jukwaani na kusema kwamba ajira ni tatizo hakuna maana ikiwa mhusika hatoi pendekezo la jinsi ya kumaliza tatizo hilo.

Ingawa hakutaja majina ya wanasiasa ambao wamekuwa wakizungumzia suala hilo lakini Lowassa, ambaye alijiuzulu wadhifa wa Waziri Mkuu mwaka 2008, amenukuliwa mara nyingi akiitaka Serikali kuchukua hatua za kukabiliana na tatizo la ajira kwa maneno kwamba ‘ni bomu linalosubiri kulipuka’.

Lowassa, ambaye ni Mbunge wa Monduli kupitia CCM, aliwahi kuingia hata kwenye malumbano makali na Waziri wa Kazi na Ajira, Gaudensia Kabaka.

Kabaka akiwa bungeni mjini Dodoma, Machi 21, 2012 alilazimika kutoa takwimu za namna Serikali ilivyokuwa inatengeneza ajira kwa nia ya kumjibu Lowassa, ambaye alikuwa ameeleza tatizo la ajira linavyowaathiri vijana kwenye moja ya hafla.

Lowassa ameendelea kuzungumzia suala hilo mara kwa mara kila anapopata fursa ya kuhutubia.

“Ndiyo ajira ni tatizo, hapa mkakati ni ajira itapatikana vipi? Ni tatizo kweli, tunafanyaje na tunalitatua vipi? Tunataka mtu anayesema kwamba ni tatizo na apendekeze pia suluhu yake,” alisema Rais Kikwete, ambaye aliwahi kutamka kuwa Lowassa ni rafiki yake na anafahamika kuwa alishirikiana naye katika harakati zake za kuwania urais mwaka 2005, na baadaye akamteua kuwa Waziri Mkuu.

Lowassa, ambaye ni miongoni wa makada wa CCM wanaotajwa kuwania urais mwaka 2015, alikaririwa akisema Oktoba 19, 2011 kuwa; “Sijakutana na Rais Kikwete barabarani, watu waache kunichonganisha naye.” Ilikuwa katika mkutano na waandishi wa habari jimboni kwake Monduli.

Suala la ajira nchini ni moja ya mada zinazotarajiwa kuwasilishwa kisha kujadiliwa katika semina hiyo ya CCM, na Rais Kikwete aliwataka wajumbe kupendekeza jinsi ya kuongeza ajira nchini wakati mjadala husika utakapowadia.

Hata hivyo, Rais Kikwete alisema hivi sasa ajira katika sekta ya umma ni kama hakuna, kwani zimebaki sekta za afya na elimu na kwamba hivi sasa suluhu ni kukuza sekta binafsi ili kuongeza ajira.

Alitoa mfano kwamba wakati yeye alipohitimu kidato cha nne, cha sita na chuo kikuu hakukuwa na tatizo la ajira kwa kuwa idadi ya wasomi ilikuwa ndogo ikilinganishwa na mahitaji ya sasa ya soko hilo.

Kikwete alisema wakati huo Serikali ilikuwa haijajitosheleza, tofauti na sasa ambapo imefikia ukomo wa kuajiri isipokuwa kwa sekta mbili tu.

“Kwa sasa Serikali haina uwezo tena wa kuajiri, ilifika mahali kila kiongozi anaenda kuomba serikalini na kupeleka watu wake, unakuta anatoka Kikwete anaomba mtoto wake aajiriwe, mara Katibu Mkuu naye anapeleka watu wake, ikafika mahali mashirika yakajaa tukapata kazi ya kuwapunguza,” alisema Rais Kikwete.

Rais Kikwete alisema sehemu kubwa ya ajira inatoka katika sekta binafsi na jambo la msingi ni kwa viongozi kushirikiana na Serikali kuona ni kwa jinsi gani wanaweza kuikuza.

“Tutaendelea kuwaita wawekezaji wezi halafu tunataka kukuza ajira? Tunazipataje nafasi zaidi, wakiwekeza wanafanyiwa fujo wasiwekeze,” aliongeza Rais Kikwete, ambaye bila kuingia kwa undani kuhusu fujo lakini wafuatiliaji wa mambo wanaweza kuoanisha kauli hiyo na vurugu zilizotokea hivi karibuni mkoani Mtwara ambako wananchi wanapinga ujenzi wa bomba la gesi kwenda Dar es Salaam.

Maadili ndani ya CCM
Kuhusu maadili, Rais Kikwete alionyesha kukerwa na baadhi ya viongozi wa chama hicho kutumia majukwaa kukosoa uongozi uliopo na kusahau majukumu yao kama viongozi.
“Hakuna haja ya viongozi kuwa mahodari wa kuongea kama kuna matatizo. Tatueni matatizo huko yakiwashinda tuleteeni ngazi ya juu,” alionya Rais Kikwete.

Kikwete pia alionyeshwa kukerwa na baadhi ya viongozi wenye maadili mabovu huku akitoa mfano wa viongozi wanaolewa ovyo na kukopakopa fedha kwa watu.

“Yapo mambo ambayo lazima tuyazungumze vizuri, huwezi kuwa mwenyekiti kazi yako ni kukopakopa tu, halafu unalewa hadi unakuwa wa mwisho baa. Unamalizia pombe zako kwa kusema Kidumu Chama Cha Mapinduzi.

“Unajenga taswira gani ya kwako na chama chako.
Ukishakuwa kiongozi unabeba dhamana kubwa ya chama chako, matokeo yake taswira ya chama mbele za watu inakuwa chama cha walevi.

Kamati Kuu siri
Rais Kikwete pia aliwatahadharisha wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa, kuwa hakuna mtu anayejua orodha ya wajumbe watakaoteuliwa katika Kamati Kuu (CC) zaidi yake.

“Niwatahadharishe tu kwamba asiwadanganye mtu kwamba orodha ndiyo hii au hawa ndiyo watakaochaguliwa. Anapoteza muda wake tu kwani kama alikuwa anakunywa pombe mwongezee chupa nyingine ili aondoke.

“Orodha haijatengenezwa, Rais amefika leo (jana) asubuhi, Makamu Mweyekiti naye amefika leo (jana) tutakaa sasa na kesho wala msiamke kwa kufikiria usiku huu mtapata orodha. Msisumbuke kufanya mikutano ya kuunga mkono watu wenu kwani orodha hiyo wala haina fulani. Nimesikia kuna watu wanasambaza orodha zao, nashangaa kuna wajumbe wa NEC, ambao ni hatari kwa chama chetu.”

Kikwete aliwaonya wajumbe wapya kuacha kuunda magenge kwani hayatawasaidia.

“Nasema hivi kutengeneza magenge ili fulani aharibikiwe ni jambo ambalo halina tija, unajitia kihoro bure. Uliyetaka aharibikiwe, hakuharibikiwa, kwa nini mnaenda kufanya biashara ambayo haina maana? Wekezeni kwenye kitu chenye maana, haya mambo ya kukaa vigenge wakati orodha yenyewe haipo ni kujisumbua. Lakini akili ni nywele na kila mtu ana zake,” alisisitiza.

Kikwete alisema wale wanaoingia kwa mara ya kwanza NEC wajishirikishe katika mambo ya kujenga na si kubomoa chama kwa kuwa unajipa kihoro hasa pale unapotaka mtu aharibikiwe na matokeo yake mtu huyo anafanikiwa zaidi.

No comments:

Post a Comment

POSTED TITLE

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...