Tuesday, September 18, 2012

MTAKATIFU TOM AENDA NA WACHEZAJI 18 MOROGORO, ASEMA PIGA UA UBINGWA NI WA YANGA TU


Mtakatifu Tom akiwaongoza vijana wake

KOCHA Mkuu wa Yanga, Mbelgiji Tom Saintfiet amewaomba radhi mashabiki wa Yanga kwa sare ya Jumamosi kwenye Uwanja wa Sokoine na amesema kesho anapeleka wachezaji 18 Morogoro kwa ajili ya mechi ya pili ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara dhidi ya Mtibwa Sugar, akiwa ana matumaini makubwa ya ushindi.
Saintfiet amesema leo kwamba sababu nyingi zilichangia Yanga kutocheza kwa ubora wake Mbeya, ikiwemo hoteli mbaya na chakula kibaya na kwa ujumla alisema hawakuwa vizuri kabla ya mechi hiyo.
“Mimi kwa mfano sijaoga siku mbili, kwa kweli tulikuwa katika mazingira magumu na wapinzani wetu walicheza soka ya kuudhi tangu mwanzo, kupoteza muda, na marefa hawakuchukua hatua, tulipoteza nafasi kupitia kwa Kiiza (Hamisi) na Msuva (Simon), siwezi kulaumu mchezaji wangu yeyote, lakini hiyo ndiyo hali halisi,”alisema Saintfiet.
Alisema kesho asubuhi timu itafanya mazoezi kwenye Uwanja wa sekondari ya Loyola, Mabibo, Dar es Salaam na saa 8:00 mchana watasafiri kwa njia ya barabaraba kwenda Morogoro ambako wakifika watatafuta hoteli nzuri mapema.
Alisema anajua hata Uwanja wa huko, Jamhuri si mzuri na mechi itakuwa ngumu kwa sababu Mtibwa Sugar nao walitoka sare ya bila kufungana na Polisi katika mchezo wao wa kwanza Jumamosi na anaiheshimu timu hiyo kama moja ya timu tano kubwa Tanzania, pamoja na Simba, Azam na Coastal Union.
“Lakini pamoja na kwamba Simba wamependelewa kupangiwa ratiba ya kuanza kucheza nyumbani mechi tano mfululiuzo, nakuambia Mei mwaka 2013 Yanga ndio itavishwa taji la ubingwa wa Ligi Kuu, acha wafurahie sasa hivi, watalia mwisho,”alisema Mtakatifu Tom.
Kuhusu wachezaji 18 anaokwenda nao Morogoro, Mtakatifu Tom alisema atawataja baada ya mazoezi ya kesho na hiyo inaonekana ni kwa sababu ya kufuatilia hali za wachezaji ambao kwa sasa hawako vizuri, akiwemo kiungo Haruna Niyonzima.
Wachezaji aliokwenda nao Mbeya walikuwa ni makipa; Yaw Berko, Ally Mustafa ‘Barthez’, mabeki Shadrack Nsajigwa, Juma abdul, Godfrey Taita, Mbuyu Twite, Kevin Yondan, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, David Luhende, Oscar Joshua na Stefano Mwasyika. Aliwataja viungo ni Athumani Iddi ‘Chuji’, Haruna Niyonzima, Frank Domayo, Rashid Gumbo, Nizar khalfan, Shamte Ally na Simon Msuva, wakati washambuliaji ni Jerry Tegete, Didier Kavumbangu, Said Bahanuzi na Hamisi Kiiza, wakati waliobaki walikuwa ni kipa Said Mohamed, mabeki Ladislaus Mbogo, Job Ibrahim, viungo Juma Seif ‘Kijiko’, Salum Telela, Omega Seme, Nurdin Bakari, Idrisa Assega na Issa Ngao wa Yanga B, anayekomazwa kikosi cha kwanza.

No comments:

Post a Comment

POSTED TITLE

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...