Friday, January 31, 2014

ZITTO KABWE ADAIWA KUWAJIBU CHADEMA MIKOA 4


Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe.

USHINDANI wa kisiasa kati ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) umefikia hatua mpya baada ya CCM kuibuka na mkakati wa kumtumia Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe, kupambana na CHADEMA waziwazi.

Katika mkakati huo CCM imepanga kukodisha helikopta ya kumpeleka Zitto katika mikoa minne kwa gharama ya sh milioni 50 mara tu baada ya CHADEMA kuhitimisha Operesheni yao ya M4C Pamoja Daima.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka vyanzo vilivyo karibu na Zitto na CCM, yeye na chama hicho sasa wana adui mmoja – CHADEMA; na wameamua kujibu mapigo baada ya kuridhika kwamba kwa vyovyote Zitto amekwisha kupoteza uanachama wake katika CHADEMA.

Nia yao ni kumtumia Zitto kuleta mpasuko katika CHADEMA, na kufunika mjadala wa mgogoro wa CCM, kero za wananchi na mchakato wa Katiba mpya.

Zitto ambaye alivuliwa nyadhifa zake zote ndani ya CHADEMA – Naibu Katibu Mkuu Bara, Mjumbe wa Kamati Kuu, Mjumbe wa Baraza Kuu na Naibu Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni – anatarajia kutumia helikopta yenye uwezo wa kubeba watu wanne, ambayo inadaiwa kukodishwa na wapinzani wa CHADEMA.

Kwa mujibu wa habari hizo, lengo la ziara ya Zitto ni kujibu mapigo ya CHADEMA, hasa katika maeneo ambayo baadhi ya makada na viongozi wa chama hicho wamepita na kuzungumzia hatima yake kisiasa, hasa walipojibu maswali ya wananchi kuhusu sakata lake kuvuliwa uongozi kwa tuhuma za usaliti, na hatimaye Zitto kwenda mahakamani kuzuia chama kujadili uanachama wake.
Katika kesi ya msingi, Zitto aliyewahi kuwa maarufu akiwa kiongozi wa CHADEMA, anaomba arudishiwe nyadhifa zake zote, na apatiwe nakala za uamuzi wa Kamati Kuu (CC) ili aweze kukata rufaa Baraza Kuu.

Taarifa zinasema tayari chama kimempatia nyaraka hizo, lakini kwa mujibu wa Katiba ya CHADEMA, Zitto amekwisha kujiondoa kwenye chama hicho kwa kupeleka shauri mahakamani.

Taarifa za Zitto kuanza ziara mikoani zilianza kusikika mwishoni mwa wiki iliyopita.

Mikoa iliyotajwa ni Kilimanjaro, Arusha, Tanga, Morogoro na Dar es Salaam, ingawa maandalizi yanaendelea na kuna uwezekano wa kubadili baadhi ya mikoa kulingana na mkakati wao.

Kwa hadhi yake ya sasa, CHADEMA imeshasema haitahusika na mikutano yake, na wanachama wake hawatajihusisha nayo. Uratibu wa mikutano yake unafanywa na viongozi waandamizi wa CCM.

Baadhi yao walizungumza na gazeti hili kwa kujitapa kwamba hii ndiyo njia ya kuimaliza CHADEMA, lakini hawakutaka kutajwa majina gazetini.

Iwapo Zitto atakubali ufadhili huo wa CCM na kuendelea na mikutano yake, ni wazi atakuwa amekamilisha ushahidi wa kinachodaiwa na chama chake kwamba amekuwa akikisaliti kwa masilahi ya CCM.

Hata hivyo, baadhi ya viongozi wa CCM walipoombwa maelezo juu ya urafiki wao na Zitto kiasi cha kumkosanisha na chama kilichomlea kisiasa, CHADEMA, walisema kwamba urafiki uliopo si wa Zitto na CCM, bali Zitto na Rais Jakaya Kikwete.

Gazeti hili linafahamu kwamba wakati fulani mwaka juzi Zitto alipobanwa na wabunge wenzake kuhusu tabia zake za kuwasaliti kwa Rais Kikwete, alisisitiza kuwa Rais Kikwete ni rafiki yake binafsi, kwa hiyo wamwelewe.

Vilevile, wapo wanaohoji nia ya ziara hii wakati kwa muda mrefu amekuwa akikwepa kuambatana na viongozi wenzake katika ziara na operesheni nyingi za kichama.

Wanasema kwa kuwa operesheni ya sasa ya CHADEMA imepewa jina la M4C Pamoja Daima, kitendo cha CCM kuandaa ziara ya Zitto na kumkodishia helikopta, ni uthibitisho kuwa Zitto hayuko pamoja na CHADEMA tena.

Wameongeza pia kuwa kama hilo litafanyika, litakuwa limemwingiza Zitto katika orodha ya makada kadhaa wa upinzani waliotumikia CCM baada ya kufukuzwa au kunyimwa fursa za uongozi katika CHADEMA, kama Tambwe Hiza, Dk. Aman Walid Kabourou na Dk. Masumbuko Lamwai.

