Saturday, February 23, 2013

CHADEMA: Kawambwa amebakiza siku kumi



Mkurugenzi wa Habari na Uenezi, John Mnyika

KAULI ya Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk. Shukuru Kawambwa kwamba hawezi kujiuzulu, imeamsha hasira ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), ambacho kimesisitiza kwamba maandamano ya kumng’oa yako pale pale na sasa amebakiza siku kumi.


Kauli hiyo ilitolewa jana na Mkurugenzi wa Habari na Uenezi, John Mnyika wakati alipotakiwa kueleza msimamo wa chama chao, hasa baada ya kauli ya Waziri Kawambwa jana kwamba hawezi kujiuzulu.


Akizungumza na gazeti hili jana, Mnyika ambaye ni Mbunge wa Ubungo, alisema kauli aliyoitoa Mwenyekiti wa chama hicho taifa, Freeman Mbowe kwamba anampa siku 14 Waziri Kawambwa ajiuzulu, vinginevyo atang’olewa kwa maandamano bado ipo pale pale.


Alisema majibu ya Waziri Kawambwa yameonesha dharau kwa Watanzania, hasa walalahoi ambao ndio watoto wao wengi wamepata ziro katika mitihani yao ya kidato cha nne.


“CHADEMA tunaendelea kusisitiza kwamba Waziri Kawambwa ang’oke, awajibike, ameshindwa kazi na hili tunamaanisha,” alisisitiza Mnyika.


Alisema CHADEMA inaangalia namna ya kuitisha maandamano hayo kwa kuwashirikisha vijana waliofeli kwani wanaamini wamehujumiwa.


Mnyika aliwataka Watanzania na wengine wenye uchungu na udhaifu wa elimu ya Tanzania, hasa wazazi wajitokeze kwani fedha walizowekeza kwa watoto wao kwa ajili ya elimu, zimeteketea.


Wakati akihutubia mkutano mkubwa wa hadhara uliofanyika hivi karibuni katika viwanja vya Furahisha, Manispaa ya Ilemela mkoani Mwanza, ikiwa ni ufunguzi wa Baraza la Viongozi wa CHADEMA, Kanda ya Ziwa Magharibi, Mbowe alitoa siku 14 kwa Dk. Kawambwa na Naibu wake, Philipo Mulugo, kuhakikisha wamejiuzulu nyadhifa zao.



Mbowe ambaye aliongoza maandamano makubwa ya magari na pikipiki kuelekea uwanjani hapo, alisema Kawambwa, naibu wake, Mulugo, pamoja na katibu mkuu wa wizara hiyo, wameshindwa kuiongoza sekta hiyo muhimu, ndiyo maana kwa sasa wanafunzi wanaishia kuandika matusi na kupata sifuri katika mitihani.


Alisema waziri huyo lazima ajiuzulu nafasi hiyo, kwani taifa ameliingiza pabaya na kuanza kuzalisha maelfu ya watoto wa maskini kumaliza elimu zao za msingi na sekondari wakiwa hawajui kusoma na kuandika.


Alisema hili ni janga la kitaifa, hivyo lazima Kawambwa aondoke ndani ya wiki mbili, vinginevyo CHADEMA itaitisha maandamano makubwa nchi nzima kushinikiza kiongozi huyo ang’oke madarakani.


“Kwa vile Kawambwa ameshindwa kuisimamia vema sekta hii ya elimu, na kwa vile watoto wetu wengi wanafeli na kuishia kuandika matusi kwenye mitihani yao, CHADEMA tunampa wiki mbili awe amejiuzulu.


“Kila mwaka wanafunzi 1,200,000 hadi 1,300,000 nchi nzima wanafanya mitihani yao. Lakini wanaoshinda ni kati ya 35,000 hadi 400,000 pekee, hivyo watoto wengine wanashindwa kuendelea na masomo yao. Kwa hiyo tunataka huyu waziri na naibu wake wajiuzulu ndani ya wiki mbili,” alisema Mbowe.


Alisema kwa sasa Tanzania inazalisha vijana wapatao 800,000 kwa mwaka ambao wanakosa fursa ya kuendelea na masomo yao, na alimtaka Rais Jakaya Kikwete kuacha kucheka na kubembeleza viongozi wabovu wanaodidimiza maendeleo ya nchi na raia wake, na kwamba Tanzania inakabiliwa na majanga makubwa mawili ya elimu duni na udini.


Naye Naibu Katibu Mkuu wa CHADEMA, Zitto Kabwe, alimtaka Waziri Kawambwa na Naibu wake, Mulugo, kuwajibika na kupisha katika wizara hiyo.


Pia alimtaka Rais Kikwete aichukue wizara hiyo na kuwa chini ya ofisi yake.


Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari, Zitto alisema kuwa ni muhimu viongozi wanaosimamia wizara hiyo wakawajibika.


Alisema uwajibikaji huo unapaswa kufanyika kuanzia kwa katibu mkuu wa wizara hiyo pamoja na kamishna.


Zitto alisema kuwa rais anapaswa aelezwe kuwa iwapo matokeo yatabaki hivi mwakani, na yeye atatakiwa kuondoka katika nafasi hiyo.


Chanzo: Tanzania Daima

No comments:

Post a Comment

POSTED TITLE

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...