Friday, August 3, 2012

MKUTANO MKUU WA WANACHA WA TIMU YA SIMBA KUFANYIKA AGOSTI 5

MKUTANO MKUU
MKUTANO Mkuu wa Wanachama Wote wa Simba utafanyika Agosti tano mwaka huu katika Bwalo la Maofisa wa Polisi Oysterbay kama ilivyopangwa.
Mipango yote kwa ajili ya mkutano huo muhimu kikatiba imekamilika na klabu inawaomba wanachama wake wote hai kuhudhuria mkutano huo muhimu.
Uongozi umepanga kutoa mabasi kwa ajili ya kuwasafirisha wanachama wake kutoka katika maeneo mbalimbali kwenda katika ukumbi wa mikutano.
Kutakuwa na mabasi matatu kwenye eneo la Shibam Magomeni... Mabasi matatu Temeke mwisho na mabasi matatu katika makao makuu ya Simba SC Mtaa wa Msimbazi.
Pia klabu itapeleka mabasi mawili katika wilaya za Mkuranga na Kibaha kwa ajili ya kuwaleta wanachama wake walio katika mkoa wa Pwani kuhudhuria mkutano huo.
Mwenyekiti wa Simba, Mhe; Ismail Aden Rage, amewahakikishia wanachama wa Simba kwamba mkutano huo utaendeshwa kisasa na usalama umehakikishwa kwa asilimia 100 kwa vile eneo la mkutano liko chini ya Jeshi la Polisi.
"Napenda kuwahakikishia wanachama wote wa Simba kwamba mkutano huo utakuwa bora na wote watakaokuja watafurahi na kujisikia fahari kuwa washabiki wa klabu ya soka ya Simba. Kwa wale ambao wamepanga kuja kufanya vurugu kwenye mkutano huo, klabu itaviachia vyombo vya dola vifanye kazi yake," alisema.
NGASSA
MCHEZAJI mpya wa Simba, Mrisho Ngassa, leo amekabidhiwa jezi namba 16 atakayokuwa akiitumia kwenye klabu yake msimu huu.
Ngassa alikabidhiwa jezi yake hiyo katika makao makuu ya Simba Mtaa wa Msimbazi jijini Dar es Salaam na Makamu Mwenyekiti wa Simba, Geofrey Nyange Kaburu.
Kaburu alisema Simba inamkaribisha Ngassa kwa moyo mmoja na kwamba wapenzi wote wa Wekundu wa Msimbazi wana imani kubwa naye kwani uwezo wake mkubwa wa soka unafahamika ndani na nje ya nchi.
"Tunashukuru kwamba tumekidhi vigezo vyote vilivyohitajika kwa ajili ya usajili wa mchezaji huyu. Tumeingia naye mkataba wa mwaka mmoja baada ya kumaliza muda wa mkopo wake kutoka Azam na ni imani yetu kwamba ujio wa Ngasa utaimarisha zaidi timu kwani yeye ni miongoni mwa wachezaji ambao Kocha Mkuu wa Simba, Milovan Cirkovic, anawapenda," alisema.
Akizungumza katika tukio hilo, Ngassa alisema amefurahi kusajiliwa na Simba kwani ni sawa na historia kujirudia, akikumbusha kwamba baba yake mzazi, Khalfan Ngassa, aliwahi kuwa mchezaji wa klabu katika miaka ya 1990.
Kabla ya mkutano huo na waandishi wa habari, Ngassa alifanya mazoezi na wachezaji wenzake wa Simba katika ufukwe wa Coco, jijini Dar es Salaam ambako Simba inaendelea na mazoezi yake chini ya makocha Amatre Richard na James Kisaka.
Imetolewa na
Ezekiel Kamwaga
Ofisa Habari

Simba SC

No comments:

Post a Comment

POSTED TITLE

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...