Thursday, February 7, 2013

MAGUNIA MENGINE 97 YA BANGI YAKAMATWA NA JESHI LA POLISI ARUSHA



Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha Kamishna Msaidizi wa Polisi Liberatus Sabas akiwaonyesha waandishi wa habari madawa ya kulevya aina ya bangi ambayo yalikuwa kwenye magunia 97 yaliyokamatwa na askari wa jeshi hilo katika eneo la Usa river wilayani Arumeru (Picha na Rashid Nchimbi wa Jeshi la Polisi)

Askari wa jeshi la polisi wakiwa wanashusha magunia ya madawa ya kulevya aina ya bangi mara baada ya kukamatwa eneo la Usa River wilayani Arumeru yakiwa yanasafirishwa kwenye gari aina ya Fuso lenye namba za usajili T.282 AAJ kuelekea Moshi (Picha na Rashid Nchimbi wa jeshi la Polisi Arusha)
Na: Rashid Nchimbi wa Jeshi la Polisi Arusha
Jeshi la Polisi mkoani hapa limemkamata mtu mmoja akiwa na magunia 97 ya madawa ya kulevya aina ya bangi ambayo yalikuwa yanasafirishwa toka mkoani hapa kuelekea Moshi. Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha Kamishna Msaidizi wa Polisi Liberatus Sabas amesema...


kwamba, tukio hilo lilitokea muda wa saa 10:00 alfajiri eneo la Usa River wilayani Arumeru.
Alisema mafanikio hayo yametokana na ushirikiano mzuri kati ya jeshi hilo na wananchi ambapo taarifa za tukio hilo zilitolewa na raia wema ambapo askari wa jeshi hilo waliweka mtego eneo hilo na kufanikiwa kulikamata gari aina ya Fuso lenye namba za usajili T. 282 AAJ.
Kamanda Sabas aliongeza kwa kusema kwamba, ndani ya bodi ya gari hilo kulikuwa na mboga aina ya kabeji iliyosambazwa vizuri huku chini ya mboga hiyo kukiwa na madawa hayo yaliyokuwa kwenye magunia huku yakivingirishwa kwenye mifuko ya “plastiki” kwa ndani.
Alisema katika gari hilo kulikuwa na watu watatu na mara baada ya askari hao kulisimamisha dereva pamoja na msaidizi wake walifanikiwa kukimbia huku mtu mmoja aliyejulikana kwa jina la Praygod Marick (22) Mkazi wa Dar esalaam akikamatwa.
Jeshi la polisi Mkoani hapa linaendelea kumhoji mtuhumiwa huyo huku watuhumiwa wengine wakiendelea kutafutwa. Kwa mara nyingine tena Kamanda huyo aliendelea kuwashukuru wananchi wa Mkoa huu kutokana na ushirikiano wao mkubwa wanaoutoa kwa jeshi hilo na kuendelea kuwasisitizia kuimarisha mahusiano na jeshi hilo.
Kwa muda wa kipindi cha mwezi mmoja toka januari 07, 2013 mpaka hivi leo jeshi hilo limeshakamata madawa ya kulevya aina ya mirungi magunia 372 katika magari mawili tofauti na pia limeshakamata jumla ya magunia 117 ya madawa ya kulevya aina ya bangi ambapo mwanzoni mwa wiki hii jumla ya magunia 20 yalikamatwa yakiwa yanasafirishwa kwa kutumia wanyama aina ya Punda maeneo ya Losoiti wilayani Longido

No comments:

Post a Comment

POSTED TITLE

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...