Alipotafutwa athibitishe kuhusu ziara hii na kama ni kweli inafadhiliwa na CCM, Zitto hakuweza kupatikana.

Mbowe kuwania tena uenyekiti

Katika hatua nyingine, Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe, amesema kuwa kamwe hatakiacha chama hicho katika uchanga wa harakati za kulikomboa taifa kama kiongozi wake wa juu.

Akihutubia katika mikutano ya Operesheni M4C Pamoja Daima katika sehemu mbalimbali mkoani Morogoro jana, mwenyekiti huyo alisisitiza kuwa, bado atagombea nafasi ya uenyekiti kwa lengo la kuendeleza harakati za ukombozi wa pili wa taifa hili.

Bila kutaja jina, Mbowe alionya kuwa wenye fikra za kuachiwa chama hicho kikiwa katikati ya ukombozi huo hawatapata nafasi, kwa sababu hawana nia thabiti ya kukiendeleza, bali wana nia ya kukibomoa kwa kutumiwa na wapinzani wa CHADEMA.

“Makamanda, kumbukeni kuwa chama hiki na sisi viongozi wake tumepita katika majaribu makubwa na hata kukoswakoswa kuuawa. Mimi nimekoswakoswa kuuawa kwa bomu huko Arusha, lakini pia kuna watu wamepoteza maisha, wamefungwa jela, wengine wamekuwa vilema, halafu watu wengine wanatusaliti kwa kupewa visenti ili wakivuruge chama na wanataka tuwape chama. Huu ni uendawazimu,” alisema.

Mwenyekiti huyo alisema CCM imekuwa ikifanya jitihada za kuihujumu CHADEMA kwa mbinu mbalimbali, zikiwemo za kupandikiza migogoro, jambo ambalo limeshindwa kufanikiwa kwani Mungu ameweka mkono wake ili kisisambaratike.

“Harakati hizi tunazofanya za kuwakomboa Watanzania mjue tunahatarisha maisha yetu, tumejaribiwa kushawishiwa ndani na nje ya Bunge ili tuwe kondoo, tumekataa. CCM wamekuja na mbinu za kupandikiza migogoro wameshindwa na sasa wanaomba nife wakifikiri nikifa na CHADEMA itakufa. Nawaambia CHADEMA haifi kwa kuwa tumezalisha makamanda wengi, watakiendeleza,” aliongeza Mbowe.

Akielezea kwa mara ya kwanza kwa undani zaidi kuhusu mauaji ya Arusha, mwenyekiti huyo alisema wana ushahidi wa kutosha kwamba polisi walihusika na mauaji hayo na kuongeza kuwa waliohusika ni polisi wa kutoka mkoani Morogoro.

“Kwa mara ya kwanza niliseme hili, mauaji ya Arusha yaliyofanyika kwa kurusha bomu katika mkutano wa kampeni za CHADEMA, yalifanywa na polisi ambao walitoka mkoani Morogoro. Ndiyo maana tunaendelea kumwambia Rais Jakaya Kikwete aunde tume ya kimahakama ili kupata ukweli wa jambo hili,” alisema.

Kuhusu Katiba
Akizungumzia msimamo wa CHADEMA kuhusu muungano, Mbowe alisema chama hicho kinaunga mkono maoni yaliyokusanywa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba inayoongozwa na Jaji Joseph Warioba, ya serikali tatu.

Alisema hata tafiti mbalimbali zilizofanyika, zikiwemo za wanasheria na wachumi zinaonyesha kuwa Muungano utaimalika zaidi chini ya muundo wa serikali tatu.

“Nawaonya Wana CCM wasijaribu kuingilia mjadala wa Bunge la Katiba na kama wanataka nchi ichimbike, basi walazimishe serikali mbili,” alisema Mbowe.

“Zipo tetesi za CCM kutaka kupitisha hoja zao kwa nguvu kutokana na idadi yao ndani ya wabunge zaidi ya 600, wakiwemo 356 wa Bunge la Tanzania Bara, 84 kutoka Zanzibar na 201 kutoka makundi mbalimbali watakaokwenda kwenye bunge hilo. Wasidanganyike kwamba wanaweza kutumia wingi wao kubadilisha maoni ya Watanzania kuhusu serikali tatu,” alisisitiza Mbowe.

Halima Mdee anguruma

Naye Mbunge wa Kawe, Halima Mdee, ambaye yuko katika msafara wa mwenyekiti huyo, alisema vijana wengi wanaochipukia katika siasa kupitia chama hicho, wamelelewa na Mbowe, ambao leo wamekuwa chachu ya mabadiliko nchini.

“Ukweli ni kwamba kamanda huyu wa anga (Mbowe), ndiye ametulea vijana wengi nikiwemo mimi, tena wengine hatukuwa na ujasiri tulionao sasa, asiwadanganye mtu, hasa sisi vijana kwamba tuliingia CHADEMA na umaarufu, hawapo hao, tumelelewa na huyo kamanda,” alisisitiza huku akipigiwa makofi.

CHANZO NI TANZANIA DAIMA

No comments:

Post a Comment

POSTED TITLE

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...