Monday, February 1, 2016

YONDANI KUIKOSA MECHI YA SIMBA VS YANGA!

Beki wa kati wa Yanga, Kelvin Yondani.

HASIRA hasara, hivyo ndivyo unavyoweza kusema baada ya beki wa kati wa Yanga, Kelvin Yondani kukumbwa balaa ambalo litakuwa ni pigo kubwa kwa timu yake.

Yondani ataikosa mechi ya Ligi Kuu Bara dhidi ya Simba ambayo itapigwa Februari 20 mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam baada ya kadi nyekundu ya moja kwa moja aliyoipata juzi Jumamosi kwenye Uwanja wa Mkwawani jijini Tanga.Yondani alikumbwa na balaa hilo baada ya kumtandika konde Daktari wa Coastal Union, Kitambi Mganga katika mchezo uliozikutanisha timu hizo na Yanga ikachezea kichapo cha mabao 2-0.
Tukio hilo lilitokea dakika za majeruhi za mchezo huo baada ya Maganga kuingia uwanjani kwa ajili ya kumtibu kipa wa Coastal Union, Fikirini Bakari aliyekuwa ameumia.


Wakati akiendelea kutoa huduma hiyo, Yondani alionekana akizungumza na Manganga akimtaka kumhudumia kipa hiyo haraka ili atoke nje mechi iweze kuendelea.
Hata hivyo, Maganga naye alionekana kumjibu kitu Yondani na ghafla beki huyo wa kutumainiwa wa Yanga, alionekana akimrushia konde.
Kitendo hicho kilimkera vilivyo daktari huyo na kujikuta akitaka kujibu mashambulizi hali iliyomfanya mwamuzi wa mechi hiyo aingilie kati na kumtoa nje ya uwanja, kisha akamgeukia Yondani na kumzawadia kadi nyekundu.


Kutokana na hali hiyo kwa mujibu wa kanuni ya 25 ya Ligi Kuu Bara inayozungumzia udhibiti wa wachezaji, kifungu cha kwanza kipingele (C), “Mchezaji atakayetolewa nje kwa kadi nyekundu kwa kosa la kupiga/kupigana atasimamishwa kushiriki michezo mitatu (3) inayofuata ya klabu yake na atalipa faini ya shilingi laki tano (500,000) za Kitanzania.”
Hali hiyo itamfanya Yondani azikose mechi tatu zijazo za klabu hiyo ambazo ni dhidi ya Prisons, JKT Ruvu na ile ya Simba. Hata hivyo, kabla ya mchezo huo dhidi ya Simba, Yanga ilitakiwa icheze na Mtibwa Sugar lakini mechi hiyo haitakuwepo, itapangwa baadaye ambapo Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Ligi, Boniface Wambura alipoulizwa itachezwa lini, alijibu kwa ufupi: “Itapangwa.”
Katika hatua nyinge dhabu hiyo ambayo atakumbana nayo Yondani ni tofauti na ile ya Maganga.
Mwenyekiti wa Chama Cha Waamuzi Tanzania (Frat), Nassor Mwalimu, alisema: “Kama ripoti ya mwamuzi itaonyesha kuwa wawili hao walipigana uwanjani, basi daktari huyo wa Coastal Union yeye ataendelea kuitumikia klabu hiyo kama kawaida katika mechi zitakazofuatia ila atapigwa faini.”
Hata hivyo uongozi wa Yanga kupitia kwa mkuu wake wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano, Jerry Muro, ulipoulizwa kuhusiana na tukio hilo, ulisema: “Kwa sasa suala hilo hatuwezi kulizungumzia kwa kuwa bado hatujui ripoti ya mwamuzi inasemaje, tutakuwa tayari kulizungumzia pindi tutakapokuwa tumeipata ripoti hiyo.”


Majibu hayo ya Muro hayakuwa na tofauti kubwa na yale ya Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Baraka Kizuguto ambaye alisema: “Suala hilo bado halijatufikia, hivyo hatuwezi kulizungumzia kwa sasa.”
Hata hivyo kwa upande wa Simba, kaimu kocha mkuu wa timu hiyo, Jackson Mayanja alisema: “Hatupaswi kufurahi kuwa Yondani hatakuwepo katika mechi hiyo kwa sababu Yanga haina mchezaji mmoja, tunachopaswa ni kujipanga kwa ajili ya kuhakikisha tunafanya vizuri katika mechi zetu zote.”

POSTED TITLE

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...