Thursday, May 7, 2015

MAMISS ‘VICHWA’ WALIOGOMA KUPOTEA!


Millen Magese.
Na Hamida Hassan LICHA ya fani ya u-miss hapa nchini kughubikwa na changamoto mbalimbali ikiwemo tabia mbaya mbele ya jamii hususan kipindi cha hivi karibuni, lakini baadhi ya washindi na washiriki wa shindano hilo ambao ni vichwa wamejitahidi kusimama thabiti katika mbio za kukimbizana na mafanikio.
Wapo wachache walioajiriwa na serikali pamoja na makampuni na mashirika binafsi kutokana na ujuzi wa taaluma zao huku wengine wakijikita kwenye ujasiriamali.Hapa chini ni orodha ya baadhi ya mamiss ambao wamegoma kupotea na wanatumia elimu, ujuzi na utundu wao kufanya mambo ya kuwakwamua kimaisha pia kuisaidia jamii. Hawa ni tofauti na wale waliojikita kwenye uigizaji.
Jokate Mwegelo ‘Kidoti’.
Jokate Mwegelo ‘Kidoti’
Alishiriki shindano hilo mwaka 2006 na kuambulia nafasi ya pili. Nje ya ‘taito’ ya u-miss, mrembo huyu amekuwa ‘akifurukuta’ katika nyanja za ujasiriamali huku akiitumia alama yake ya usoni (kidoti) kama fursa kwani amekuwa akianzisha na kutengeneza ‘projekti’ mbalimbali kupitia nembo hiyo.

Amekuwa akifanya ujasiriamali akihusisha shughuli za urembo pamoja na kubuni mitindo ya mavazi chini ya nembo ya Kidoti. Anamiliki Kampuni ya Kidoti inayojumuisha maduka ya urembo ikiwemo nywele za Kidoti, mavazi, viatu, nguo na  malapa. 
Hoyce Temu.
Hoyce Temu
ALINYAKUA Taji la U-miss Tanzania mnamo mwaka 1999. Tangu hapo amekuwa akijihusisha na mambo ya ujasiriamali ikiwemo uandishi wa vitabu ambapo alitoa kitabu chake cha kwanza alichokipa jina la Nakumbuka Yote ambacho kilimwingizia kipato kikubwa kutokana na historia yake kwa jamii.


Mbali na hapo, amekuwa akiwasaidia watu wenye matatizo katika jamii kwa kuendesha Kipindi cha Mimi na Tanzania kinachorushwa na Runinga ya Channel Ten ambacho kimekuwa kikiendesha harambee kwa lengo la kupata misaada kutoka kwa wasamaria wema wanaoguswa.
Millen Magese
HUYU anashughulika na mambo ya mitindo chini ya ‘lebo’ yake ya Magesse Foundation. Ni mshindi wa taji hilo mwaka 2001. Mrembo huyu amekuwa msaada mkubwa kwa jamii kwani anawasaidia wasichana na akina mama wenye matatizo ya uzazi. Pia amekuwa akitoa michango katika elimu ikiwemo madawati na vifaa mbalimbali huku akitarajia kujenga shule mkoani Mtwara.

Faraja Kotta
LICHA ya kushikilia taji la shindano hilo mwaka 2004, huyu kwa sasa ni mke wa Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Lazaro Nyalandu. Mrembo huyu anatajwa kuwa ni msimamizi wa Kipindi cha Njia Panda (Programme Officer) kinachorushwa kupitia Kituo cha Redio cha Clouds FM.

Mbali na hapo, Kotta amekuwa akijihusisha na uandishi wa vitabu na tayari ameshaandika kitabu cha Unaweza kinachotumiwa na wanafunzi wa shule mbalimbali.
Nargis Mohamed.
Nargis Mohamed
KUTOKANA na taaluma yake, ameajiriwa na benki ya Cooperative Rural Development Bank (CRDB). Alishiriki shindano hilo mwaka 2003 na kushika nafasi ya tatu. Mbali na kuajiriwa katika benki hiyo, Nargis amekuwa akijishughulisha na ujasiriamali kwa kumiliki maduka ya urembo na mavazi ya kike na kupamba maharusi ya Fashionista na Habibity.

Nasreen Karim
‘HILI ni zao’ la Mwanza. Alinyakua ushindi wa taji mwaka 2008. Amejikita katika ujasiriamali wa kuuza urembo wa wanawake wa kabila la Kimasai linalojihusisha na hereni na cheni zinazotengenezwa na wanawake wa kabila hilo. Lengo la kuanzisha duka hilo liitwalo Enjipai  ni kuitangaza jamii ya K-imasai kimataifa.

Nancy Abraham Sumari
ALILITANGAZA Taifa letu kimataifa zaidi mwaka 2005 katika kiwango cha Dunia.  Amekuwa akijihusisha na uandishi wa vitabu ambapo ameandika kitabu kwa ajili ya watoto kinachoitwa Nyota Yako na kukisambaza bure katika shule mbalimbali.

POSTED TITLE

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...