Saturday, May 30, 2015

WANATUPIA PAMBA F’LANI AMAZING

Msanii wa Bongo Fleva, Juma Musa 'Jux'.
Lucy Mgina,Dar es Salaam
UTANASHATI ni jambo kubwa sana kwa wasanii na watu wa kawaida. Mara nyingi utanashati humtambulisha muhusika namna anavyojiweka kuanzia nyumbani hadi katika mwili wake.Hapa Tanzania kuna wasanii kibao ambao wamekuwa wakijitahidi kujiweka fresh kwa uvaaji wao na hilo limewafanya kujiongezea umaarufu zaidi na sifa kujaa kwao.

Msanii wa Bongo Fleva, Gerry wa Rhymes.
Mara nyingi imekuwa ikichukuliwa kuwa watu wenye mkwanja ndiyo wanatakiwa kupendeza, lakini siyo hivyo! Unaweza kuwa na fedha nyingi na ukanunua kila aina ya nguo unayotaka lakini kitu kidogo tu kikakuangusha ambacho ni kushindwa kupangilia rangi ya nguo au kutojua uvae nini kwa wakati gani.
Wasanii wengi wa Bongo Fleva ambao leo ndiyo nawazungumzia wamekuwa wakijitahidi kujiweka sawa, na hii ni kutokana na kuwa na mizunguko mingi ya ndani na nje ya nchi hasa katika shoo, hivyo hupata fursa zaidi za kujifunza huko.
Sasa wafuatao ni baadhi ya mastaa wa Bongo Fleva ambao wanajua kupangilia mavazi yao na kufanya waonekane ng’aring’ari muda wote wanapokuwa mbele ya jamii.

Jux
Juma Mussa maarufu kama Jux, ndiye msanii anayeongoza kwenye utupiaji wa nguo zenye brand kali za aina mbalimbali na huwa zinampendeza. Wapo wengi ambao wanavaa vizuri lakini Jux amekuwa akiwavutia wengi kila anapoonekana kutokana na kutupia vyema mavazi yake.

Anafanya muziki wa R&B na amekuwa akifananishwa zaidi na msanii wa Marekani, Trey Songz katika uimbaji. Licha ya kuwa hajaoa (anatajwa kutoka na msanii Vanessa Mdee) lakini linapokuja suala la mavazi jamaa ni msafi na anajua kupangilia hiyo yote inasababishwa na yeye mwenyewe.
Kamikaze ‘Cyril’
Anafahamika zaidi kwa jina la Cyril ambapo alilazimika kulibadili na kujiita Kamikaze, ni msanii ambaye pengine katika orodha hii anaweza kuwa hafahamiki sana lakini jamaa anajua kutupia.Staa huyu mavazi yake mara nyingi anakuwa akipendelea kupiga fulana za kubana na ‘jeans’. Sasa hivi Kamikaze anayefanya muziki wa Bongo Fleva anakimbiza na Kibao cha Nikikuona.

Izzo Business.
Izzo Business
Ukimtaja kwa jina la Emmanuel Simwinga utapata tabu kumtambulisha kwa mashabiki wa Muziki wa Hip Hop lakini ukimtaja kwa jina lake la kisanaa la Izzo Business utakuwa umepatia. Jamaa pia hufahamika kama Mr Mbeya City, huyu yupo mstari wa mbele kulitangaza jina la mkoa huo ambako ndiko alikozaliwa. Mavazi yake mara nyingi huwa ni suti au ‘jeans’, fulana na sweta jepesi juu yake, hapo utamtaka.


Jamaa anajitahidi sana kwenye mpangilio wa mavazi, hata kwa wale ambao hawajafanikiwa kuonana naye ‘live’ basi ukweli wanaupata kupitia picha za mnato na video za ngoma zake mbalimbali ambazo anaonekana ‘anang’ara’. 
Mr Blue
Herry Sameer au Mr Blue kama anavyofahamika na wengi kupitia kazi yake ya muziki, alianza kuwika kitambo akiwa bado mdogo baada ya kuachia ngoma yake ya Mr Blue na kufanikiwa kuwateka watu wengi hasa wanafunzi wa kike.
Jamaa ni mzuri pia kwenye upangiliaji wake wa mavazi na amekuwa akijitahidi mara kwa mara kwenda na wakati. Kwa sasa anaishi na mchumba wake anayeitwa Wahida ambaye amezaa naye mtoto mmoja.

Msanii wa Bongo Fleva, Nasib Abdul au Diamond Platinumz.
Msanii wa Bongo Fleva aliye juu kwa sasa, Nasib Abdul au Diamond Platinumz ana jina kubwa sana ndani na nje ya Tanzania kutokana na kazi zake kukubalika vilivyo lakini pia huwa hakosei kwenye kupangalia mavazi yake kulingana na sehemu anayokwenda.
Amekuwa na mvuto mkubwa na ni ‘role model’ wa vijana wengi wa sasa katika uvaaji lakini pia usisahau anajiita Rais wa Wasafi Tanzania, kweli anafaa hata kungekuwa na cheo zaidi ya rais naamini angefanikiwa kukamata nafasi hiyo.
Hemed Suleiman ‘PhD’
Ukimtambulisha kama PhD peke yake kidogo inaweza kuleta ugumu kumfahamu bila kuweka jina Hemed, ukweli ni kwamba Hemed Suleiman maarufu kama PhD anajua kupiga pamba hasa katika ‘kumechisha’. Mtazame akiwa amevaa suti iwe nyekundu, bluu na rangi nyingine mbalimbali, yeye ni mweupe na amekuwa akipendeza akivaa nguo za aina yoyote.

Huyu ni msanii wa filamu na muziki wa Bongo Fleva ambaye alitokea kwenye shindano ya Tusker Project Fame. Inadaiwa kuwa katika maisha yake anapenda sana kula na kwa siku hujitahidi kufukia chakula mara nane na hadi kufikia saa sita usiku kila siku anakuwa amemaliza kuku wawili na nusu au watatu.
Gerry wa Rhymes
Jamaa anafahamika zaidi kwa jina la Gerry wa Rhymes, huyu alianza kufahamika zaidi baada ya kutoa Ngoma ya I Love You aliyofanya mwaka 2010 tangu hapo akaanza kujikusanyia mashabiki na sasa yupo juu.Licha ya hivyo, jamaa hayupo nyuma kwenye suala la kutupia, amekuwa akijitahidi sana kujiweka sawa katika maeneo hayo na hii imekuwa ikimuongezea sifa popote anapokwenda. Zaidi anapenda kutupia fulana ya kawaida na jeans wakati mwingine suti mara mojamoja siyo mbaya kwake.

Bob Junior
Raheem Nanji maarufu kama Bob Junior anajiita rais wa Masharobaro Tanzania, yaani wale vijana wote wanaopenda kupendeza huyu ndiyo kiongozi wao mkuu hiyo ni kwa mujibu wake yeye mwenyewe.Miongoni mwa nguo ambazo pengine anapenda kuzivaa ni fulana za kubana, jeans na koti lililotengenezwa kwa kitambaa cha ‘leza’, hapo mtoko wake unakuwa umekamilika.

No comments:

Post a Comment

POSTED TITLE

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...