Binti wa miaka 17 nchini India katika jiji la Parbhani amejiua baada ya wazazi wake kumkataza asitumia ukurasa wa Facebook ili apate muda wa kuzingatia masomo aliyokuwa akishindwa vibaya darasani tofauti na ilivyokuwa kabla yajaanza kutumia Facebook ambapo alikuwa akifaulu.
Aishwarya Dahiwal alikutwa ananing'inia chumbani kwake baada ya kuzuka mabishano baina yake na wazazi wake ambao
walikuwa wanakerwa na muda mwingi anaoutumia kwenye mtandao wa Facebook na mazungumzo marefu kwenye simu yake ya mkononi.
Gazeti tando la habari za teknolojia, Gawker limeripoti kuwa marehemu aliacha ujumbe usemao kuwa asingweza kuishi bila mitandao ya kijamii na moja ya yaliyoandikwa humo ni pamoja na kuuliza, "Je, Facebook ni mbaya hivyo?" "Siwezi kuishi katika nyumba yenye vizuizi vya aina hii na siwezi kuishi bila Faceboook" na hivyo kuwalaumu wazazi wake kwa hatua ya kujiua aliyoichukua.
Kama ilivyo kwa wazazi wowote ambao kwa kawaida wameyaona maisha na kufahamu mbinu za kukabiliana nayo, walikuwa na nia njema ya kutaka kumsaidia mtoto wao aweze kufanikiwa lakini mabadiliko ya kila kizazi yanayokuja na changamoto zake ambazo hazina vigezo wala vielelezo vya namna ya kumsaidia mtoto akabiliane navyo vyema hali akiyamudu maisha kwa uwiano, walijikuta katika huzuni ya kulazimika kukubaliana na jambo ambalo hawakutarajia lingetokea.
Bila shaka ujio wa internet umebadili maisha ya vijana na familia kwa ujumla. Pamoja na kuwa na faida nyingi kwa wale wanaojua namna ya kuitumia vyema, bado madhara na hasara zake ni kubwa ambazo zinaonekana dhahiri kwenye mahusiano ya aina zote iwe kikazi, kifamilia, kijamii au hata kutoka kwa mtu msiyefahamiana kabisa ila kwa kuwa amekuona kwenye moja ya mitandao ya kijamii, anaweza kukutisha na hata kukudhuru.
Jirani yangu alinisimulia jinsi rafiki yake alivyoibiwa nyumbani kwake baada ya kuandika kwenye ukurasa wake wa Twitter kuwa baada ya uchovu wa kazi wiki nzima, amekwenda kubarizi ufukweni na atarudi majira ya jioni hivi, kwa kuwa anwani yake ilikuwa kwenye wasifu wake (profile details) basi taarifa hizo zikawa maelezo ya kutosha kwa wezi kufanya watakavyo.
No comments:
Post a Comment