Friday, January 24, 2014

MUIGIZAJI WA FILAMU ZA KIBONGO BLANDINA CHAGULA 'JOHARI', YUKO HOI KITANDANI



MASKINI! Ndiyo neno linaloweza kumtoka mtu yeyote mwenye mapenzi mema na staa wa filamu za Kibongo, Blandina Chagula ‘Johari’ ambaye kwa sasa afya yake si ya kuridhisha, Ijumaa lina kila kitu.
Johari ni mgonjwa kwa zaidi ya siku tano sasa akiwa mtu wa kwenda hospitali mara kwa mara kwa ajili ya kuendelea na matibabu.
TAARIFA ZA AWALI
Shostito wa karibu na staa huyo alipiga simu chumba cha habari cha gazeti hili, wiki iliyopita akieleza kwamba Johari ni mgonjwa na amekuwa mtu wa kupumzika ndani.

Rafiki huyo ambaye aliomba hifadhi ya jina lake alisema: “Najua mtakuwa hamna hii habari, lakini kiukweli Johari anaumwa, jana (Jumanne iliyopita) nilikwenda kwake, hali niliyomkuta nayo kwa kweli nilimhurumia, yawezekana pia ile ishu yake na Ray inamchanganya, ukimuona amepungua, siyo yule unayemjua.”
JOHARI ATAFUTWA
Katika kutaka kujiridhisha, mmoja wa wahariri wa Global Publishers, alimvutia waya Johari Jumanne iliyopita, ambapo alipokea na kuzungumza kwa shida huku sauti ikiwa chini sana.

“Siwezi kuzungumza vizuri, sauti yangu iko chini sana... nahisi kama inakauka. Naumwa sana. Nina fluu,” alisema Johari.

Baada ya mazungumzo hayo, gazeti hili lilipata uhakika kuwa ni kweli Johari ni mgonjwa lakini hakuwa ‘siriazi’ kivile, likachukulia poa.

HALI YABADILIKA
Siku mbili baadaye, chanzo chetu kilekile cha awali kilipiga tena simu na kutoa taarifa kuwa hali ya Johari ilibadilika ghafla na kwamba alifikishwa hospitalini.

Hata hivyo, alipoulizwa ni hospitali gani amelazwa, alisema hana uhakika lakini alisikia kama amepelekwa AAR ya Sinza. Simu ya Johari ilipopigwa, haikupatikana achilia mbali marafiki zake wa karibu.

MAPAPARAZI HOSPITALINI
Timu yetu ilifunga safari hadi Hospitali ya AAR (Sinza) na ile nyingine ya Posta na kujaribu kudodosa kama alifikishwa hospitalini hapo, likaambulia patupu.
STEVE NYERERE AANZA KAZI
Katika kuonyesha kuwa mwenyekiti mpya wa Klabu ya Bongo Movie Unity, Steven Mengere ‘Nyerere’ amedhamiria kuweka umoja na ushirikiano kwa wasanii walio kwenye klabu hiyo kwenye shida na raha, ndiye aliyemtoa Johari hospitalini.

Steve Nyerere aliweka picha kwenye ukurasa wake wa Instergram inayomwonesha Johari akiwa katika hali ya kuugua, huku mkononi mwake akiwa na plasta iliyoonyesha kuwa alitundikiwa drip na kuandika: “Johari haya ndiyo maisha, usijali utapona.”
MAPAPARAZI NYUMBANI KWA JOHARI
Juzi Jumatano, timu ya waandishi wetu ilifunga safari hadi nyumbani kwa Johari, Ubungo – External, Dar ili kujua hali yake.

Hatua chache kabla ya kufika nyumbani kwake, gazeti hili lilimpigia simu, lakini hakupokea badala yake alilitumia ujumbe mfupi uliosema: “Siwezi kuongea, naomba unitumie meseji, naumwa sana na fluu, naamini nitapona. Nitakutafuta.”

Ijumaa: Nipo na karibu na kwako, nakuja kukuona.
Johari: Sipo nyumbani, nipo hospitalini.
Ijumaa: Hospitali gani?
Johari: AAR.
UHAKIKA
Pamoja na majibu ya Johari, bado gazeti hili lilitaka kujiridhisha zaidi, halikuishia njiani, lilifika hadi nyumbani kwake ambapo lilipokelewa na kijana wa kiume aliyekataa kutaja jina lake lakini alijitambulisha kama mdogo wake na Johari.

Alipoulizwa kuhusu Johari, haraka alisema: “Dada anaumwa, amekwenda hospitali. Kwa nini msiwasiliane naye kwenye simu?”
POLE JOHARI
Kuugua ni sehemu ya maisha Johari. Ni mitihani ambayo binadamu wote tumeumbiwa hivyo jipe moyo, utapona. Mungu aisimamie afya yako, upone haraka – Amina.
Stori: Hamida Hassan na Gladness Mallya

No comments:

Post a Comment

POSTED TITLE

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...