Sunday, March 30, 2014

WANAFUNZI WA CHUO KIKUU CHA UDOM WAAHIDI KUJIUNGA NA PPFMeneja Uhusiano na Masoko wa Mfuko wa Pensheni wa PPF, Lulu Mengele, akitoa mada kuhusiana na huduma mbalimbali zitolewazo na Mfuko huo kwenye semina iliyoandaliwa na Mfuko huo kwa wanafunzi wa mwaka wa mwisho Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), ambapo zaidi ya wanafunzi 500 walihudhuria
Baadhi ya wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), wakifuatilia mada kutoka kwa Meneja Uhusiano na Masoko wa Mfuko wa Pensheni wa PPF, Lulu Mengele.


Meneja wa Kanda ya Mashariki na Kati wa Mfuko wa Pensheni wa PPF, John Mwalisu, akitoa mada kwenye semina ya siku mbili, iliyoandaliwa na Mfuko huo kwa wanafunzi wa Chuo kikuu cha Dodoma (UDOM).


Baadhi ya wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), wakifuatilia mada.
WANAFUNZI wa mwaka wa mwisho wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), wameridhishwa na mada mbalimbali zilizotolewa na Mfuko wa Pensheni wa PPF, na wameahidi kujiunga kwa wingi na Mfuko huo, kwani wengi wao wanatarajia kujiajiri, hivyo itakuwa fursa nzuri kwao kuandaa maisha yao ya baadaye watakapostafu.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti chuoni hapo jana mara baada ya semina iliyoandaliwa na PPF kwa wahitimu wa elimu ya juu, walisema awali walidhani kwamba Mfuko wa Pensheni wa PPF ni kwa ajili ya wafanyakazi walioajiriwa tu, lakini sasa wamefahamu kuwa milango iko wazi hata kwa wale ambao wamejiari ili mradi tu wawe na umri wa kuanzia 18.

Mmoja wa wanafunzi hao, Oneck Mwalongo, alisema kwa muda wote ambao amekuwa chuoni alikuwa hajawahi kuona maofisa wa mifuko inayojihusisha na masuala ya hifadhi ya jamii wakifika kwa ajili ya kuwapa semina kuhusiana na fursa zinazotolewa, lakini PPF imekuwa ya kwanza kuwapa elimu hiyo.

"Lakini leo hii tunashukuru PPF wametufumbua macho kwani tulikuwa tunajua ili uwe mwanachama ni lazima uwe umeajiriwa, kwangu mimi nitajiunga na PPF kwa sababu kozi yangu ya sayansi ya kompyuta si lazima niajiriwe nitajiajiri mwenyewe," alisema Mwalongo.

Alisema mfumo wa uwekaji amana wa hiari ulioanzishwa na PPF utasaidia vijana wengi watakaokuwa wamejiajiri kujiwekea akiba.

Pia alisema amefurahishwa na mpango wa baadaye wa PPF wa kuanza kukopesha wanachama wake viwanja, kwani nyumba ndiyo jambo muhimu kwa maisha ya binadamu.
Mwalongo, alisema wakati akiingia kwenye semina hiyo alikuwa hafahamu kama maisha ya kesho huanza kuandaliwa leo, hivyo atakapoondoka chuoni hapo ataanza kujiwekea akiba ili asikumbane na msemo wa fainali uzeeni.

"Nilikuwa sifahamu kama maisha ya kesho yanaandaliwa leo wamenionesha njia sasa naanza kuandaa maisha ya uzeeni," alisema.

Kwa upande wake, Elizaberth Elibarick, alisema PPF ni mfuko wa kujiunga nao hasa kwa kuzingatia mfuko huo una mfumo wa uwekaji amana wa hiari na unatoa fao la elimu kwa watoto wa mwanachama anapofariki akiwa bado kazini.

Alisema si jambo la mchezo Mfuko kumsomesha mtoto au watoto wa wanachama ambao wamefariki kuanzia darasa la awali hadi kidato cha sita na kizuri zaidi wanalipa mafao kwa wakati.

Naye Leonard Mgeja, alisema kupitia semina hiyo yeye na wanafunzi wenzake wameweza kufahamu vitu vya msingi ambavyo walikuwa hawafahamu kuhusiana na Mfuko wa PPF.

"Leo tumefahamu umuhimu wa maandalizi ya maisha ya baadaye tukiwa na umri mdogo ili kufanya mambo sahihi kabla ya kufikia uzeeni," alisema na kuongeza kwamba;

"Hivi sasa ambapo tunakaribia kwenda makazini tunaenda na mwanzo mzuri kwani hatutegemei kuajiriwa tu, bali na kujiajiri hivyo tutajiunga na uchangiaji wa hiari kama hatutakuwa kwenye mfumo rasmi wa ajira."

Awali Meneja Uhusiano na Masoko wa Mfuko huo, Lulu Mengele, aliwaasa wanafunzi hao wa mwaka wa mwisho zaidi ya 500 waliohudhuria semina hiyo, kujiunga na PPF kupitia Mfumo wa asili wa Pensheni au ule wa uwekezaji amana pale ambapo wataamua kujiajiri wenyewe.

“Mfumo wa uwekezaji amana, unaandikisha watu kutoka sekta isiyo rasmi, kama wakulima, wafugaji, machinga na mama lishe”. Alifafanua.

Katika mada ya uwekezaji amana, Lulu alisisitiza umuhimu wa kuweka akiba kwani matayarisho ya maisha ya kesho yanaanza sasa.

Kwa upande wake Meneja wa Mfuko wa Pesnheni wa PPF, Kanda ya Mashariki na Kati, inayojumuisha Mikoa ya Morogoro, Dodoma na Singida, John Mwalisu, alisema PPF imeandaa semina hiyo kwa wanafunzi wa mwaka wa mwisho wa chuo hicho kwa kuwa wao ndiyo wanaingia kwenye soko la ajira.

Alisema kutokana na wao kuwa na nguvu ya kuajiriwa au kujiajiri wameona ni vema kuwaelimisha namna nzuri ya kutunza akiba ili iwasaidie watakapokuwa fikia hatua ya kustaafu.

POSTED TITLE

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...