Elly Kalekwa
MABINGWA wa zamani wa Kenya, Sofapaka wanataka kocha mpya na wametoa sharti awe wa kigeni- hapana shaka hii ni fursa nzuri kwa makocha wa Tanzania wenye kujiamini kuomba kazi.
Rais wa klabu, Elly Kalekwa amesema wanasaka kocha mwenye rekodi nzuri, mwenye nidhamu na morali ya kazi.
“David Ouma ni kocha wa muda kwa sasa. Tumepokea maombi kutoka kwa makocha wengi, lakini nataka ifahamike, hii ni kwa makocha wa kigeni tu.”
“Tunatafuta mtaalamu mwenye nidhamu, ambaye ana rekozi ya matokeo mazuri katika timu alizofundisha awali. Kila kitu ni yeye tu na ninachotaka ni mtu ambaye ataipa timu matokeo mazuri, kuleta mataji”alisema.
Sofapaka imetolewa kwenye michuano ya Top 8, lakini bado ina nafasi ya kushinda mataji mawili, Ligi Kuu ya Kenya na Kombe la FKF.
Kalekwa amesema anayetaka kazi awasiliane na ofisi yake.
“Wanatakiwa kutuma maombi yao katika ofisi za Sofapaka au baruapepe info@sofapaka.com.”
Kwa sasa klabu hiyo, anayaochezea beki Mtanzania, Idrisa Rajab inashika nafasi ya pili katika Ligi Kuu, ikiwa na poitni 38, ikizidiwa pointi sita na vinara wa ligi hiyo, AFC Leopards na Jumamosi watamenyana na Chemelil Sugar Uwanja wa Nyayo.
Tanzania kuna makocha wazuri na wenye rekodi nzuri kama Abdallah Kibadeni, aliyeifikisha Simba fainali ya Kombe la CAF mwaka 1993, Charles Boniface Mkwasa aliyeiwezesha timu ya taifa ya wanawake ya Tanzania kucheza Fainali za Mataifa ya Afrika mara mbili.
Kwa sasa Kibadeni yupo Kagera Sugar na Mkwasa Ruvu Shooting na bado kuna makocha wengine vijana wanaoinukia vizuri kama Suleiman Matola, ambaye kwa sasa anafundisha Simba B.
No comments:
Post a Comment