Friday, October 5, 2012

WALIMU WAGOMEA SIKU YAO


 
CHAMA cha Walimu Tanzania (CWT) kimegoma kushiriki maadhimisho ya Siku ya Walimu Duniani inayoadhimishwa leo kwa madai kina huzuni na hakina mafanikio yoyote ya kuwaambia walimu.
Aidha, chama hicho kimetoa mwito kwa Serikali kukubali ushauri wa Bunge na uamuzi wa Mahakama, ili warudi katika meza ya majadiliano kwa ajili ya kuendeleza walipoachia.
Katibu wa CWT, Ezekiel Oluoch alisema hayo jana Dar es Salaam wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maadhimisho hayo ambayo kaulimbiu yake ni ‘Kuwatetea walimu’.
“Kesho (leo) ni Siku ya Walimu Duniani, kwa bahati mbaya hatutakuwa na sherehe ama maadhimisho kwani hakuna chochote cha kuelezea … hatuwezi kusherehekea tukiwa na matatizo mengi ambayo hayajafikia suluhu,” alisema Oluoch na kuongeza kuwa wataadhimisha siku yao wakiwa kazini na wamekata tamaa.
Alisema mwajiri wao ambaye ni Serikali hajalipa madai ya wakufunzi wa vyuo vya ualimu, hajashughulikia madai ya walimu ambayo hayajalipwa na kutoajiri walimu waliohitimu ingawa fedha zimetengwa na Bunge.
Alisema katika siku hiyo, CWT inatoa mwito kwa Watanzania na jumuiya za kimataifa kujitokeza kutetea walimu dhidi ya manyanyaso wanayopata kutokana na mishahara duni isiyokidhi mahitaji muhimu ya kila siku.
Pia alitaka walimu kushikamana katika kudai maslahi bora zaidi kama watumishi wengine wa umma na Serikali ilipe madeni yote wanayodai walimu, wakufunzi wa vyuo vya ualimu nchini pamoja na wakaguzi wa shule.
Kuhusu kurudi katika meza ya majadiliano, Rais wa CWT, Gratian Mukoba alidai Serikali imegoma kukutana na chama hicho kama ilivyoagizwa na Mahakama na Bunge.
Alisema pamoja na leo kuwa Siku ya Walimu, Serikali imekataa mapendekezo ya CWT ya kuteua timu ya majadiliano nje ya chombo cha majadiliano ya pamoja kwenye utumishi wa ualimu ili madai ya walimu yashughulikiwe ndani ya mwaka huu wa fedha.
“Hadi sasa Serikali imekiuka amri ya Mahakama ya Kazi ambayo iliagiza pande zote, yaani CWT na Serikali zirudi kwenye meza ya majadiliano… kwa uelewa wetu, meza iliyokuwa inatumika kwa majadiliano kabla ya mgomo ndiyo inayostahili kutumika kuendeleza mazungumzo kati ya pande hizi,” alisema Mukoba.
Alisema CWT inalaani kwa nguvu zote ukaidi huo wa Serikali ambao hauna tija kwa nchi, bali unazidi kuwasababishia walimu kuishi maisha magumu yasiyo na mfano na kudhulumu wanafunzi haki yao ya kupata elimu.
Akijibu hoja ya Serikali kukaidi uamuzi wa Mahakama na Bunge, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Celina Kombani alisema Serikali inapanga tarehe mwafaka ya kukutana na kwamba haijakaidi agizo hilo.
Alisema baada ya CWT kuwaandikia wako katika majadiliano na kwamba wameahidi kukutana ili kuzungumza.

No comments:

Post a Comment

POSTED TITLE

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...