Taifa
Stars imetoka sare ya mabao 3-3 na wenyeji Botswana (Zebras) katika
moja kati ya mechi kadhaa za kirafiki za kalenda ya Shirikisho la
Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) zilizochezwa leo (Agosti 15 mwaka
huu) usiku.
Hadi mapumziko kwenye mechi hiyo iliyochezwa Uwanja wa Molepolole ulioko Kilometa 40 nje ya Jiji la Gaborone,
timu hizo zilikuwa zimefungana mabao 2-2. Stars ndiyo iliyokuwa ya
kwanza kupata bao dakika ya 17 lililofungwa kwa penalti na beki Erasto
Nyoni.
Mwamuzi
Lekgotia Johannes Stars alitoa adhabu hiyo baada ya beki Oscar Obuile
Ncenga wa Zebras kumuangusha ndani ya eneo la hatari mshambuliaji
Mrisho Ngasa aliyekuwa akimkabili kipa Mompoloki Sephekolo.
Bao hilo halikudumu muda mrefu, kwani Zebras walisawazisha dakika ya 26 baada ya shuti kali lililopigwa na Lemponye
Tshireletso nje ya eneo la hatari kumshinda nahodha wa Taifa Stars,
Juma Kaseja. Dakika tano baadaye kiungo mshambuliaji Mwinyi Kazimoto
aliifungia Stars bao la pili kwa shuti la mbali.
Tshireletso
aliisawazishia tena Zebras dakika ya 37. Mfungaji alifunga bao hilo
kwa kichwa akiunganisha mpira wa krosi kutoka wingi ya kushoto
uliopigwa na Tebogo Sembowa ambaye kabla alimtoka beki Aggrey Morris.
Kipindi
cha pili kilianza kwa Kocha Kim Poulsen wa Stars kuwatoa Frank Domayo
na Salum Abubakar na nafasi zao kuchukuliwa na Shabani Nditi na Athuman
Idd. Safari hii Zebras ndiyo walioanza kufunga dakika ya 69 ambapo
kiungo Michael Mogaladi aliifungia bao la tatu kwa kichwa akiunganisha
krosi fupi iliyotokana na mpira wa kurusha.
Dakika
13 za mwisho Stars walicheza pungufu baada ya beki Erasto Nyoni
kutolewa nje kwa kadi nyekundu kutokana na kumchezea rafu mshambuliaji
Lovemore Murirwa.
Mrisho
Ngasa ambaye alikuwa nyota kwenye mchezo huo aliisawazishia Stars
dakika ya 84 baada ya kugongeana one-two na mshambuliaji Simon Msuva
aliyetokea benchi kuchukua nafasi ya Haruna Moshi.
"Licha
ya timu kucheza vizuri, tatizo kubwa lilikuwa kwenye safu ya ulinzi
ambapo mabeki waliruhusu mipira mingi ya krosi na kuwaacha
washambuliaji wa Botswana wakifunga bila bughudha. Mabeki hawatakiwi
kuruhusu mipira ya krosi, wakiruhusu ni lazima wahakikishe wanawadhibiti
washambuliaji wa timu pinzani.
"Kwa
upande wa washambuliaji, Said Bahanuzi alikuwa akicheza mechi yake ya
kwanza ya kimataifa akiwa na Stars tangu nilipomjumuisha kwenye timu
kwa mara ya kwanza. Kuna makosa madogo madogo ambayo niliyatarajia,
hivyo nitamrekebisha polepole," alisema Kocha Poulsen mara baada ya
mechi hiyo.
Stars;
Juma Kaseja, Erasto Nyoni, Amir Maftah, Aggrey Morris, Kelvin Yondani,
Frank Domayo/Shabani Nditi,Mrisho Ngasa, Salum Abubakar/Athuman Idd,
Said Bahanuzi/Simon Msuva, Haruna Moshi/Ramadhan Singano na Mwinyi
Kazimoto.
Zebras;
Mompoloki Sephekolo, Tshepo Motlhabankwe/Tshepo Maikano, Edwin
Olerile, Oscar Obuile Ncenganye, Mompati Thuma, Patrick Motsepe/Jackie
Mothatego, Lemponye Tshireletso, Michael Mogaladi, Tebogo Sembowa,
Ntesang Simanyana na Galabgwe Moyana/Lovemore Murirwa.
Stars
inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager inarejea nyumbani kesho
(Agosti 16 mwaka huu) ambapo itawasili Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa
Julius Nyerere (JNIA) saa 1.20 usiku kwa ndege ya Kenya Airways.
No comments:
Post a Comment