Wednesday, December 18, 2013

AIRTEL YATOA SOMO KWA WANAFUNZI NAMNA YA KUTUMIA MAENDELEO YA TEKNOLOJIA


 
Wanafunzi wa shule za sekondari kote nchini wameaswa kutumia vizuri maendeleo ya teknolojia yanayotokea kwa sasa ili kuongeza kiwango cha ufaulu nchini.
Madai hayo yalitolewa na Meneja Biashara wa Kampuni ya simu za mkononi ya Airtel kanda ya ziwa Raphael Daudi wakati akikabidhi kompyuta kwa wanafunzi wa shule ya sekondari ya Kalangalala iliyopo mkoani Geita.

Meneja huyo alisema kumekuwa na wimbi la wanafunzi ambao hutumia kompyuta kwa matumizi ambayo ni kinyume na maadili na kusababisha jamii kuelekea kwenye mkondo tofauti na uliokusudiwa.

“Baadhi ya wanafunzi wamekuwa wakibatilisha matumizi ya kompyuta kwa kujifunza mambo yasiyofaa badala ya kuitumia kupanua uelewa wao wa masomo. Wanasahau kuwa kufanya hivyo maadili humomonyoka kwa kiasi kikubwa katika jamii yetu,” alisema Daudi.

Kwa upande wake Mwalimu mkuu wa shule ya sekondari Kalangala, Deusdedith Omchamba alisema mpango wa kuleta mapinduzi katika sekta ya elimu kwa kusababisha matokeo makubwa kwa wanafunzi unaofahamika kama “Big results now” utafanikiwa katika shule hiyo kwa kutumia teknolojia ya kompyuta kujifunzia.

“Teknolojia ya kompyuta ni muhimu sana kwa maendeleo ya wanafunzi kwa sasa kwani wanafunzi wanaweza kutumia kompyuta kusomea na hata kutafuta habari mbalimbali zinazoshabihiana na masomo yao,” alisisitiza Mwalimu Omchamba.


Aliongeza kwa kusema kuwa ni jukumu la wanafunzi kutambua umuhimu wa teknolojia hiyo na kuitumia vyema kwa kujiendeleza katika suala la elimu zaidi kuliko mambo mengine ambayo hayana kipaumbele kwa jamii yetu ya Tanzania.

Baadhi ya wanafunzi katika shule hiyo walielezea hisia zao na kusema kuwa wanafurahia sana kuwa na somo la kompyuta shuleni hapo na pia watajitahidi kutilia maanani ushauri uliotolewa na Meneja biashara wa Airtel kuhusu matumizi yanayofaa.


Pamoja na kutoa vitabu kwa shule za sekondari nchini Kampuni ya simu za mkononi ya Airtel Tanzania imekuwa ikisaidiana na serikali kuhakikisha kiwango cha elimu kinaimarika na kuleta mapinduzi katikla sekta hiyo kwani elimu ndio ufunguo wa maisha.

No comments:

Post a Comment

POSTED TITLE

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...