Tuesday, September 3, 2013

TUSKER FC YA KENYA KUTUA DAR ALHAMISI HII KWA MECHI YA SIMBA NA YANGA TAIFA



MABINGWA wa Kenya, Tusker FC wanawasili nchini siku ya Alhamisi kwa ajili ya michezo miwili ya kujipima nguvu dhidi ya mabingwa wa Tanzania Bara, Yanga SC Jumamosi na Simba SC Jumapili Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Mechi hizo zimeandaliwa na Chama cha Soka Dar es Salaam (DRFA) na Yanga SC wanataka kuutumia kwa ajili ya maandalizi ya michezo yao ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara wiki ijayo Nyanda za Juu Kusini.
Yanga SC itacheza mechi mbili mfululizo Mbeya wiki ijayo dhidi ya timu za huko, ikianza na Mbeya City Septemba 14 na baadaye Prisons Septemba 18, Uwanja wa Sokoine mjini humo Mabingwa wa Kenya, Tusker FC wanakuja kucheza na Simba na Yanga

Tayari timu ya Yanga SC imecheza mechi mbili za Ligi Kuu msimu huu Dar es Salaam dhidi ya Ashanti United waliyoshinda 5-1 na Coastal Union waliyotoka na sare ya 1-1.
Tusker nayo itautumia mchezo huo kama sehemu ya maandalizi yake ya mechi za Ligi Kuu ya Kenya inayoendelea nchini humo.
Kadhalika Simba SC watautumia mchezo wao na Tusker kwa maandalizi ya mechi zake za Ligi Kuu wiki ijayo.
Baada ya mechi mbili mikoani, Tabora dhidi ya Rhino Rangers waliyotoka nayo sare ya 2-2 na JKT Oljoro waliyoshinda 1-0 Arusha, Simba SC watacheza mechi zaidi ya tano Dar es Salaam kuanzia wiki ijayo, wakianza na Mtibwa Sugar Septemba 14.
Kwa kuwa Tusker ni mabingwa wa Kenya na timu yenye uzoefu wa kucheza Tanzania, wazi Simba na Yanga zitapata mechi nzuri za kujipima.







No comments:

Post a Comment

POSTED TITLE

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...