Monday, January 13, 2014

THT YASAJIRI DARASA JIPYA LA MASTAA 2014


Wanafunzi wapya walioingia kwa mwaka wa 2014 kwenye nyumba ya kukuzia vipaji nchini THT,wakiwa kwenye picha ya pamoja.
 NYUMBA ya kukuza vipaji inayokwenda kwa jina la Tanzania House of Talents ‘THT’ imeanza kuandaa wasanii wapya ambapo tayari darasa kwa wanafunzi wapya limeshaanza kwa kuwapiga msasa ili wawe poa kwenye gemu la muziki wa Bongo Fleva kama ilivyofanya kwa nyota waliotokea mikononi mwa jumba hilo.

Akizungumza na mtandao huu, Mkurugenzi wa THT, Ruge Mutahaba alisema hadi sasa ameshapokea wanafunzi zaidi ya kumi na walimu wameshaanza kufundisha.

“Tumepokea vijana zaidi ya kumi na tayari darasa la mwaka 2014 limeshaanza kufundisha, kiukweli tunamshukuru Mungu vijana tuliowachukua karibu wote wana vipaji na wanaelewa kilichowaleta hapa, kama wataendelea hivi basi natumaini hadi mwisho wa mwaka huu tutapata mastaa wenye uwezo mkubwa kupita hata waliotangulia,” alisema Ruge.

“Ujue watu wengi huwa hawaelewi kama THT huwa kuna darasa jipya kila mwaka na kwamba mara nyingi imekuwa ikiingiza vijana wapya ambao huungana na wa zamani ambao wameshaanza kutoka kimuziki, vilevile huwa tuna kawaida ya mastaa waliotokea hapa kuwanoa wadogo zao kila wanapotembelea hapa maana tunalazimika kufanya hivyo ili waweze kuwaonesha namna walivyoweza kufanikiwa wao,” alisema Ruge.

Kwa upande wa msimamizi wa mazoezi na darasa hilo, Nash Designer alisema kwamba katika madarasa yote yaliyowahi kupita, wa mwaka huu wamechangamka sana maana wanaonyesha hali ya kuelewa mapema tofauti kabisa na matarajio yao.

“Vijana wangu wako poa na wanaonesha uelewa wa hali ya juu kiasi kwamba kama wataendelea kuonyesha nidhamu zaidi ya hapa basi wanaweza kutoka mapema kuliko tulivyozoea, maana kuna wachache hadi sasa tumeshabaini uwezo wao ni mkubwa kupita maelezo,” alisema Nashi.
Vijana hao wakiwa wamepozi ndani ya jengo la mazoezi ya kuimba na kucheza lililopo Kinondoni jijini Dar es Salaam.
Vijana hao wakiimba moja ya wimbo walioutunga.

No comments:

Post a Comment

POSTED TITLE

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...