Tuesday, February 11, 2014

WAIRAN WAKAMATWA WAKIINGIZA MADAWA YA KULEVYA TANZANIA

WIKI iliyopita Jeshi la Polisi Kikosi Kazi cha Wanamaji Tanzania, walikamata shehena ya madawa ya kulevya ‘unga’ wenye thamani ya mabilioni ya shilingi zikiwa ndani ya meli.


Wairan wakipandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar.
Taarifa za uhakika zinadai kuwa meli hiyo ambayo ni mali ya Kampuni ya Almansoor SA ya Iran ilikamatwa Jumanne iliyopita katikati ya bandari za Zanzibar na Dar es Salaam.
Meli hiyo ilikamatwa baada ya askari waliokuwa doria kuilitilia shaka na kufuatilia kwa karibu ili kujua ilikuwa imebeba nini.
Vyanzo vilivyokuwa katika eneo la tukio vinasema kuwa meli hiyo ilikuwa na watu 12 na baada ya kupekuliwa ndipo walikuta kilo 201 za madawa ya kulevya aina ya heroine.


Wairan wakiwa kizimbani.
Watu waliokamatwa katika meli hiyo ni Mohamed Hassan (30), Abdul Nabii (30), Fahiz Muhamad (34) na Rahi Baksh (30), wote raia wa Pakistani.
Wengine ni Abdulsamad Badreuse (47), Hazra Azat (60),
Nahimu Musa (25), Khalid Ally (35), Kher Murad (38), Said Mohamed (34), Murad Gwaharam (38) na Ayub Hot (50) ambaye ni nahodha wa meli, wote raia wa Iran.
Meli hiyo ilikuwa na mtazamo wa kivuvi na lengo la wahusika ilikuwa wasishtukiwe kirahisi.
“Ilikuwa si rahisi kuigundua kama uwezo wako wa kufikiri ni mdogo lakini askari wetu wana akili sana na ndiyo maana meli ile ilihisiwa mara moja,” alisema mtoa habari mmoja kutoka jeshi la polisi.
Naye Kamanda wa Kikosi cha Wanamaji Tanzania, ACP Mboje Kanga alisema ilikuwa ni kazi kubwa kuibaini meli hiyo ilikuwa imebeba nini lakini kwa kutumia mbinu za kiintelijensia waliweza kuitilia shaka na kuipeleka bandari ya Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa uchunguzi wa Uwazi, unga huo ulikuwa utue katika maeneo ya Ilala jijini Dar ambapo baadaye ungesambazwa kila kona ya nchi ya Tanzania.
“Ndugu waandishi, Ilala kuna maeneo ambayo ni maarufu sana kwa biashara kama hiyo, ule unga ulikuwa upelekwe Ilala halafu upelekwe nchi nzima,” kilisema chanzo chetu.
Kwa upande wake Kamanda wa Kikosi cha Kupambana na Kudibiti Madawa ya Kulevya Tanzania, Godfrey Nzowa akizungumza na gazeti hili kuhusu madawa hayo, alisema kama yangefanikiwa kutua Dar na kusambazwa nchini watu milioni 3 mpaka 4 wangetumia, hasa vijana.
Kamanda Nzowa alisema meli hiyo ilitiliwa shaka kutokana na kutokuwa na utambulisho wa nchi husika, yaani bendera kama meli zingine.
Akasema baada ya upekuzi waligundua zaidi ya kilo 201 za heroin zenye thamani zaidi ya shilingi bilioni 9.
“Mpaka sasa upelelezi unaendelea ili kubaini mwenyeji wao ambaye angewapokea Dar es Salaam ni nani maana kwa vyovyote yupo, tukimbaini amekwisha,” alisema Nzowa.

No comments:

Post a Comment

POSTED TITLE

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...