BENKI ya Barclays Tanzania (BBT) imetangazwa kuwa mshindi wa Tuzo ya Benki Bora kwa mwaka 2012 hapa Tanzania. Taarifa hiyo ilitolewa jijini London, Uingereza, Alhamisi ya Novemba 29 mwaka huu wakati wa hafla ya Tuzo za Benki ya Mwaka zinazoratibiwa na kusimamiwa na gazeti la Financial Times.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo, Mkurugenzi Mtendaji wa BBT, Bwana Kihara Maina alisema: “Lengo letu ifikapo mwaka 2015 ni kuhakikisha kila mtu anataka kuja kwetu kwa kupitia kauli mbiu ya ‘Kaweke Pesa Benki’ (Go-to-bank). Heshima hii kubwa kwetu imeletwa na moyo wa kujitoa wa wafanyakazi kwa kuwahudumia vyema wateja wetu na hivyo kuyarahisisha maisha yao.”
Bw.Maina aliongeza: “Kwa jumla Tanzania kuna benki 50 na kuchaguliwa kuwa Benki Bora nchini ni furaha kubwa kwa wanafamiliwa wa Barclays, wateja na wadau wote. Hii ni kwa kutambua uwekezaji wetu mkubwa tulioufanya katika biashara ili kutoa huduma bora kwa wateja wetu.
Tunawaahidi Watanzania kuwa tutawekeza zaidi na kutoa huduma za kibenki zinazokubalika duniani.”
Kwa mujibu wa jarida lifahamikalo kama ‘The Banker Magazine’, Barclays imeshinda tuzo hiyo ya mwaka kutokana na matumizi ya Teknolojia ya Mawasiliano kama vile uwekezaji katika mfumo wa kazi (workflow and imaging systems), kuanzisha huduma za bure za ATM, kuanzisha huduma za kibenki kwa njia ya mtandao, maendeleo katika biashata ndogo ndogo na za kati (SMEs) na kuongezeka kwa faida mwaka 2010 na 2011.
No comments:
Post a Comment