Monday, September 10, 2012

HIVI NDIVYO YONDAN ALIVYOTEKWA, ALIVYOJINASUA KWENYE MAKUCHA YA MNYAMA SIMBA HADI KUFUNGUA KESI POLISI


Mateka Yondan

WAKATI leo Kamati ya Sheria, Maadili na Hadhi za Wachezaji ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), chini ya Mwenyekiti wake, Alex Mgongolwa inatarajiwa kutoa uamuzi kuhusu kesi za mabeki wawili wa Yanga, Mbuyu Twite na Kevin Yondan, ambao usajili wao unapingwa na Simba, sakata hilo limechukua sura mpya jana.
Inadaiwa Yondan jana alitekwa na klabu yake ya zamani, Simba SC katika kile kinachoelezwa jitihada za kumrudisha nyumbani, lakini dili hilo likakwama baada ya mchezaji mwenyewe kuwatoroka viongozi wa Simba.
Akizungumza na BIN ZUBEIRY jana usiku, Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Yanga, Abdallah Ahmad Bin Kleb alisema kwamba mchezaji wa zamani wa Simba, ambaye aliwahi kukutwa na kashfa ya kutaka kumhonga mchezaji wa timu pinzani akitumiwa na klabu yake hiyo, ndiye aliyemuingiza Yondan kwenye mtego.
“……..alikwenda kwa Yondan, akasema amekwenda kumsalimia na kwa kuwa wanafahamiana wamewahi kucheza wote wa Simba, Yondan hakuwa na tatizo. Baada ya mazungumzo akaaga anaondoka, akaomba asindikizwe hadi mjini, kufika mbele kidogo, yule mchezaji akaomba aendeshe gari la Yondan. Yondan akampa.
Yule jamaa akapeleka lile gari moja kwa moja hadi kwa…………..(kiongozi wa juu wa Simba), kufika wakaingia ndani, Yondan anamuuliza huku wapi tena, ooh naenda kuchukua mpunga (fedha) kidogo kwa…..(huyo kiongozi). Walipofika, akamshawishi Yondan waingie naye ndani, na kwa kuwa Yondan alikuwa anajiamini, akashuka wakaingia.
Kufika, jamaa (kiongozi) akamtolea (Yondan) Sh. Milioni 20 ili asaini fomu za Simba na muda ule ule azungumze na Radio Clouds kutangaza kwamba yeye ni mchezaji halali wa Simba, Yondan akakataa. Jamaa akaongeza burungutu la fedha, bado mchezaji akakataa. Alipoona anazidi kubanwa, akaomba aende chooni mara moja. Ndipo alipotoka akampigia simu Seif (Ahmad ‘Magari’) kumuambia haraka haraka kinachoendelea.
Seif akamuambia ajitahidi atoke nje ya jengo hilo na gari lake aliache tu humo ndani, kwa kuwa ufunguo wa gari lake alikuwa nao huyo mchezaji aliyetumwa, wale kule wakajiamini atarudi tu. Yondan akafanikiwa kutoka na anafika tu nje ya geti, tayari mtu kafika kumchukua na baada ya muda Seif naye akafika.
Kule ndani walipoona Yondan harudi, yule mchezaji akatumwa kutoka kumfuatilia, akatoka nje akakutana na Seif, akamkamata akampakia kwenye gari akaondoka nao wote.
Sema naye yule (mchezaji aliyetumwa) kule mbele akafanikiwa kumtoroka Seif, ila kesi imefunguliwa Polisi dhidi ya huyo kiongozi wa Simba na huyo mchezaji. Na aliyefungua ni Yondan mwenyewe. Sasa hii ndio picha halisi,”alidai Bin Kleb.
Ikumbukwe, mapema Jumatatu wiki iliyopita, kikao cha baina ya klabu hizo mbele ya Kamati ya Sheria, Maadili na Hadhi za Wachezaji ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), chini ya Mwenyekiti wake, Alex Mgongolwa, kilivunjika bila kufikia makubaliano kuhusu pingamizi za Simba dhidi ya Yanga.
Katika kikao hicho kilichoanza majira ya saa 7:00 mchana, hoja ya kwanza kuwasilishwa mezani ilikuwa ni suala la beki Twite na upande wa Yanga uliwakilishwa na Sanga na Katibu, Celestine Mwesigwa wakati kwa Simba walikuwepo Makamu Mwenyekiti, Geoffrey Nyange ‘Kaburu’ na Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili, Kapteni wa zamani wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ), Zacharia Hans Poppe.
