Tuesday, February 4, 2014

LOWASSA TISHIO CCM

Waziri Mkuu aliyejiuzulu, Edward Ngoyai Lowassa.
Stori: Jelard Lucas na Makongoro Oging’
PATASHIKA nguo kuchanika ni kauli ya kibabe inayoweza kutumika kuelezea sakata la siasa za makundi ndani ya Chama cha Mapinduzi (CCM)  linaloshika kasi huku baadhi ya wanachama wakitupiana lawama kwa kuunga mkono upande fulani kuelekea mbio za urais hapo mwakani.Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili umebaini kuwa, waziri mkuu aliyejiuzulu, Edward Ngoyai Lowassa hajawahi kutoa tamko lolote juu ya kugombea urais mwakani lakini shutuma kwamba anautaka zimekuwa zikiibuka kila kukicha.
Hali hiyo inatafsiriwa na wengi kuwa, Lowassa ni tishio kwani wote waliowahi kumshambulia wanaambulia kutokwa jasho huku wakijibiwa hoja zao na watu wengine.
Hivi karibuni Katibu wa Chipukizi na Uhamasishaji wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM), Paul Makonda aliibuka na kudai Lowassa anakivuruga chama kwa kuanza mbio za urais kabla ya muda wake.
Naye Waziri Mkuu Mstaafu, John Malecela aliunga mkono hoja ya Makonda na kumtupia lawama mwanachama mwenzake huyo kwamba amechapisha fulana zilizoandikwa ‘Friends of Lowassa’ (marafiki wa Lowassa), akadai hazina nia nzuri ndani ya chama hicho.
Hata hivyo, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Shinyanga, Khamis Mgeja, Jumamosi iliyopita aliwaambia waandishi wa habari jijini Dar kuwa, Makonda na mzee Malecela wawaombe radhi viongozi wa dini kwa kudai kwamba wanapokea mamilioni ya fedha kutoka kwa kiongozi huyo ambaye ni Mbunge wa Monduli.
 
Waziri Mkuu Mstaafu, John Malecela.
Mgeja alisema anashangaa kuona panya akimfukuza paka huku taarifa hizo zikimpa uzito Lowassa ambaye licha ya kwamba hajawahi kutoa tamko la kugombea urais mwaka 2015 lakini jina lake liko vinywani mwa wanasiasa kila kukicha.
Naye Makamu Mwenyekiti wa CCM (Bara), Philip Mangula wiki iliyopita alisema anafurahishwa kuona wanachama wake wakionesha ukomavu wa demokrasia ndani ya chama huku akiwataka wazingatie taratibu, kanuni na misingi waliyojiwekea.
Makamu Mwenyekiti wa CCM (Bara), Philip Mangula.
“Tunafurahi kuona wanachama wetu wakionesha ukomavu wa demokrasia ndani ya chama lakini tuzingatie misingi, kanuni  na taratibu tulizojiwekea kulinda chama chetu,” alisema Mangula.

POSTED TITLE

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...