Thursday, October 24, 2013

WABUNGE WALIA NJAA KWA SPIKA WA BUNGE


Spika wa Bunge, Anne Makinda.

OFISI ya Bunge inaangalia utaratibu wa kufundisha wabunge ujasiriamali baada ya kubainika baadhi ya wanaokoma kushika wadhifa huo, kukabiliwa na hali mbaya ya ukwasi na kulazimika kuomba msaada.

Spika wa Bunge, Anne Makinda amesema maisha ya siasa kwa sasa sio kazi ya kutegemea kwa sababu hawana mkataba na wananchi; hivyo umefika wakati kuangalia jinsi ya kufundisha wabunge ujasiriamali kuondokana na adha ya ukata mara ubunge unapokoma.

Akizungumza na Spika wa Bunge la Uswisi, Maya Graf jijini Dar es Salaam jana, Spika Makinda alisema moja ya changamoto inayokabili bunge hivi sasa ni kwamba wabunge hawana pensheni baada ya ubunge kukoma. Alisema baadhi ya wabunge wamekuwa katika hali mbaya kifedha mara wamalizapo kipindi chao cha ubunge.

“Kwa kweli hali ni mbaya, ni wakati sasa umefika tutaanzisha programu ya kuwafundisha ujasiriamali wabunge, ili wawe na kitu cha ziada cha kufanya, ili hata kama hatachaguliwa kwenye awamu nyingine, asiwe kwenye hali mbaya kimaisha, awe na kitu cha kufanya”, alisema Makinda.

Akifafanua hilo alisema siasa siyo kazi ya kudumu kwa sasa, na kwamba hata wale wanaokosa nafasi ya kurudi bungeni kwa awamu nyingine, huwa vigumu kupata ajira kwa kuwa hata waajiri hudai hao ni wanasiasa.

Alisema, ubunge ni kazi ambayo mtu anakuwa na mkataba na wananchi na kwamba kama wananchi wataamua kutomchagua kwa mara nyingine, ndio mwisho wa ubunge hivyo ni vyema kuwa na kazi mbadala kufanya maisha yaendelee.

Alisema ingawa ubunge ni kazi ambayo haina pensheni baada ya mhusika kumaliza kipindi , lakini wanapokuwa kwenye nafasi, fedha wanazopata huzitumia pia kwa ajili ya maendeleo ya majimbo yao.

Mishahara ya wabunge Aidha, alisema ingawa mishahara ya wabunge siyo mikubwa kama ilivyo kwa wabunge wa nchi nyingine, hata kama ikiongezwa haitatosha kutatua matatizo wanayokumbana nayo.

“Wakipatacho mara nyingine hukitumia pia kwenye majimbo yao kusaidia wananchi,” alisema.

Aliongeza, “Kwa kweli tuna changamoto, nafasi ya ubunge haina pensheni mara ubunge unapokoma, tunapata kiinua mgongo, sasa kama mbunge hakuchaguliwa tena kuendelea na nafasi hiyo, kwa awamu nyingine baadhi yao wanakuwa kwenye hali mbaya.” Waomba mshiko Aliongeza,

“hali ni mbaya, wapo wabunge wastaafu unawaona unashituka, wengine wanafululiza hapa unawapa chochote ulichonacho sasa, ili kuondokana na adha hii tunaangalia jinsi ya kuwasaidia kabla ya kumaliza kipindi cha ubunge wawe na kazi au biashara”.

Hata hivyo alisema hivi sasa wabunge wengi ni vijana na kwamba kwa hali halisi ya kazi ya ubunge ni wazi kwamba wenye uamuzi ni wananchi, hivyo ikiwa wanakosa kwa awamu nyingine, na hawana kazi nyingine ya kufanya, hali itakuwa mbaya zaidi.

Akifafanua jinsi watakavyoweza kugawa muda wa ujasiriamali na kazi ya ubunge, Makinda alisema katika programu hiyo wataangalia pia jinsi ya kutenga muda ili kufanya mambo yote kwa ufasaha na umakini. Rafu katika uchaguzi

Akizungumzia uchaguzi Makinda alisema, chaguzi nyingi za ubunge zimekuwa za kufa kupona kwa wagombea kwa kuwa wanafahamu ikiwa watakosa na hawana kazi nyingine, huo unakuwa mwanzo mgumu wa maisha.

“Mnapogombea nafasi ya ubunge kwenye majimbo ya uchaguzi unakuwa wa kufa au kupona kwa kuwa wengi wa wagombea wameacha kazi au hawana kazi na kama watakosa nafasi hiyo basi hapo ndio ugumu wa maisha unaanza”, alisema Makinda.
Kadhalika, alisema ili kuondoa migongano na ugomvi mara baada ya uchaguzi kumalizika, ni vyema wabunge wakafundishwa ujasiriamali ili kama akiwania nafasi na kushindwa kwa haki asiwe na kinyongo na aliyeshinda, bali atafanya biashara kwa kuwa ana elimu au mafunzo.

Spika wa Uswisi ashauri Kwa upande wake Spika wa Uswisi, Maya Graf alisema mfumo wa Bunge la Tanzania na wa kwao hautofautiani kwani wao pia kama mbunge hatachaguliwa kwa awamu nyingine, hufanya kazi nyingine.

“Kwetu kupata kazi sio shida, ukiwania nafasi ya ubunge ukakosa, unaweza kupata kazi kwa kuangalia fani uliyonayo, hii ndio tofauti ya kwenu na kwetu, ila kupata ubunge ni matakwa ya wananchi kama wanakukubali”, alisema Graf.

Aliongeza kuwa ni vyema changamoto hiyo ya ajira au biashara mara baada ya ubunge kukoma ikaangaliwa na kutafutiwa ufumbuzi, ili kuwasaidia wabunge waweze kuendelea na maisha na kuondokana na umaskini.



CHANZO HABARI LEO

No comments:

Post a Comment

POSTED TITLE

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...