Ikumbukwe, Simba iliwasilisha malalamiko ya kufanyiwa mchezo usio wa kiungwana na Yanga kwa Twite. Ilidai Twite alisaini mkataba na klabu yao Agosti 1, mwaka huu mbele yao, viongozi wa Shirikisho la Soka Rwanda (FERWAFA) na APR na kulipwa dola za Kimarekani 30,000 na nyingine 2,000 za nauli ya kuja Dar es Salaam kujiunga na klabu hiyo. Hata hivyo, mchezaji huyo akahamia Yanga.
Katika mjadala huo, Simba ilikubali kurudishiwa fedha zao, lakini viongozi wa Yanga wakasema hawawezi kutoa hadi waombwe radhi na Mwenyekiti wa Simba, Alhaj Ismail Aden Rage, ambaye alisema viongozi wa klabu hiyo yenye maskani yake makutano ya mitaa ya Twiga na Jangwani wana ‘fedha chafu za EPA’.
Simba wakasema kauli yake ya Rage ilikuwa sehemu ya utani wa jadi, kama ambavyo Yanga walimvalisha jezi Twite yenye jina la Rage.
Kufikia hapo, Simba wakasema hawawezi hata kujadili suala la Kevin Yondan na Kamati ya Mgongolwa ikasema itapitia maelezo ya pande zote, watatoa majibu kwa mujibu wa kanuni na sheria Septemba 10, mwaka huu, yaani leo.
Katika kesi ya Yondan, walalamikaji ni Simba, ambao wanadai beki huyo alisaini Yanga akiwa bado ana mkataba na klabu yao.
Awali, Kamati ya Mgongolwa ilikutana Jumapili iliyopita asubuhi hadi usiku, bila kupata suluhisho la pingamizi hizo na kuamua kutumia busara ya kuzikutanisha pande zinazopingana kujaribu kupata suluhu siku iliyofuata.
Pingamizi nyingine zilikuwa ni, Azam inayopinga usajili wa Ramadhan Chombo ‘Redondo’ kwenda Simba kwa maelezo bado ina mkataba naye unaomalizika Juni 11 mwakani na inaelezwa tayari klabu hizo zimekwishamalizana juu ya kiungo huyo.
Yanga inapinga Simba kuwaacha wachezaji Dan Mrwanda, Haruna Shamte, Kanu Mbiyavanga na Lino Masombo kwa maelezo walishapatiwa leseni za kucheza Ligi ya Tanzania walizozitumia kwenye mashindano ya Kombe la Kagame. Pia inapinga Ramadhan Chombo ‘Redondo’ kujiunga Simba kwa vile ana leseni ya kuchezea Azam kwa msimu wa 2012/2013.
Pingamizi lingine la Yanga kwa Simba ni kuwa imezidisha idadi ya wachezaji wa kigeni wanaotakiwa kusajiliwa kwa maelezo inao wanane wakati wanaoruhusiwa ni watano. Imewataja wachezaji hao kuwa ni Lino Masombo, Felix Sunzu, Emmanuel Okwi, Mussa Mude, Kanu Mbiyavanga, Pascal Ochieng, Komalmbil Keita na Daniel Akuffor.
Pingamizi nyingine ambazo jumla zinahusu wachezaji 17 walioombewa usajili katika timu za Ligi Kuu ni Toto Africans ya Mwanza imewawekea pingamizi wachezaji Enyinna Darlington aliyeombewa usajili Kagera Sugar, na Mohamed Soud anayekwenda Coastal Union kwa maelezo kuwa bado ina mikataba na wachezaji hao.
Pia Flamingo ya Arusha inapinga usajili wa wachezaji wake Kelvin Friday Iddy katika timu za Azam na Salim Walii (Polisi Mara) kwa vile taratibu za kuwahamisha bado hazijafanywa. Nayo Kagera Sugar inapinga usajili wa beki David Charles Luhende kwenda Yanga kwa vile ada ya uhamisho haijalipwa.
Super Falcon ya Chanjamjawiri, Chakechake, Pemba inapinga wachezaji wake wanne; Edward Christopher Shija, Samir Said Luhava (Simba), Robert Joseph Mkhotya (African Lyon) na Sultan Juma Shija (Coastal Union) kusajiliwa katika timu hizo kwa maelezo taratibu halali za uhamisho hazikufuatwa.
Mchezaji Othman Hassan aliyeombewa usajili Coastal Union anapingwa na Oljoro JKT kwa vile bado ana mkataba na timu hiyo unaomalizika Mei 24, 2013. Nayo Rollingstone Multipurpose Ateclass Foundation ya Arusha inapinga usajili wa Kigi Makassy kutoka Yanga kwenda Simba hadi itakapolipwa fidia ya kumlea mchezaji huyo kwa vile bado hajafikisha umri wa miaka 23. Pingamizi zote zitatolewa majibu leo na Kamati ya Mgongolwa.

No comments:

Post a Comment

POSTED TITLE

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...