Friday, January 22, 2016

NIYONZIMA AREJEA YANGA AANZA MAZOEZI RASMI LEO, YANGA HII....!


Wachezaji wa Yanga wakifanya mazoezi ya kukimbia mapema leo katika uwanja wa Karume jijini Dar es Salaam.
Yanga tayari leo imeanza kufanya mazoezi na kiungo wa timu hiyo Haruna Niyonzima baada ya kurejea kwenye kikosi hicho, ambapo alifungiwa na klabu hiyo takribani mwezi mmoja baada ya kupishana kauli na mabosi wake hao.

MZUNGUKO wa kwanza wa Ligi Kuu Bara msimu wa 2015/2016 ulikamilika jana, Alhamis kwa kuchezwa mechi tatu, lakini mabingwa watetezi wa ligi hiyo, Yanga ndiyo wamemaliza mzunguko wakiwa kileleni baada ya kuitandika Majimaji mabao 5-0.

Yanga imepata ushindi huo mnono kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam na kurejea kileleni kwa kuwa na pointi 39 sawa na Azam, lakini inaongoza kwa tofauti nzuri ya mabao ya kufunga na kufungwa.
Utamu wa ushindi wa jana na kurejea kileleni haukuwa kwenye pointi tatu tu bali kuna mengi mazuri yaliyojitokeza ambayo ni burudani nzuri kwa Wanajangwani kama ifuatavyo:
MAJIMAJI NDEMBENDEMBE
Licha ya kuanza mchezo kwa kasi ndogo, Yanga ilipata bao la mapema kupitia kwa kiungo wake mchezeshaji, Thaban Kamusoko dakika ya nne, ambaye alifunga kiufundi kwa shuti la mbali baada ya kupata pasi kutoka kwa Deus Kaseke.

Kipindi cha pili ndiyo kilikuwa kizuri kwa Yanga kwa kuwa waliongeza kasi na kufanikiwa kupata bao la pili dakika ya 47 mfungaji akiwa ni Amiss Tambwe, la tatu likafuata mfungaji akiwa ni Donald Ngoma dakika ya 57 kisha Tambwe tena akatupia la nne dakika ya 72 na kuongeza la tano dakika ya 85.
VIJANA WAMEIVA
Yanga ikiongozwa na nahodha wake, Kelvin Yondan, ilionekana kuelewana zaidi kipindi cha pili, huku ushirikiano wa Tambwe, Kamusoko, Kaseke na Ngoma ukionekana kuwa kivutio kwa jinsi walivyokuwa wakipigiana pasi zenye macho.

TAMBWE NI MASHINE YA MABAO
Tambwe ambaye alitua Yanga akitokea Simba ambako alionekana ameisha kiuwezo, ameendelea kuthibitisha kuwa yeye ni noma linapokuja suala la kutupia mabao, kwani amefikisha mabao 13 msimu huu, hivyo kuwa kinara katika ufungaji mabao akimzidi Elius Maguri wa Stand United mwenye mabao 10.

Tambwe ambaye imekuwa ni kawaida yake kutupia hat trick, pia amemzidi Hamis Kiiza wa Simba ambaye naye pia ana mabao 10, huku Ngoma akifikisha mabao 9.
Tambwe na Ngoma wamethibitisha kuwa wao ndiyo wenye makali zaidi katika ligi kuu kwa kuwa wamefikisha jumla ya mabao 22, idadi ambayo haijafikiwa na timu 13 katika ligi hiyo.

Stand wamefunga mabao 17, Mtibwa (17), Prisons (16), Mwadui FC (18), Toto (12), Mgambo (13), Mbeya City (13), Ndanda (17), JKT Ruvu (16), Majimaji FC (9), Coastal (8), Kagera (5), African Sports (4). Simba imefunga mabao 23, Azam mabao 30 huku Yanga jumla ikiwa na mabao 36.

No comments:

Post a Comment

POSTED TITLE

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...