Wednesday, January 15, 2014

KOCHA WA YANGA AHITAJI MPIRA WA KASI,AANZA KUKINOA KIKOSI LEO UTURUKI



Kocha Mkuu mpya wa Yanga, Hans van Der Pluijm, raia wa Uholanzi, amesema anataka soka la kasi huku kikosi chake kikicheza kwa ushirikiano katika kushambulia na kukaba.
Van Der Pluijim (64), amemueleza mmoja wa viongozi wa Yanga kwamba ana imani siku chache atakazokaa na timu nchini Uturuki, atafanya mabadiliko huku akiahidi kuwatumia Mrisho Ngassa, Emmanuel Okwi na Simon Msuva katika aina ya ushambuliaji wa kasi anaoutaka.
“Kocha kasema anapenda soka la kasi, tumemueleza kuhusu wachezaji kadhaa wenye aina hiyo, amefurahia. Unajua alitaka kujua baadhi ya mambo, mfano alitaka kujua kama tuna wachezaji wenye kasi, tumemtajia Ngassa, Okwi, Msuva na amesema pia anataka timu inayocheza kwa ushirikiano. Lakini naamini ataanza na safu ya ulinzi,” alisema kiongozi huyo.
“Ana mambo mengi anataka kufanya, lakini ametaka kwanza kuiona timu, vizuri atawaona wakicheza mechi kwa kuwa atafika kesho (leo), halafu saa chache watacheza mechi. Atapata nafasi ya kuwaona.”
Kocha huyo Mholanzi, amekuwa akisifiwa kwa soka la nguvu wakati akiifundisha Berekum Chelsea ya Ghana na alipofanya mahojiano mafupi na Championi Jumatano, alisisitiza suala la subira.
SALEHJEMBE: Unapenda soka la aina gani?
Van Der Pluijim: Kwanza ni mpira wa kasi, lazima niwe na wachezaji wenye uwezo wa kumiliki mpira na kupeleka mashambulizi kwa kasi, lakini timu yangu inacheza pamoja kama timu. Muwe na subira kidogo, lazima wachezaji wajifunze.
SALEHJEMBE: Labda ulifahamu lolote kuhusu soka la Tanzania?
Van Der Pluijim: Kwa kusikia ndiyo, ukiangalia timu zinazotoka Tanzania ndiyo maarufu zaidi kwa Afrika Mashariki, lakini sijui mambo mengi ya hapa.
SALEHJEMBE: Nini sasa unataka kufanya kwa Yanga?
Van Der Pluijim: Kikubwa ni kuwa na timu yenye uwezo wa kushinda mechi na baadaye makombe, sina hofu kwa kuwa Yanga ni timu kubwa.
SALEHJEMBE: Unajua upinzani wa Yanga na Simba ulivyo?
Van Der Pluijim: Kokote hilo halikosekani, timu kubwa haikosei kuwa na mpinzani mkubwa.
SALEHJEMBE: Umewahi kukutana na Logarusic, huyu ni kocha wa Simba. Rekodi zinaonyesha ulimshinda mabao 4-1, unafikiri itakuwa rahisi kwako kuifunga Simba mtakapokutana?
Van Der Pluijim: Ndiyo maana mwanzo nilisema subira inahitajika, Logarusic alikuwa Ashanti Gold, mimi Berekum Chelsea. Sasa yuko Simba, mimi niko Yanga. Nitalijibu vipi hilo? Maana sijawahi kuiona Simba anayoifundisha, wala Yanga ninayokwenda kuifundisha. Halafu tulikuwa Ghana, hapa ni Tanzania, hivyo lazima mambo yaende kitaalamu kwanza. Vuta subira.
Kocha huyo alilazimika kuahirisha safari ya kwenda Zanzibar, akapandishwa ndege na kwenda nchini Rwanda alikopanda ndege kwenda Antalya, Uturuki ambako Yanga imeweka kambi ya wiki mbili.
Van Der Pluijm atachukua kikosi hicho wakati Kocha Msaidizi, Charles Boniface Mkwasa atakuwa anarejea nchini kwa ajili ya sherehe maalum ya ndoa yake iliyotimiza zaidi ya miaka 20. 
CHANZO:SALEHJEMBE BLOG

No comments:

Post a Comment

POSTED TITLE

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...